Unyerere, Unkrumah kuhusu Afrika, usife

Sunday July 7 2019Julius Mtatiro

Julius Mtatiro 

By Julius Mtatiro

Bila shaka, ziara ya hivi karibuni ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kumtembelea Rais John Magufuli nyumbani kwake Chato, pamoja na masuala mengine ilikuwa pia na lengo la kurekebisha hali ya hewa ya mahusiano ya nchi zetu mbili hasa baada ya mbunge mmoja maarufu nchini Kenya kuhamasisha Watanzania wafukuzwe nchini Kenya na kutoa saa 24 kwa ajili hiyo.

Kidiplomasia kwa wasiojua, kauli ile ya mbunge iliyosambaa sana kila mahali ilikuwa na maana kubwa na iliipasa serikali ya Kenya iifafanue na kuijulisha Tanzania kuwa uongozi wa kiserikali wa Kenya, Wakenya na nchi yao wamejiweka mbali nayo.

Mara baada ya kauli ile, Rais Uhuru Kenyatta alituma ujumbe wake wa awali nchini Tanzania kufafanua na kujiweka kando na kauli ile ya hovyo.

Wataalamu wa masuala ya diplomasia walijua bado kitu kimoja hakijafanyika, na chenyewe ni kwa wakuu wa hizi nchi mbili kukutana na kuweka mambo sawa, jambo hilo limefanyika haraka.

Umuhimu wa kukutana

Kidiplomasia, na wakati mwingine mambo makubwa yanapotokea, haitoshi hata kidogo kukutanisha maofisa wa ngazi za juu wa Serikali peke yake kufafanua au kuzungumza, huwa inawapasa viongozi wakuu wa nchi mbili kukutana na kuzungumza, hata kama wao si chanzo cha tofauti kubwa zilizopo.

Advertisement

Uamuzi wa wakuu wa nchi kukutana una maana ya kumaliza kila chokochoko ambazo zingeliweza kupelekea utangamano wa nchi na Afrika Mashariki uyumbe na kuwa na madhara kwa pande zote mbili.

Kenya, Tanzania ‘pacha’

Ujirani mwema baina ya Kenya, Tanzania na Uganda si jambo la mchezo, si jambo la hiari, ni jambo la lazima tu. Waswahili wanasema unaweza kuchagua rafiki, huwezi kuchagua ndugu na jirani.

Miaka ile ambayo Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika, wazee wetu wanasema mahusiano ya nchi zote tatu wakati huo yalikuwa mabaya kiasi cha juu. Ilifikia wakati Watanzania wakitaka kwenda nje ya Tanzania wanaanza kuhaha kutafuta ndege za kuunganisha kutoka Dar es Salaam kwa sababu isingelikuwa rahisi kupita Nairobi, Kenya; walau siku hizi tunazo ndege zetu na viwanja vyetu vikubwa kwa hiyo hatuitegemei tena Nairobi kama sehemu muhimu ya kuunganishia ndege za kwenda nje.

Maneno ya mbunge Jaguar yangeliweza kabisa kuwa chanzo cha kuivuruga Afrika Mashariki kama wakuu wa nchi zetu wasingelianza kuchukua hatua za haraka kama walivyofanya. Kazi ambayo imebaki mikononi mwetu ni kutambua kuwa sisi ni wamoja na tusonge mbele.

Mambo ya kikoloni

Uwepo wa Kenya na Tanzania ni njama tu za wakoloni, si jambo lingine. Fitina za wakoloni wa wakati huo zilitumaliza kirahisi, bara letu likagawanywa vipandevipande na matokeo yake tukaanza kupewa majina tofauti; sisi Wakenya, wao Waganda, wale Watanzania na mengineyo.

Ukweli halisi unabakia kuwa uleule, sisi ni Waafrika tu na siyo zaidi ya hapo, hata tujidai kwa mbwembwe kubwa kiasi gani, Waafrika wetu hauondoki, upo na unatusuta asubuhi mchana na jioni.

Hata tukienda kuishi katikati ya mabara ya wenzetu na kujifunza tamaduni zao na kuzungumza lugha zao na kula kama wao na kuvaa nguo kama zao na kuchukua elimu kama yao, hayo yote hayaondoi hali halisi kuwa sisi ni Waafrika tu na hakuna kitakachobadilisha hali hiyo.

Utangamano huu wa Afrika Mashariki unapaswa kwenda mbele sana, kwanza kwa sisi sote kuendelea kujenga uwezo wa ndani wa kiuchumi na kimifumo ili siku moja mifumo yetu yote ifanane, elimu, lugha, uendeshaji wa serikali na nyanja zingine zote.

Tukikamilisha yote hayo hatupaswi kurudi nyuma, lazima siku moja tuwe na shirikisho la Afrika Mashariki lenye nguvu na uwezo mkubwa wa kidola, tunaweza kuanza polepole, lakini inatupasa kwanza tujenge uwezo wa kila nchi na huenda jambo hili linahitaji karne kadhaa mbele yetu

Afrika ya Nyerere, Nkrumah

Tunahitajiana kuliko tunavyodhani, ndiyo maana waasisi wa bara letu kina Mwalimu Nyerere na Nkrumah na wengine, waliamini kuwa siku moja Afrika inapaswa kuwa nchi moja.

Mwanamuziki Bob Marley alishajihisha mawazo hayo kwa kutengeneza nyimbo mbalimbali kuonyesha maono hayo ya mbali na mbele.

Wazee wanasema Nyerere na Nkrumah walitofautiana kwenye namna ya kuifikia Afrika Mashariki; Mwalimu akitaka mchakato huo uende polepole na kwa uhakika huku Nkrumah akitaka ufanyike mara moja.

Mawazo ya Nyerere tunapaswa kuyatumia hata kwenye utangamano wa Afrika Mashariki, tunapaswa kuweka mipango ya muda mrefu na ya uhakika, lakini tunapaswa kuachana na chokochoko za aina yoyote ile. Uamuzi wa Rais Kenyatta na Rais Magufuli kukutana na kuzungumza unatupatia picha kuwa Waafrika wanapaswa kulinda bara lao wao wenyewe.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala mbalimbali Simu; +255787536759 (Whatsup, na meseji)/ Barua Pepe; [email protected])

Advertisement