Vibwagizo vinavyombeba Mwanri kwenye utendaji

“Sukuma ndani, kitanda kwa kitanda, mguu kwa mguu, injinia soma hiyooo, anayebisha anyooshe mkono, jifanye unajikuna, fyekelea mbali na tatizo ni berti.”

Si kauli ngeni masikioni mwa Watanzania hasa kwa wale watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini.

Kauli hizo ni zile zilizowahi kutolewa na zinazoendelea kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri ambaye kila anaposimama anakuja na misemo yake ya kusisitizia uamuzi ama maagizo anayoyatoa kwa watendaji anaowaongoza.

Misemo hiyo ambayo imepata wasomaji na wasikilizaji wengi mitandaoni kwa muda mrefu sasa, amekuwa akiitoa katika maeneo tofauti mkoani Tabora wakati wa ukaguzi wa miradi, ufunguzi wa mikutano na uzinduzi wa miradi.

Mwananchi lilipomuuliza ni wapi alikotoa staili hiyo ya utendaji, Mwanri aliyewahi pia kuwa mbunge wa Siha mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya CCM, anasema, “hii ni staili yangu ya kufikisha ujumbe kwa ninawakusudia na ninalenga kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani kwangu.”

Mwanri aliteuliwa na Rais John Magufuli Machi 13, mwaka 2016 kuwa Mkuu wa Tabora, hali inayomfanya kuingia kwenye orodha ya wakuu wa mikoa waliodumu kwa muda mrefu kwenye mkoa mmoja katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Hata hivyo, ingawa mkoa huo una historia ya kipekee kama ya kuwa na shule aliyosoma Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyeyere, lakini unatajwa kuwa maendeleo yake bado yako nyuma licha ya kupitiwa na reli ya Uhuru.

Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa iliyo na barabara za lami zinazounganisha wilaya na mikoa mingine.

Akizungumzia shughuli za maendeleo za mkoa wake, Mwanri anasema kwa sasa mkoa huo ambao una utajiri wa maziwa na asali lakini bado watu walikuwa wanakataa kufanya kazi huko, sasa wanaukimbilia.

“Ndugu yangu, hayo mambo yalikuwa ya zamani, lakini hivi sasa mtu asikudanganye, watu wanakimbilia kuja tena siyo mkoani tu hata huko wilayani mambo yamepambana moto,” anasema Mwanry ambaye ni kada wa CCM. Kiongozi huyo ambaye ni miongoni mwa wakuu wa mikoa 13 walioteuliwa, anasema bado anaugulia deni la kuona mkoa wake unakuwa kilele katika nyanja zote.

Ujenzi wa Viwanda

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo kuhusu ujenzi wa viwanda, Mwanri anasema kwake mambo ni moto na hakuna kilichokwama.

Anasema wilaya zote za mkoa wake zimejaza viwanda, uchumi umekua, ajira zimeongezeka na maisha ya watu wake yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Anasema maoni ya Rais Magufuli ya Serikali ya viwanda kwake hakuna shaka, yametimia kwasababu wamelitekeleza agizo hilo la kuwa na viwanda kwa zaidi ya asilimia 100.

“Hivi viwanda vinavyotajwa katika uzalishaji mali, mbona kwangu wilaya zote zimekamilisha. Tuko juu ya kiwango sisi. Hapa ukienda Igunga viwanda kibao, Ukienda Nzega, Uyui, Urambo na maeneo mengine mambo yetu sisi ni bambam,” anasema Mwanri.

Anatoa mfano katika wilaya za Nzega na Igunga kuwa ina viwanda vyenye uwezo wa kuajiri watu watano hadi 12 kuwa ni 113.

Anasema kati ya viwanda hivyo, 75 vinamilikiwa na watu binafsi huku 38 vikimilikiwa na vyama vya ushirika na taasisi nyingine.

Kuhusu kiwanda cha Kuchambua Pamba cha Manonga, Mwanri anasema miongoni mwa mambo yanayomfurahisha zaidi ni kufufuliwa kwa kiwanda cha Manonga ambacho kilikuwa kimekufa kwa zaidi ya miaka 20.

Anasema kiwanda hicho kwa sehemu kubwa kinachangia uchumi wa wilaya ya Igunga na kimeajiri watu 320 tangu kifufuliwe.

Akizungumzia mifugo, Mwanry anasema Tabora una idadi ya watu ambayo ni sawa na ile ya mifugo inayofikia milioni 2.

Anasema nguvu kazi hiyo inayoendana na idadi ya mifugo ni chachu ya kuwafikisha panapotakiwa.

