SIASA ZA KITAA: Siwezi kumshangaa meya wa Arusha kuhama Chadema

Wednesday November 27 2019

 

By Dk Levy

Hawawezi kuwa wazi kwenye hili. Lakini huu ndio ukweli. Kwamba ndani ya Chadema kuna mdudu mbaya wa kila mtu kutaka nafasi ya uongozi. Wameachana na mizuka ya kuitana kamanda, sasa wengi wanataka kuitwa bosi au mheshimiwa. Huu ndio ukweli na ndio chanzo cha haya yote.

Unaweza kuuliza, mbona wanaohama wengi ni watu wenye nafasi ndani ya chama? Pia, jiulize huko wanakohamia wanakuwa wanachama wa kawaida? Na pia jiulize wanaohamia huko mbona ni viongozi na si wanachama na wafuasi wa kawaida? Chadema ya 2015 kwenda 2020 ni yenye tamaa na hamu ya uheshimiwa.

Maendeleo popote huja kama mafuriko. Kwa maana kuwa mafuriko husomba vitu vizuri na vichafu. Na hata ukuaji wa chama ni kama mafuriko. Husomba watu wenye nia ya dhati ya kuwatumikia watu. Na husomba watu wenye nia ya dhati ya kujitajirisha wao binafsi kupitia siasa. Hatua hii CCM wameshaivuka kitambo. Sasa ni kwa watu wa Chadema. Kuanzia wabunge, viongozi wa chama, wanachama na wafuasi wao, wengi wao wanatamani kuwa watu fulani ndani ya chama. Watu wanataka kuingiza pesa kwa uongozi wa siasa zetu. Na si kupata pesa kwa ubora wa siasa zetu. Hili ndilo linaloendelea kwenye siasa zetu.

Fungu ambalo mbunge angetumia kwa miaka mitano jimboni na kumsaidia kurudi bungeni bila presha, sasa analitumia kwa watu wake wachache ili arudi tena. Wengi wao wanatumia nafasi hizi kujinufaisha binafsi zaidi. Sayansi ya siasa imewapita kushoto wanasiasa wetu.

Walioshindwa kutumia nafasi zao vizuri kwa miaka minne. Ndiyo unawasikia wanaunga mkono juhudi. Kwa sababu hawakubaliki tena maeneo yao kwa uzembe wao wenyewe. Lakini, si kwa sababu wanazozieleza wao.

Kuunga juhudi za Mzee Baba, ni kufanya kazi kwa bidii. Kutotoa wala kupokea rushwa. Kuheshimu watu, kuamini binadamu wote ni sawa, kulinda rasilimali za taifa. Lakini, kuacha kazi ili upewe kazi hiyohiyo, kwa ahadi ambazo mtoa ahadi anatumia pesa za walipa kodi haohao, ni ngumu kusamehewa. Mungu ni mwema. Jilinde.

Advertisement

Siwezi kumshangaa Meya wa Arusha. Ndivyo ambavyo sikushangaa mwanamama Anna Mghwila, David Kafulila, Julius Mtatiro, Mwita Waitara, Mtolea, Molel, Machali na wengine. Siasa ni kitu kigumu sana wakati huu. Ni wakati muafaka wa kuangalia njia mbadala ya kuendesha wanachofanya sasa.

Advertisement