PLO Lumumba na athari za Afrika kutokuungana

Mara baada ya nchi za Afrika kuanza kupata uhuru katika miaka ya 1950 na 60, viongozi wa Afrika walitafakari haja kuliunganisha Bara hilo, hoja hiyo ikitolewa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi akiwemo Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa kwenye mkutano huo uliofanyika Addis nchini Ethiopia miaka 56 iliyopita, walipinga wakitaka kwanza kuwe na muungano wa kikanda, kabla ya kufikia Umoja wa Afrika.

Akitoa mada ya Umoja wa Afrika katika tamasha la Mwalimu Nyerere hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Profesa wa Sheria kutoka Kenya, PLO Patrick Lumumba anasema hilo ni kosa kubwa ambalo Mwalimu Nyerere alikuja kulijutia miaka 40 baadaye.

“Ninavyozungumza sasa, utumwa umerudi tena Afrika, ninavyoongea sasa kuna makumi elfu ya Waafrika wanavuka bahari ya Mediteranea kila mwaka (kwenda Ulaya) ,” anasema Profesa Lumumba.

Licha ya kushindwa kuungana, Profesa Lumumba anasema nchi mmoja moja bila kujali udogo wake zimekuwa zikijitutumua na kujiunga na mataifa makubwa.

“Nchi ndogo yenye Pato la Dola 2 bilioni kwa mwaka nazo zina Rais na Baraza la Mawaziri na Bunge na Rais wa nchi hiyo anaingia kwenye uhusiano na nchi kubwa kama China akisema mataifa yote yako sawa. Huo ni utani,” anasema.

Anasema miongoni mwa sababu za Afrika kushindwa kushindana na mataifa mengine ni udhaifu unaotokana na kugawanywa na Wakoloni, jambo analosema kwa methali ya Kiswahili kuwa ni “Vita vya panzi furaha ya kunguru.”

Huku akionya kuhusu uwekezaji mkubwa unaofanywa na China kwa Bara la Afrika, Profesa Lumumba anasema nchi hiyo imeingia kwa kasi Afrika ikiwekeza katika miundombinu na taasisi za elimu.

“Leo katika nchi za Afrika Wachina ndiyo wanajenga viwanja vya michezo, sijui kwa hapa Dar es Salaam umejengwa na nani, lakini Nairobi, Kenya wamejenga, Uganda na nchi nyingi za Afrika wanajenga.

“Hakuna chakula cha bure, Wachina wameshajua tuna udhaifu na ndiyo maana wanaona njia nyepesi ya kushika ufahamu wetu ni kuwekeza kwenye taasisi za elimu ya juu.”

Kwa suala hilo, Profesa Lumumba anaona nchi hiyo inaelekea hata kupandikiza utamaduni wake kupitia lugha yake inayoelekea kumeza utamaduni wa Afrika.

Akizungumzia umoja wa sarafu ya Afrika Profesa Lumumba anasema umoja huo pia umeshindwa kuwa na nguvu, akitoa mfano wa kuwa na fedha ya pamoja.

“Natoka Nairobi kwa saa 1:05 nikifika Dar es Salaam natakiwa nibadilishe Shilingi ya Kenya nipate ya Tanzania. Natoka Tanzania nakwenda Burundi, natakiwa niwe na Faranga ya Burundi, natoka huko nakwenda Rwanda niwe na Faranga ya huko, Nikienda Uganda niwe Shilingi ya Uganda.

“Nchi zote za Afrika zina fedha yake ambayo hata hivyo haina thamani,” anasema.

Kuhusu demokrasia, Profesa Lumumba anasema nchi za Magharibi zimekuwa zikiifundisha Afrika cha kufanya bila kujali utawala uliokuwapo.

“Nakumbuka wakati Dola ya Urusi ikisambaratika, tuliambiwa kupitia asasi za kiraia kuwa demokrasia maana yake muwe na vyama vingi, ukiangalia kwa mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina vyama 233, kiasi kwamba ukiangalia karatasi ya kupigia kura ni ndefu kama wewe.

