Tuwaache kubughudhi wataalamu wazalendo

Wednesday October 23 2019

 

By Salim Said Salim

Huwa nafarijika na kufurahi ninaposikia viongozi wa Serikali ya Zanzibar wanasisitiza umuhimu wa kuwa na wataalamu wazalendo badala ya kuwa tegemezi kwa wataalamu wa nchi za nje.

Lakini, nikishapata furaha hiyo hubaki kujiuliza swali, haya yanatamkwa tu au yamewekwa mazingira mazuri yanayopelekea kujitolea kwa vijana wetu kutumikia nchi yao kunathaminiwa?

Yapo mambo yaliyowakuta wataalamu wa Zanzibar ambayo yalikirihisha na kila pakichomoza juhudi za kuyarekebisha haichukui muda utaona yanarudiwa kama vile matokeo ya zamani hayajatupa mafunzo.

Hivi karibuni nilimsikia Makamo wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alipozungumza katika sherehe za kutoa vyeti na zawadi kwa wanafunzi wa Chuo cha Kiislamu kilichopo Micheweni, Pemba juu ya umuhimu wa kuwa na wataalamu wazalendo watakaoitumikia nchi yao.

Lakini, ninaamini SMZ haijachukua hatua madhubuti ili wataalamu wa visiwani waone elimu na ujuzi wao unathaminiwa.

Watu hawa wanachotaka ni ujuzi wao kutambulika na kuutumia kwa mujibu wanavyoona sahihi na wanaaka ni kuthaminiwa (si kuabudiwa).

Advertisement

Lazima niseme wazi ninaona kukosana kwa hilo ndio kulikopelekea wataalamu wengi wa Zanzibar kwenda kufanya kazi nje na wengine kuacha kufanya kazi za fani walizosomea na kuingia katika siasa kwa kuona watapata masilahi mazuri na wanathaminiwa.

Huu ndio ukweli, Bara na Visiwani. Ndiyo maana tunaona wasomi waliobobea wa fani mbalimbali huacha kufanya kazi walizosomea na kuingia katika siasa.

Hii inatokana na wengi kuona huko kuna tonge zito na la kuvutia kuliko malipo ya mkia wa mbuzi wanayopata wakibaki katika serikali kufanya kazi za taaluma walizozisomea.

Kinachowakera zaidi wataalamu wetu wa nyumbani ni kuingiliwa katika utendaji wao wa kazi na wana siasa na kupewa maelekezo wanayoyaona na kuamini ni kinyume na utaalamu wao.

Siku moja nilishangaa kuona mwanasiasa ambaye uelewa wake wa tiba ni hohehahe kama mimi anawaelekeza madaktari na wauguzi mpangilio wa kutoa tiba na hali ya chumba cha maabara ya hospitali iwe vipi.

Ninawajua watu walioitwa na kupokelewa kwa furaha vifijo na vigelegele kutoka Bara na nje kuja kufanya kazi Zanzibar na kupewa nafasi kutumia ujuzi wao, lakini baada ya muda mfupi tukaona thamani na heshima wanayopata hailingani hata kidogo na wanayopewa huko walikotoka.

Watu hawa siku hizi wanazungushwa kama pia. Kwa kupewa uhamisho kila baada ya muda mfupi kabla hawajazoea mazingira ya sehemu waliopelekwa kutumia ujuzi wao kishada kinachotakiwa kupata eneo lenye upepo mzuri kukirusha.

Wengine hivi sasa wamegeuka kama makarani wa kawaida katika baadhi ya ofisi na mashirika ya umma wakati walipokuwa huko walikuwa na mamlaka na madaraka yanayotambulika.

Hali kama hii inaumiza kifikra na kupelekea huyo mtaalamu si tu kuvunjika moyo, bali hata kujutia uamuzi wake wa kurudi nyumbani kutumikia jamii yake.

Baya zaidi watu ambao hawana nia njema na maendeleo ya nchi hii hufurahia na kuwaambia hao wanaopata mitihani kama hiyo… “Si tulikwambia, baki hukohuko. Sasa unamlaumu nani?”

Matokeo yake ni kuona baadhi ya sehemu zinaongozwa na watu ambao uwezo, ujuzi na ubunifu wao wa kikazi ni mdogo au songombingo.

Naelewa wapo ambao ukiyasema haya hununa na kuvimba kwa sababu wamejijengea dhana ya kwamba ukishapewa nafasi ya uongozi unakuwa na haki ya kujifanya mtaalamu wa kila jambo na kuwaongoza na kuwaburuza wataalamu.

Nawaomba wale wanaowadharau wataalamu wajitafutie nafasi kusikiliza wimbo maarufu wa taarab usemao…‘Nipeni nafasi nimsifu mpenzi wangu.’

Wakishasikiliza watafakari ujumbe anaotoa mwimbaji wa kutaka aachwe apumue afurahie maisha yake na kujifunza kwa kuamua na wao kuwapa nafasi wataalamu kutumia ujuzi wao katika fani mbalimbali.

Uongozi ni kuonyesha njia sahihi na si kujivisha kilemba cha ukoka cha utaalamu na joho la ujuzi wa mambo ambayo wenzako wamechukua miaka

kuyasomea na kuyafanyia kazi.

Tujifunze kuheshimu mgawanyo wa kazi kama mwili wetu unavyotuonyesha kwa kila kiungo kufanya kazi yake na si kuingilia kazi ya mwenzake.

Advertisement