Anasema mifugo hiyo imemsukuma kuhamasisha wawekezaji ambao kwa sasa wameanza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama Wilayani Nzega.

Anasema kiwanda hicho kinachotarajiwa kujengwa kwa haraka kwa kasi aliyoiita ya 4G, lengo likiwa ni kuongeza ajira na kupunguza safari za kupeleka ng’ombe Jijini Dar esa Salaam.

Anasema baada ya ujenzi wa kiwanda hicho, watapeleka nyama iliyochakatwa kwenye kiwandani hapo. Katibu huyo wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, anasema kwa wingi huo wa mifugo wameamua kuutumia kama fursa badala ya kuona kuwa ni changamoto ya uharibifu wa mazingira na anawahamasisha watu wale nyama zaidi na kunywa maziwa kwa wingi.

Uzalishaji asali

Mwanri anasema kwa sasa hatua waliyofikia si ya kuuza asali kwenye chupa, badala yake Serikali ya Mkoa na Wilaya wameshirikiana kutoa mafunzo kwa wajasiriamali yatakayowawezesha kuanzisha viwanda vya kuchakata asali.

Anasema mafunzo hayo pia yanalenga utunzaji wa mizinga ya kisasa, ndio maana imechochea kuwapo kwa ongezeko kubwa la mavuno ya asali kutoka kwa wakulima.

Hata hivyo, anasema bei inayotolewa na wanunuzi haivutii kwa ajili ya kuwapatia kipato wakulima wake.

Hata hivyo, anasema jukumu kubwa liko mikononi mwa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo Nchini (Sido) na kwamba, ameshatoa maelekezo kwa wilaya na mkoa wawapatie watu elimu ya kutengeneza mizinga yenye gharama nafuu kusudi waongeze kipato.

Akizungumzia suala la mikopo, kiongozi huyo mkuu wa mkoa anasema suala hilo lilikuwa na changamoto hasa kwa vijana, wanawake na walemavu kwa sasa limewekewa udhibiti na usimamizi mkali hivyo linakwenda vizuri.

Anasema hakuna mkaidi kwa sasa kwa sababu kila kitu kinawekwa wazi, hivyo vijana na wanawake wanajua kuwa asilimia 10 ya mapato ya wilaya ni yao.

Anasema jambo hilo liko wazi na fedha hizo ndizo zinazochagiza ukuaji wa miradi mingi ndani ya mkoa.

Miradi ya kimkakati na miundombinu

Mwanri anasema Sh 602 bilioni zimepelekwa na Serikali hivi karibuni kwa ajili ya kujenga miradi mikubwa ya kimkakati na kukamilika kwake kutaendelea kuipaisha Tabora na kuifanya ionekana kuwa ya thamani zaidi.

Kuhusu ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege mkoani humo, Mwanri anasema ni heshima kubwa kwa watu wa mkoa huo.

Hata hivyo, anasema safari za ndege (bombadia) zinazoruka na kutua zimeuchangamsha mji kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wa upelekaji wa maji kwenye Ziwa Victoria, anasema mipango inakwenda vizuri kufikisha maji katika maeneo yote ambayo yanatakiwa kupatiwa maji na maandalizi ya mipango hiyo yanamtia moyo kuwa ipo siku tatizo la maji mkoani humo litaisha.

Maisha yake kisiasa

Anapoulizwa kuhusu hatma yake katika mwaka huu wa uchaguzi, Mkuu huyo wa mkoa anasema ni mapema kuelezea nini kitatokea kwa sababu amepewa jukumu kubwa la kuwaongoza watu maskini.

“Mungu hajasema nami kuhusu jambo hilo, naamini yapo makusudi yake. Lakini akisema nami hakuna kitakachofichika. Mbona tutasemezana na kuambiana ukweli. Lakini kwa sasa bado nahangaika na hawa maskini wenzangu,” anasema huku akicheka.

Kuhusu mbinu gani anazozitumia kufanikisha mambo hayo, anasema mkoa wa Tabora ameugawa kwa kila wilaya katika mahitaji yanayotakiwa ambayo anaamini kwa ushauri wa wataalamu wake yanapatikana.

Anatoa mfano wa Wilaya kama ya Nzega ambayo imekabidhiwa kushughulikia kilimo hasa pamba na viwanda kama ilivyo kwa Igunga, lakini wilaya ya Kaliua wanashughulika na kilimo cha alizeti, huku wilaya za Urambo na Sikonge wakishughulikia tumbaku.