Tunahitaji nini kati ya ujuzi na ujasiriamali?

Jumapili iliyopita niliibua mjadala kuhusu hali halisi ya uwepo wa digrii nyingi sana mitaani ambazo hazina tija yoyote.

Nilisisitiza kuwa ni muhimu sasa taifa letu likawekeza nguvu kwenye ujuzi wa vijana ili hata kama wanakwenda na kupata digrii wawe pia wamepitia kwenye vyuo vya ufundi na kujifunza ujuzi fulani ambao unaweza ukawa mbadala wa kazi ya kuajiriwa pindi wanapokosa ajira hizo rasmi.

Nilikwenda mbali nikazungumzia dhana ya uanzishwaji wa vyuo vya ufundi vya kila tarafa nchi nzima, niliijenga hoja hii kwa kutumia uzoefu wa uwezo wa nchi yetu kufanikiwa kujenga shule za sekondari katika kata zote. Msingi wa hoja yangu umerudi tena wiki hii baada ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji mbalimbali waliomo kwenye sekta inayohitaji ujuzi dhidi ya ile inayohitaji njia za ujasiriamali wa kawaida, ambao unaweza kujumuisha ujuzi na mtaji.

Kimkakati, ujasiriamali kwa maana yake halisi unaegemea zaidi kwenye mtaji na mjasiriamali mwenyewe, unagusa kidogo eneo la ujuzi.

Ujasiriamali ndiyo msingi?

Tanzania ifanye nini kuondoa lindi kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana hasa wanaomaliza digrii na kurejea mtaani? Je, inahitaji kuwafanya vijana hawa kuwa wajasiriamali? Au inahitaji kuwa na vijana wengi wenye ujuzi?

Rafiki yangu mmoja ameniletea barua pepe, akikubaliana kidogo na dhana ya kupigia chapuo ujuzi lakini akiikosoa dhana kuwa mataifa kama Tanzania yanahitaji kuwekeza zaidi kwenye shughuli za ujasiriamali (nguvu kazi na mitaji) kuliko kuwekeza kwenye ujuzi pekee (nguvu kazi).

Jamaa ameniletea hoja nyingi za kuchachafya mjadala huo na kuweka tafiti nyingi zinazoonesha kuwa ni bora kuwekeza kwenye ujasiriamali kuliko kitu kingine chochote kama utegemezi wa ujuzi.

Jamaa huyo amepingwa na wengine kadhaa ambao nao waliniletea ujumbe mbalimbali wakiunga mkono au kupinga hoja ya kuwekeza kwenye ujuzi na vyuo vya ufundi kila tarafa.

Kama ujasiriamali ndiyo msingi, ninalo la kuongeza, itatupasa tuendelee na mpango wa vyuo vya ufundi kwa kila tarafa na kutengeneza mafundi mchundo wengi kwa kadri tuwezavyo na bila kujali elimu yao, na kisha mafundi hawa bado wakawa na chaguo la kutumia digrii zao, ufundi wao au kuvitumia vyote viwili kufanya ujasiriamali mkubwa.

Haya niyasemayo yanawezekana, si lazima tukafuata tafiti zinazoonyesha kuwa kiini cha utatuzi wa suala la ukosefu wa ajira kwa vijana wasomi ni ujasiriamali.

Digrii, ujuzi na ujasiriamali

Muungano huu ni wa kipekee na unaweza kutumika Tanzania. Tukawa na vyuo vya ufundi vya kila tarafa vikifundisha fani mbalimbali na walimu wake wakiwa ni walewale mafundi mashuhuri ambao watatuzalishia mafundi wengi vijana ambao wataendelea kubaki vyuoni na kufundisha.

Tukawa na vijana wanaohitimu darasa la saba hadi vyuo vikuu; katika ngazi yoyote ya uhitimu, vijana wetu watakiwe kuamua muda wowote, ikiwa wanahitaji, kujiunga kwenye vyuo vya ufundi vya tarafa.

Vijana waliohitimu darasa la saba walio na sababu za msingi waruhusiwe kujifunza ufundi pia, lakini msingi wa ufundi wetu uwe na elimu ya chini ambayo inapaswa kuwa kidato cha nne.

Vijana wetu wanaweza pia kujengewa uwezo wa namna ya kuhimili shughuli za ujasiriamali kwa kutumia ujuzi na elimu zao na tukajikuta tuna taifa ambalo mambo yote matatu yanafanyika kwa wakati mmoja.

Tukikariri kuwa ujasiriamali ni kila kitu, bado tutawapoteza vijana wengi ambao wana kasumba kuwa ujasiriamali ni mtaji. Tuanze kuwajengea uwezo watambue kuwa ujasiriamali ni matumizi ya kipaji na ujuzi pia, wafundishwe kuwa ufundi mchundo ni ujasiriamali bora, usiohitaji fedha za mtaji isipokuwa nguvu kazi peke yake.

Mchanyato ujengewe misingi

Ili mchanyato wa digrii, ujuzi na ujasiriamali ufanye kazi kwa uhakika, ni lazima ujengewe misingi ya kimitaala na utashi wa kisiasa.

Yako mambo yanaweza kuingizwa kwenye mtaala wetu bila tatizo, masuala ya elimu ya ujasiriamali na nidhamu zake yanaweza kufundishwa tangu elimu ya msingi.

Sijui kama vyuo vya ufundi ni suluhisho, sijui kama ujasiriamali ni suluhisho, siamini kuwa digrii nyingi sana za wanafunzi wetu zinatoa msaada kwao na kwa taifa, naamini tunahitaji mjadala mkubwa kuhusu mfumo wetu wa elimu, ajira, ujuzi na maamuzi ya kisiasa.

Julius Mtatiro ni nchambuzi wa masuala mbalimbali +255787536759; Barua Pepe; [email protected])