Tushike lipi kwa hili la sare za jeshi la polisi?

Wednesday May 15 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alitoa kauli inayoibua maswali pale alipodai kuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ni muongo mkubwa.

Kiini cha kauli ya Lugola ambayo aliitoa bungeni ni taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG na kubaini manunuzi hewa ya sare za polisi zenye thamani ya zaidi ya Sh16 bilioni.

CAG anasema mkataba wa kununua sare hizo za polisi ulisainiwa Novemba 2, 2015 kati ya Katibu mkuu wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi na mzabuni aliyetajwa ni Daissy General Traders.

Katika kufanya ukaguzi huo aliomba nyaraka mbalimbali kutoka kwa kampuni hiyo ambazo ni pamoja na hati ya kupokelea shehena, hati ya madai, orodha ya mali zilizopo melini na cheti cha ukaguzi.

CAG hakuishia hapo akaenda kuuliza Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi ambapo mzigo huo ulipaswa kufikia huko, majibu aliyopewa ni kwamba hakuna mzigo wowote uliopokelewa.

Haikutosha, akaenda bandarini katika Mfumo wa forodha (Tancis) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao taarifa za mzigo uliotoka au kushushwa bado hakuona mzigo wowote.

Ripoti hii ambayo ndio inabamba mitandao ya kijamii kwa sasa ndio iliyomsukuma Lugola aliyewahi kuwa ofisa wa polisi, kumshambulia CAG kwa kiwango cha kumdhalilisha kuwa ni muongo.

“Sijawahi kuona mtu muongo kama CAG katika nchi ya Tanzania. Haiwezekani sare zinadaiwa kuwa hewa,” alisema Waziri Lugola kwa ukali akiwa bungeni na kuongeza kusema;-

“Mimi waziri ambaye nimekwenda kwenye makontena na magodown (maghala) ya jeshi la polisi ambapo nimekuta sare nyingi ambazo zimeletwa, halafu CAG anapeleka taarifa ya uongo kwa Rais.”

Lakini, asichokijua Lugola ni kwamba hoja ya ufisadi katika sare za polisi aliyeanzisha ni Rais mwenyewe mara tu alipoingia madarakani na ni moja ya mambo yaliyoelezwa kumchefua.

Aprili 16, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali na wakuu wa vikosi kilichofanyika Dodoma, aligusia ufisadi huu.

Rais hakuishia hapo, Julai 2016 akizungumza wakati wa hafla ya kula kiapo cha utumishi wa umma kwa maofisa wa polisi waliopandishwa vyeo, alizungumzia kwa ukali kuhusu suala hilo.

“Nina uhakika Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo (Mwigulu Nchemba), IGP (Inspekta Jenerali) na Katibu mkuu mmelisikia. Ninategemea siku moja wahusika watapelekwa mbele ya haki,” alisema Rais.

Hakuna hatua iliyochukuliwa na baadaye akamwondoa Nchemba na kumteua Lugola na Rais alieleza waziwazi mambo 13 yaliyomfanya amwondoe Mwigulu kuwa mojawapo ni hilo la sare.

Wakati akimwapisha Lugola, moja ya majukumu aliyompa ni kwenda kushughulikia ufisadi huo, lakini leo Lugola ameshasahau kuwa moja ya mambo aliyotumwa kuyashughulikia ni hilo.

alisema Rais.

Sasa leo miaka mitatu kupita tangu CAG akague maghala hayo ya polisi na wahusika kumweleza sare hizo hazikupokelewa, anataka CAG akakague sare, hivi zilikuwa zinafanya nini miaka yote hiyo?

Kichekesho cha karne ni kwamba Kangi amesahau hata katibu mkuu wake, Meja Jenerali Rwegasira alishanukuliwa na gazeti moja akisema inavyoelekea hata hiyo kampuni yenyewe ni hewa.

Advertisement