Pinda ataka viongozi wa dini wahusishwe katika migogoro

Sunday December 1 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda amesema viongozi wa dini wakishirikishwa katika matatizo makubwa wanaweza kusaidia kuyamaliza kutokana na nafasi yao katika jamii.

Pinda, ambaye alitoa mifano ya matukio mawili yaliyomsumbua wakati wa uongozi wake wa miaka minane, alikuwa akizungumza jijini Mwanza juzi wakati wa kikao cha kusaini maazimio baina ya Serikali na viongozi wa dini kuhusu mapambano dhidi kifua kikuu.

Pinda alisema mambo hayo mawili, ambayo ni mauaji ya albino na mgogoro wa kugombea kuchinja mifugo, yalikuwa magumu kwa Taifa, lakini yalimalizwa kwa mashauriano na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Pinda aliwaambia washiriki wa kikao hicho kilichoandaliwa na Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Kifua Kikuu kuwa nguvu na ushawishi wa viongozi wa dini katika jamii ikitumiwa vema huweza kuvusha Taifa kwenye mambo magumu.

“Tulipopata tu janga la mauaji ya walemavu wa ngozi nilikuja Kanda ya Ziwa kukutana na viongozi wa dini pamoja na watendaji wa Serikali. Tuliwaambia viongozi wa dini kuwa chondechonde mkatusaidie jambo hili liishe. Leo hii mtu akiniuliza ‘kulitokea nini’, mimi nitamwambia sijui. Ila ninachojua mauaji hayo hayapo,” alisema Pinda.

Wakati huo, Pinda alipitia kipindi kigumu baada ya kuwaambia wananchi mkoani Tabora kuwa wawaue watu ambao wangewaona wakiwachinja walemavu wa ngozi, au albino kwa ajili ya kuchukua viungo vyao.

Advertisement

“Mkimuona mtu anamkata mwingine shingo, naye muueni kwa kuwa sasa viongozi wote tumechoka. Hakuna zaidi, siwezi kuvumilia zaidi,” alisema Pinda akisisitiza kuwa kuwapeleka mahakamani ni kuwachelewesha.

Lakini siku chache baadaye akabanwa bungeni kuhusu kauli yake kuonyesha kutoheshimu utawala wa sheria, ndipo alipoomba radhi kwa kauli hiyo huku akibubujikwa na machozi.

Pinda pia alizungumzia mgogoro wa kuchinja mifugo ulioibuka wilayani Tunduma ambao ulisababisha wananchi waandamane.

“Ukatokea mtafaruku mwingine wa nani achinje na nani asichinje kati ya Waislamu na Wakristo. Kha! Pale nikaona uwaziri mkuu ni mchungu kwelikweli. Lakini tulichukua mtindo huuhuu wa kuwaita na kuzungumza na viongozi wa dini na kukaa pamoja,” alisema.

“Nakumbuka nilienda na Geita tukaitisha kikao cha viongozi wa madhehebu ya dini, tukajaribu kuwaelewesha vizuri sana, Mungu ni mwema jambo hilo nalo likaisha, wote tukabaki kuulizana tukisema kulitokea nini?”

Mgogoro huo wa kuchinja ulidumu kwa takriban siku tatu baada ya wananchi kutoridhishwa na ushauri wa mkuu wa mkoa wa wakati huo wa kuwataka wasubiri ufumbuzi wa tatizo na hivyo kuhamasishana kuandamana na kuchoma matairi mitaani hadi polisi walipowatuliza kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Katika vurugu hizo walikuwemo pia viongozi wa kidini.

Pinda alisema kwamba matukio hayo mawili na mengine mengi yaliyowahi kutokea nchini ni uthibitisho kuwa viongozi wa dini wana nguvu na ushawishi katika jamii kutokana na imani ya waumini kwao na wakitumika vema wanaweza kusaidia kutatua mambo mengine kwa faida, maendeleo na maslahi ya Taifa.

“Ukaribu wao na Mungu na ushawishi wao kwa jamii unawafanya viongozi wa dini kubeba kundi kubwa la Watanzania wanaowaamini na kuwasikiliza sana. Hata katika hili la kupambana na kifua kikuu watatuvusha,” alisema Pinda maarufu kama ‘mtoto wa mkulima’.

Aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii kupambana na maadui watatu, ujinga, maradhi na umaskini kufanikisha mpango wa kuwa na Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Ukitangaza vizuri gonjwa hili linaloitwa TB na utapiamlo utavihusisha na maadui watatu waliotajwa na Baba wa Taifa,” alisema.

Advertisement