Uongozi wa Mbowe miaka 15 akipoteza viongozi Chadema

Unaweza kusema Freeman Mbowe amebaki peke yake. Hii ni kutokana na viongozi wote wa juu wa Chadema alikuwa nao katika uongozi aliposhika uenyekiti wa chama hicho mwaka 2004, kutokuwapo tena kwenye chama hicho kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuhamia CCM.

Hiyo inaelezwa kuwa ni moja ya sababu za wanachama kuendelea kumuhitaji Mbowe kukiongoza chama hicho kwa miaka mingine mitano kwa sababu amekuwa na msimamo thabiti wakati wote wa miaka 15 ya uongozi wake.

Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba Mbowe alichaguliwa kuwa mwenyekiti mwaka 2004 akichukua nafasi ya Bob Makani wakati makamu mwenyekiti akiwa ni Dk Amani Kabourou na Katibu Mkuu akiwa ni Dk Willibrod Slaa.

Makamu mwenyekiti wake kwa upande wa Zanzibar wakati huo alikuwa Mzee Said Mzee ambaye baadaye nafasi yake ilichukuliwa na Said Issa Mohamed ambaye yupo hadi sasa.

Naibu Katibu Mkuu – Bara alikuwa ni Shaibu Akwilombe wakati Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar akiwa ni Hamad Mussa Yussuf ambaye sasa yuko ACT-Wazalendo.

Mwaka 2006, Dk Kabourou alitangaza kukihama chama chake na kujiunga na CCM ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kushindwa ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.

Nafasi ya Dk Kabourou ilichukuliwa na Chacha Wangwe ambaye wakati huo alikuwa pia ni mbunge wa Tarime.

Mwaka huohuo, Akwilombe naye alitangaza kujiunga na CCM na nafasi yake kama Naibu Katibu Mkuu – Bara kuchukuliwa na Zitto Kabwe ambaye naye wakati huo alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Mwaka 2008, Wangwe alifariki dunia kwa ajali ya gari na nafasi yake kujazwa na Said Arfi ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Mpanda Mjini.

Uchaguzi ulifanyika tena mwaka 2009 na 2014, Mbowe akachaguliwa kuwa mwenyekiti huku safu yake ya uongozi ikibaki ile ile; Makamu Mwenyekiti akiwa ni Said Arfi, Katibu Mkuu, Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu – Bara – Zitto.

Hata hivyo, Julai 2015 Arfi alitangaza kujiuzulu wadhifa huo akipinga kitendo cha kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo.

Nafasi ya Arfi ilichukuliwa na Profesa Abdallah Safari ambaye katika uchaguzi wa sasa hatagombea tena wadhifa huo.

Baadaye Arfi alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM wakati Zitto naye akivuliwa uanachama na kwenda kuanzisha chama chake cha ACT -Wazalendo ambacho anakiongoza mpaka sasa. Nafasi ya Zitto ilichukuliwa na John Mnyika ambaye yupo hadi sasa.

Mwaka huo huo, Dk Slaa naye alijivua uanachama wa Chadema wakati chama hicho kikiwa kwenye mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Miaka miwili baadaye, Dk Slaa aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Hamad Yusuf Mussa aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar aliondolewa kwenye uchaguzi wa mwaka 2014 na nafasi yake ilichukuliwa na Salumu Mwalimu aliyepo hadi sasa.

Licha ya viongozi walioanza na Mbowe kuachana na chama hicho, yeye ameendelea kuwa mwenyekiti wa chama na hata sasa chama hicho kikiwa kwenye uchaguzi wa ndani, bado wanachama wanamhitaji na tayari wamemchukulia fomu ili agombee nafasi hiyo. Hoja hiyo pia inabebwa na wabaya washindani wake na wale wa chama kuwa amekaa muda mrefu na anapaswa kuondoka.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema moja ya sababu za wanachama kuvutiwa na uongozi wa Mbowe ni msimamo wake thabiti usioyumbishwa.

Anasema sababu nyingine ni mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 15 ya uongozi wake ambayo yamekuwa ni kielelezo cha uongozi bora uliokijenga chama hicho na kuwa chama kikuu cha upinzani.

“Wamepita viongozi mbalimbali kwenye chama chetu lakini hatunao tena, lakini wanachama bado wanamuhitaji Mbowe, kitu kikubwa wanachohitaji ni msimamo wake thabiti na uongozi makini wa kukijenga chama,” alisema Mrema.

Katibu Mkuu wa chama cha CCK, Renatus Muabhi anasema Chadema inamuhitaji Mbowe sasa kuliko wakati wowote kwa sababu ndiye mtu anayeweza kuhimili figisu, hila na changamoto zote ambazo chama hicho kinapitia katika awamu h.

Alisema haoni mtu mwingine ndani ya chama hicho ambaye anaweza kuwa mbadala wa Mbowe kwa sababu akiwekwa mtu legelege chama hicho kitakufa kwa sababu si wote ni wavumilivu na mahiri kama Mbowe.

“Mbowe anahitajika Chadema sasa kuliko wakati wowote. Kwa hiyo, haijalishi ameongoza miaka mingapi, suala ni amefanya nini kama kiongozi. Katika kipindi hiki watu wananunuliwa, chama kinahitaji mtu ‘active’ ambaye atakabiliana na changamoto hizo,” anasema.

Anasema Chadema inahitaji kiongozi ambaye akitoa kauli inaonekana kweli imetoka kwa kiongozi na siyo kiongozi ambaye hana ushawishi.

Muabhi anaamini Mbowe ni mtu makini mwenye uwezo, ndiyo maana wanachama wa Chadema bado wanamuhitaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema vyama vya upinzani hapa nchini havijawa imara kubadilishana uongozi kwa sababu vinajengwa katika misingi ya kiitikadi.

Kwa sababu hiyo, alisema Mbowe anastahili kuendelea kuongoza Chadema hasa wakati huu ambao kuna siasa za rushwa na fedha kutumika kununua viongozi. Alisema demokrasia ni mchakato ambao unakwenda na wakati wake.

“Sisi tunachokiangalia ni usalama wa chama uko sawasawa? Haijalishi ameongoza kwa miaka mingapi, tunaangalia mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa, huwezi kuondoka na kukiacha chama kwa kiongozi ambaye hana ideology (itikadi) ya chama,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema Mbowe amejipambanua kama kiongozi ambaye harubuniwi, kwa sababu hiyo anakiweka chama katika hali ya usalama.

“Hebu fikiria inatokea mwenyekiti wa chama kama Chadema anatangaza kujivua uanachama na kuhamia CCM kama walivyofanya wengine, hicho chama si ndiyo kinakufa hivyo? Nadhani wana hoja ya kumhitaji Mbowe,” alisema mwanazuoni huyo.