Ni aibu tunajadili kodi katika taulo za kike

Wasichana wanakosa kwenda shule kwa siku kadhaa kila mwezi kwa sababu ya kukosa kabisa taulo za kike, kuzikosa kwa idadi ya kutosheleza au kutumia mbadala – kama nguo chakavu - kusiowapa stara ya kuridhisha. Wapo pia wanawake huacha kwenda kufanya kazi zao za uzalishaji za kila siku kwa sababu hizohizo.

Wasichana na wanawake wanaojilazimisha kwenda kazini au shule licha ya kutokuwa na vifaa toshelevu na vyenye ubora vya kujihifadhi katika siku zao za mwezi, huwa na siku ngumu na mara nyingi hata ushiriki wao katika aidha masomo au kazi huwa ni dhaifu.

Inakadiriwa kwamba wasichana na wanawake milioni 500 duniani kote wanakosa vifaa vya kujistiri wakati wa siku zao za mwezi, kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Plan International. Bila shaka hali ni mbaya katika nchi za Kiafrika, zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo jamii zake zinakabiliwa na umaskini mkubwa.

Tafiti mbalimbali nilizoziona kuhusu hali ya Tanzania zinaonyesha kuwa katika baadhi ya wilaya hususan zile za vijijini, hadi nusu ya wanafunzi hukosa shule baadhi ya siku wanapokuwa katika vipindi vyao vya hedhi, na pia idadi kubwa ya wanafunzi wanaamini taabu wanayopitia wakati wa hedhi inawarudisha nyuma kitaaluma.

Nchini Uganda, utafiti uliofanywa na Shirika la Build Africa, na kuripotiwa katika mtandao wa Gazeti la Serikali la New Vision, mamilioni ya wasichana wanakosa kwenda shule hadi asilimia 20 ya siku anazopaswa kuhudhuria masomo kwa sababu hawawezi kumudu taulo hizo.

Utafiti huohuo pia unaonesha kuwa, asilimia 25 ya wasichana na wanawake katika maeneo ya vijijini wanatumia nguo zilizochakaa na kuzirejelea tena na tena kwa ajili ya kujistiri wakati wa siku zao za mwezi, huku wengine wakitumia vitu kama majani, tishu, karatasi na mfano wa hivyo kujistiri.

Taulo za kike zisizo na ubora, zinapotumika zaidi ya muda uliopendekezwa na vilevile zile za zinazotumika kwa kurejelewa zimepelekea maambukizo ya maradhi kwa wanawake, baadhi yakiathiri hadi mfumo wa mfumo wa uzazi, kama si kupata maambukizo katika njia ya mkojo au fangasi.

Hizo ni chache kati ya changamoto nyingi wanazopitia wanawake kila mwezi katika vipindi vyao.

Bahati mbaya sana ni kuwa, mapito haya ya wanawake si mambo yaliyo ndani ya uwezo wao kuchagua kuyapitia au la. Ni suala la kimaumbile. Mungu Mwenyezi ndiye aliyeamua kuwaumba hivyo, na tena akajaalia kuwa damu hiyo ya hedhi ina uhusiano na uzazi.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, suala la Serikali kumrahisishia mwanamke upatikanaji wa vifaa vya kujisitiri ni la uchaguzi. Yaani lipo ndani ya uwezo wetu kulifanya au kutolifanya. Ni suala la uchaguzi wa aidha tuwaheshimu, tuwaenzi na kuwatukuza wanawake au tuamue kuwatweza na kuwadhalilisha utu wao!

Kwa jamii iliyostaarabika, inayoelewa heshima ya mwanamke, jawabu ni rahisi. Itachagua kuwaheshimu na kuwatukuza wanawake na kulinda utu na heshima yao. Itachagua hivyo, tena kwa kujivunia, bila kusita wala kupepesa macho kwa sababu jamii husika inatambua thamani ya mwanamke kama mama na mzazi ambaye kila mmoja wetu alitoka tumboni mwake.

Kwa kuelewa hili ndiyo maana nasema, mjadala wa hivi karibuni ulioibuka wa ama msamaha wa kodi katika taulo za kike zinazoingizwa Tanzania uendelee kuwepo au ufutwe (kama ilivyopendekezwa na Serikali) – haukupaswa hata kuwepo. Maana yake ni kuwa, hilo pendekezo la Serikali halikupaswa kuletwa kwenye bajeti kabisa.

Kwanza, kwa asili ya matumizi ya bidhaa zenyewe labda hatukupaswa hata kuziwekea tozo tangu hapo awali. Tusingepaswa kutoza kodi bidhaa hizo si tu kwa sababu ya kutaka kushusha bei bali muhimu zaidi kwa sababu ni ishara ya kumthamini mwanamke. Yaani katika vyanzo vyote vya kodi ili tupate fedha za kuendesha nchi yetu, kutoa huduma za jamii na kutekeleza miradi ya maendeleo tumeona na kodi ya taulo za kike iwemo? Kweli? Mmmh. Hapana.

Kwa hili linaloendelea hivi sasa, nionavyo, hatua ya kutoa msamaha wa kodi kwa bidhaa hizo ilichelewa kuja. Pili, hatua hiyo haitoshi, ilipaswa Serikali ifanye ziada kuhakikisha taulo hizo si tu zinapatikana kwa urahisi, bali hata bure. Kwa mantiki hiyo, huu mjadala haukupaswa kuwepo kabisa.

Naelewa hoja ya Serikali kuwa, msamaha huu haujanufaisha walengwa lakini je jibu ni kufuta huo msamaha kabisa au kutafuta njia ya kuhakikisha wanafaidika? Bahati nzuri majibu juu ya kwa nini msamaha haujawanufaisha walengwa yanajulikana.

Wapo wanaosema kuwa, mwaka mmoja ni mfupi mno kwa athari kuonekana. Sababu nyingine inayotajwa ni kuwa, kumekuwa na vigezo vingine tofauti vinavyoweza kuwa vimepandisha bei, ikiwemo anguko la thamani ya fedha zetu dhidi ya sarafu za kigeni.

Jibu jingine lipo katika namna ya usambazaji wa bidhaa, ambapo kwa sababu muuzaji anazifuata Dar es Salaam yeye mwenyewe anajipangia bei atakavyo tofauti na muundo ambao mwenye bidhaa anamfikishia mnunuzi hadi dukani au walau wilayani. Kuunga mkono hoja hii, baadhi ya watu wanadai taulo hizo zimeshuka bei maeneo ya mjini.

Vyovyote iwavyo, changamoto zilikuwa ni za kuchunguzwa zina ukweli kiasi gani na kufanyiwa kazi ili athari ya kufutiwa kodi bidhaa hii ionekane.

Kwa wanawake wanasiasa ambao waliunga mkono kurudishwa kodi hiyo, ni jambo la kusikitisha. Ujumbe wangu kwao, wasiweke mbele siasa kuliko utu na heshima ya jinsi yao.

Wanapaswa kusukuma serikali ifanye zaidi kuhakikisha afya ya mwanamke katika nyanja ya hedhi na si vinginevyo.