“Wakasema demokrasia ni lazima muwe na uchaguzi kila baada ya miaka mitano. halafu mkifanya uchaguzi, Umoja wa Ulaya ndiyo unakuja kukagua. Halafu wanatoa ripoti ya orodha ya nchi zenye demokrasia,” anasema.

Pamoja na Afrika kushindwa kuungana na kuwa Taifa moja kama anavyosema Lumumba, bado mataifa hayo yalifanikiwa kuunda umoja wao wa nchi huru za Afrika (OAU) ambao ulibadilishwa kuwa Umoja wa Afrika (AU)

Licha ya kufanikiwa katika malengo yake ya kuleta uhuru kwa nchi wanachama, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete anaona bado una changamoto kubwa tatu za kukosekana kwa utawala bora, umasikini na magonjwa.

Kikwete ambaye pia ni mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam anasema licha ya kuwepo juhudi chanya za viongozi wa Afrika kuonyesha ubunifu wa mipango ya maendeleo, bado kuna tatizo la utawala.

“Kumekuwa na changamoto zinazohitaji kuangaliwa ambazo ni kuwepo kwa sheria kandamizi, ushiriki usioridhisha wa wananchi, kutokuwepo kwa uhuru wa habari na kutokuwepo kwa mikakati ya kupambana na rushwa,” anasema Kikwete katika siku ya kwanza kongamano hilo la siku tatu.

Anaongeza, “Kama watu wa Afrika hatuna njia nyingine bali kutatua hizi changamoto za utawala kama zilivyoelekezwa.”

Pamoja na hayo, Kikwete anasema Bara la Afrika bado linatawaliwa na umasikini akisema kati ya nchi 27 zilizo masikini zaidi duniani, 25 ni za Bara hilo.

Nini kifanyike?

Mbali na wachokoza mada, mjadala mzima unaibua sauti za watu mbalimbali wenye mitazamo tofauti kuhusu Afrika.

Miongoni mwa wanapaza sauti zao ni mfanyabiashara Ally Mufuruki anayewakosoa wanasiasa wanaotumia jina la Mwalimu Nyerere kupiga siasa.

Mufuriki anasema alipata fursa ya kusafiri na Nyerere kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 1995, na alipomsikiliza alibaini kwamba alikuwa ameshabadili mtazamo wake kuhusu siasa na uchumi.

“Mwalimu mara nyingi anatumika kama kisingizio cha kuendeleza siasa ambazo zilishashindwa za mwaka 1967, ambazo mwenyewe alisema zimeshindwa,” anasema Mufuruki.

“Wapo vijana wengine ambao hata hawakuwepo wakati Mwalimu akiwa serikalini, lakini utawakuta kama wakisema ‘kama mwalimu alivyosema’. Si kweli, kwa sababu (mwalimu) alishabadili mtazamo. Alikuwa na akili na mtu mwenye akili lazima akubali kubadilika,” anasema Mufuruki

Alisema kama Mwalimu Nyerere angekuwapo leo angetaka tujadili athari za siasa za ukweli kwa uwazi.

“Hata kama ingekuwa ni kumkosoa, Mwalimu alikuwa intellectual (msomi), haogopi kuwa criticized. Intellectual haogopi kusema kuwa amekosea. Wasomi wamekuwa wakisema matatizo tuliyonayo katika kuendesha nchi yametokana na sera mbovu za IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) na WB (Benki ya Dunia), wanasema Sera za kibeberu.

“Inaweza kuwa kweli, lakini tusiishie hapo. Mimi nakataa, kwa sababu IMF kazi yao ni kusaidia kukwamua nchi zilizokwama na madeni,” alisema.

Anasema mpaka mwaka 1980 Tanzania haikuwa na shida ya kusaidiwa na IMF na WB, lakini uchumi wetu uliporomoka kwa kasi na ikafika mahali nchi ikaomba WB na IMF waje kusaidia kupanga uchumi.

“Sasa kama walitushauri kwamba mbinafsishe viwanda, Serikali iache kufanya hivi, na sisi tukatekeleza, kwa nini tulaumu?” alisema.

Badala ya kulalamika, Mufuruki anaishauri Dola kuipa nguvu sekta binafsi ili iwe na nguvu katika soko ili iweze kuinua uchumi wa nchi.