HOJA ZA KARUGENDO: Siasa zinabariki ardhi kama bidhaa nyingine?

Wakati uporaji wa ardhi unaendelea na sisi tunakubali kuifanya kuwa bidhaa sokoni, Watanzania tunaendelea kuongezeka kwa kasi.

Ni wazi tutahitaji ardhi kwa ajili ya chakula, makazi na matumizi mengineyo ya kijamii na kiuchumi na kijamii. Uporaji ukiendelea bila kukomeshwa, miaka michache ijayo tutaanza vita vya kugombe ardhi.

Ikifika wakati hakuna ardhi na jirani amelimbikiza ardhi kiasi asichohitaji, kama hakuna njia za amani kuipata ardhi hiyo, hapo si rahisi kukwepa damu kumwagika.

Nchi zinazotuzunguka, zinapigania ardhi. Kwa vile imegeuzwa bidhaa, ni tatizo kwa mtu wa kawaida kupata kiwanja cha kujenga nyumba kwenye miji yetu mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Wawekezaji wanahitaji ardhi kujenga nyumba za kukodisha, maduka, shule, hospitali, hoteli na viwanda. Wako tayari kulipa fedha nyingi. Hivyo mtu masikini hawezi kumudu kushindana na mabwana hawa.

Tunapotaka mabadiliko, ni lazima tuliangalie suala zima la haki ya kumiliki ardhi kwa umakini mkubwa. Hatuwezi kuleta mabadiliko wakati tunakubali kuweka ardhi yetu sokoni kama bidhaa nyinginezo.

Mwalimu Nyerere, alikataa kuifanya ardhi bidhaa kama vile shati, kwa hofu kwamba kwa kufanya hivyo wenye fedha wangeweza kuinunua yote na masikini wakabaki bila ardhi.

Baada ya Uhuru ardhi ilitambuliwa kisheria kuwa mali ya umma.

Wakati wa ukoloni ujenzi wa makazi kwenye miji yetu mikubwa ulizingatia matabaka. Sehemu nzuri walijenga Wazungu na hadi leo panaitwa Uzunguni.

Sehemu zenye ubora wa kati walipewa Wahindi na hadi leo panajulikana kama Uhindini na sehemu zisizo na huduma muhimu za kiuchumi na kijamii walijenga weusi na kupaita Uswahilini na hadi leo hii sehemu hizi ziko nyuma kimaendeleo.

Sheria na sera zetu zinasema ardhi ni mali ya umma, lakini hali halisi ni kwamba ardhi ni bidhaa iko sokoni na bei yake inapanda kama bidhaa nyinginezo zenye umuhimu mkubwa kiuchumi. Hivyo watu masikini wa Tanzania hawawezi kumiliki ardhi. Wenye mamlaka na fedha ndiyo watamiliki ardhi na kufanya maamuzi ya matumizi ya ardhi.

Hali halisi ni migogoro mikubwa ya ardhi. Na mingi ya wakubwa kuvamia ardhi ya wenyeji, wawekezaji kununua ardhi bila kuwashirikisha wananchi au kuwalaghai, wafugaji kuvamia ardhi ya wakulima na wakulima kuvamia ya wafungaji.

Tunahitaji mfumo wa siasa unaotambua kwamba ardhi ni uhai, uhuru, uchumi, umoja na amani. Tuwe na viongozi wa kutambua kwamba bila kulinda haki za ardhi za raia hakuna demokrasi ya kweli, kwamba nchi ikishindwa kulinda ardhi yake inakuwa imeshindwa kulinda uhuru wake.

Tunahitaji viongozi wa kutengeneza mfumo wa kutekeleza sera isemayo kwamba ardhi ni mali ya umma na kuhakikisha kwamba nguvu za kumiliki na kudhibiti matumizi ya ardhi iko mikononi mwa wananchi; kwenye vyombo vya serikali za mitaa.

Ili kuilinda ardhi ni lazima kuwepo na mfumo wa kidemokrasia ili wananchi wawe na nguvu za kuamua juu ya matumizi bora ya ardhi.