UCHAMBUZI: Polisi wanakwama wapi kuzuia, kupeleleza utekaji?

Kuna wakati yatupasa kuwa wakweli, tena wakali kwa faida ya Watanzania na usalama wao.

Ukweli huo ni kwamba Jeshi la Polisi halionyeshi mafanikio ya haraka na ya kutia moyo katika kuzuia na kupeleleza matukio ya utekaji nchini.

Matukio ya watu kutekwa yanaendelea kuripotiwa siku hadi siku. Nasikitika kusema, Tanzania sasa imekuwa maarufu kwa ripoti hizo.

Wanaofanya matukio hayo, labda wameona udhaifu wa wale waliopewa jukumu la kulinda raia na mali zao, ndiyo maana wameigeuza nchi yetu kuwa chaka la watekaji.

Hakuna ajuaye kesho na keshokutwa itakuwa zamu ya nani. Na bahati mbaya watekaji hawashikiki, hawaonekani wala hawajulikani.

Wamekuwa mizimu ya kuteka mchana na kuachia usiku bila kunaswa. Wanaharibu taswira ya Tanzania ya ndani na nje.

Ajabu ni kwamba, matukio makubwa kama mauaji ya Kibiti, katika Mkoa wa Pwani yamedhibitiwa, lakini hili la utekaji bado limekuwa kitendawili.

Hivi karibuni, Mkenya Raphael Ongangi, rafiki wa mwanasiasa wa upinzani Zitto Kabwe alidaiwa kutekwa akiwa maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam. Baada ya siku kadhaa aliachiwa akiwa Mombasa.

Hilo tukio liweke upande wowote utakao, ama kajiteka mwenyewe kama wanavyosema baadhi ya watu au katekwa. Upande wowote utakaoliweka, utagundua bado linathibitisha kuna jambo haliko sawa katika kushughulikia kadhia hii.

Swali ni vipi mtu atekwe Tanzania kisha apitishwe mpakani ambako vikosi vyetu vya usalama havilali kuilinda mipaka?

Pia, Zitto alitoa hadi namba za gari ambayo inatuhumiwa kumteka. Ila hakuna taarifa ya polisi iliyoeleza juu ya mmiliki wa gari hilo au raia kuombwa kusaidia kupatikana kwake au gari lenyewe.

Hata likiwa la kupangwa bado linaharibu taswira ya nchi, inakuwaje polisi washindwe kuzuia watu au matukio yanayoharibu taswira ya nchi?

Kana kwamba haitoshi, Allan Kiluvya, msaidizi wa Bernard Membe, waziri wa zamani wa mambo ya nje, naye ilitolewa taarifa za kutekwa.

Familia ilitaja hadi namba za gari ambalo linatuhumiwa kumteka, lakini polisi hawatoi majibu kuhusu uchunguzi wao.

Ukirudi nyuma, kuna suala Mohamed Dewji ‘Mo’ aliyetekwa kisha akarudishwa katikati ya jiji la Dar es Salaam, maeneo ya Gymkhana usiku wa manane, nayo polisi walikuwa kimya hadi ilipoingiliwa na Rais John Magufuli ndipo ikafufuka. Hata suala la Abdul Nondo ambaye polisi walisema amejiteka, alipopelekwa mahakamani, alishinda kesi.

Itoshe tu kusema, matukio haya, yawe ya kujiteka au kutekwa, bado yanadhihirisha udhaifu wa Jeshi la Polisi. Na huo ndio ukweli usiohitaji kumung’unya maneno.

Si tu kwamba wanashindwa kutoa majawabu, pia kuna kauli za kutatanisha wanazozitoa mbele ya vyombo vya habari kuhusu matukio husika.

Mathalan, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa anashangaa Ongangi kutekwa Tanzania na kupelekwa Kenya.

Kiukweli hakuna jambo la kushangaa hapo. Mshangao wake bado hautoi majibu ambayo Watanzania wanayataka.

Ikiwa kajiteka waambie Watanzania alisafiri vipi hadi Kenya wakati hapa imeshangazwa katekwa. Alipitaje mpakani wakati vyombo vya dola vina taarifa yuko mikononi mwa watekaji, pasipoti yake iligongwa kama kawaida?

Ama ikiwa katekwa, ni kwamba waje na jawabu kapitishwaje mpakani? Watekaji ni akina nani? Gari inamilikiwa na nani? Hayo ndio maswali yanayohitaji jawabu kuliko mshangao wake.

Tukio la kutekwa Allah, Mambosasa pia anasema taarifa za mtekwaji na familia yake hazifanani, yaani zinatofautiana. Bahati mbaya hakusema ni taarifa gani.

Bado kauli ya Kamanda haijakata kiu ya maswali. Kuna maswali mengi yasiyo na majibu katika kesi hizi zote. Hivi ni lazima katika upelelezi kauli zote zifanane? Zikitofautiana upelelezi unakoma?

Tuwaache waendelee kuchunguza, lakini kauli hizi za kamanda mbele ya kamera na vinasa sauti zisifanywe kuwa ndio jawabu la mwisho katika mambo haya.

Matukio haya yanaharibu nchi, yanatia hofu raia. Hasa hivi yalivyokaa kisiasa siasa. Polisi ina wajibu wa kuyazuia na kuja na wajawabu yanayoingia akilini.