MAKALA YA MALOTO: Utu wa Mdude una thamani kuliko maslahi ya kisiasa

Wednesday May 15 2019

 

By Luqman Maloto

Mungu amefanikisha Mdude Nyagali amepatikana siku ya nne baada ya kutoweka. Alikutwa ametelekezwa akiwa na hali mbaya.

Hata hivyo, imekuwa heri ameonekana. Kada wa Chadema, Ben Saanane, ana miaka miwili na miezi sita hajapatikana. Mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, ana mwaka mmoja na miezi sita hajaonekana. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye ana mwaka mmoja na miezi kumi hajulikani alipo.

Waswahili tuna msemo wetu “heri nusu shari kuliko shari kamili”. Mdude kupatikana na hiyo ni nusu shari maana ameumizwa. Wengine hawajarejea, hilo ni shari kamili.

Jinsi Mdude alivyotekwa hadi kupatikana, inakumbusha kisa cha Roma Mkatoliki na wenzake watatu miaka miwili iliyopita na sakata la Mohammed Dewji ‘MO’, takriban miezi sita iliyopita.

Mdude alitekwa ofisini kwake Vwawa, Songwe na watu wenye bunduki waliotumia magari mawili, Nissan Patrol na Toyota Land Cruiser yasiyo na namba za usajili.

Roma na wenzake, walivamiwa na watu wenye bunduki na pingu katika studio ya kurekodi muziki ya Tongwe Records, Masaki, Dar es Salaam, wakatupwa ufukweni eneo la Ununio baada ya siku ya tatu.

Katika matukio hayo, inaonekana watekaji hawawezekani maana hawajakamatwa na wanaendelea kufanya wanavyotaka.

Kama nchi, matukio ya utekaji yanapaswa kumtikisa kila mwananchi. Maana yanagusa utu, usawa na uhuru. Nchi huru, watu wanapotekwa na kupelekwa kusikojulikana ni uhaini. Ni kuifanya nchi ionekane si huru wala salama.

Hata hivyo, kumekuwa na kauli za kushangaza mitandaoni za kuyahusisha na siasa. Kuna ambao walidiriki kushangilia Mdude kutekwa, kwamba amekuwa na tabia za kutukana viongozi. Je, anayetukana viongozi anatakiwa kutekwa au kupelekwa mahakamani?

Ukitazama watu waliozungumza hivyo kuhusu Mdude, mwelekeo wao ni vyama vya siasa. Wametofautiana kiitikadi. Wanaona itikadi zao zinapita utu na uhuru wa mahasimu wao. Hawaumizwi na shambulio la utu.

Watanzania wasivifanye vyama vyao kuwa sawa na dini. Vyama ni majukwaa tu ya kusaka uongozi. Ni dhambi kubwa kufurahia Watanzania wenzako kutekwa au kuteswa kisa mmetofautiana kiitikadi.

Tutumie hekima ya King

Gwiji wa siasa za Canada na waziri mkuu kwa vipindi vingi zaidi nusu ya kwanza ya Karne ya 20, William King, alipata kuandika kanuni kuhusu wanasiasa na vyama vyao, aliandika “chama changu cha siasa si dini yangu na hakipaswi kuwa dini yako pia.”

Pia, aliweka mwongozo wenye sehemu tatu kwa wanasiasa kuhusu vyama vyao. Mosi; “Chama changu cha siasa si mwokozi wangu.” Hapa anataka wanasiasa wasivichukulie vyama vyao sawa na Wakristo wanavyomchukulia Yesu au Masiha.

Pili; “Chama changu cha siasa hakinipendi”. Hili ni darasa kuwa hakuna chama cha siasa chenye kumpenda mtu. Vyama huhitaji watu ili vijijenge kuwa vikubwa lakini pale inapobidi kinaweza kumjeruhi yeyote kwa ajili ya kutimiza malengo yake.

Tatu; “Chama changu hakina uzima wa milele”. Hakuna chama ambacho kinatoa uhakika wa uzima wa milele kwa mwanachama wake. Hivyo, kila mtu kwenye chama ni wa kupita tu, leo upo kesho haupo.

Mwongozo huo wa King ukibebwa na kila mwanasiasa kama kanuni, utaokoa kundi kubwa la watu ambao huwa waaminifu kwa vyama na kujenga chuki kwa mahasimu wao kana kwamba uhai wao unafungamana na uanachama wao.

Kila mwanachama, hasa kijana, hupaswa kufahamu kuwa kadi ya uanachama haitoi oksijeni, hivyo wanapoielekea siasa lolote linaweza kutokea kwenye vyama vyao, ama kutimuliwa au kuvihama.

Katika vyama inaweza pia kutokea kukimbiwa na watu ambao inaaminika ndiyo uhai wa chama au kuwa na viongozi ambao hukubaliani nao mitazamo, kiasi cha kujikuta unakuwa huna furaha.

Advertisement