Vita dhidi ya maadui watatu wa nchi, tunakwama wapi kuishinda?

Wednesday October 23 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi

Ni maadui watatu waliotajwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tangu tunapata uhuru – ujinga, umaskini na maradhi. Hadi anazikwa kijijini kwake Butiama Oktoba, 1999, maadui wa Taifa walibaki ni walewale watatu.

Pamoja na juhudi kubwa alizofanya Mwalimu na hatua kubwa aliyofikia maadui hawa aliwaacha duniani japo kwa viwango tofauti na hata sasa bado wangalipo.

Ndiyo maana wakati wa mijadala mbalimbali ya kukumbuka maisha yake yaliyokoma Oktoba 14, 1999, maadui hao wamekuwa katika vinywa vya watu wengi.

Katika kongamano la miaka 20 ya Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanazuoni, wataalamu mbalimbali walipata fursa ya kujadili ni kwa kiwango gani jitihada za kutekeleza malengo aliyosimamia Mwalimu yanaendelezwa.

Moja ya malengo hayo ni vita vya kutokomeza maadui hao watatu, kama anavyoeleza Profesa Lawrence Mseru, mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kongamano hilo.

Profesa Mseru anasema maradhi bado ni adui mkubwa wa maendeleo ya taifa.

Advertisement

Profesa Mseru anasema ndoto ya Nyerere ilikuwa ni kuona wananchi wanakuwa na afya njema kwa kupata kinga na tiba ya magonjwa mbalimbali.

Kwanini aliamua kuwekeza katika afya? Swali hilo linajibiwa na Dk Shindo Kilawa, daktari katika Hospitali ya Mloganzila, “maradhi yanamdhoofisha mtu, anakosa nguvu ya kufanya kazi na wakati mwingine huja kwa sababu ya ujinga.

“Mfano tu, mtu hawezi kutunza usafi wa mazingira yake mwenyewe. Vita hii bado inahitaji kupiganwa na ndiyo baba wa taifa alipambana nayo” anasema Dk Kilawa.

Profesa Mseru anasema maelekezo ya mkutano mkuu wa chama cha Tanu mwaka 1972 juu ya kupeleka huduma za afya kwa wananchi hayakuwa ya kinadharia bali ya vitendo ili kupambana na maradhi.

Wakati huo, anasema bajeti ya Wizara ya Afya iliyokuwa asilimia sita iliongezwa hadi asilimia 7.5 mwaka 1977/78.

“Huduma za afya zilipewa kipaumbele kwa msisitizo wa Azimio la Arusha kupitia mipango yote ya maendeleo. Mwalimu kwenye hotuba zake alisisitiza watu wapate chakula bora na cha kutosha ili wawe na afya nzuri,” anasema.

Zaidi ya hayo, anasema Mwalimu alisimamia ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa wananchi wake huku akitilia msisitizo kwenye kinga.

Mwasisi wa bima ya afya

Katika mada yake, Profesa Mseru anasema Mwalimu Nyerere pia ndiye aliyeasisi Bima ya Afya ya Jamii mwaka 1962.

Anasema Mwalimu aliona umuhimu wa watu kushiriki na kugharamia kwa pamoja katika kuendesha huduma za afya wakati Serikali yake ilipokuwa na miezi saba tu madarakani.

“Alijua mahitaji ya wananchi wakati huo na changamoto ambazo wangepata kwa kukosa mfumo huo. Kwa wakati ule mwalimu alimtafuta mtaalamu baada ya kuwasiliana na Serikali ya Israel ili atafiti namna gani bima ya afya kwa wananchi wake itawezekana,” amesema Mseru.

Anamtaja Dk Channan Lachman, mkurugenzi wa Bima ya Afya wa Israel wakati huo kuwa ndiye aliyewasili nchini kufanya utafiti huo.

“Serikali ya mwalimu ilimuhitaji mtaalamu huyu kujua jinsi makundi ya jamii kama waajiri, waajiriwa, familia zao na wananchi waliojiajiri mijini na vijijini wanaweza kunufaika na bima hiyo,” alibainisha.

Kitendo cha Mwalimu kuanza mapema kuhamasisha bima ya afya, alihitaji Watanzania wamwelewe.

Hata hivyo, anasema sasa mwitikio wa Watanzania kujiunga na bima za afya za NHIF na CHF ni asilimia 33 tu.

Ukiacha suala la kupambana na maradhi, Chrispin Nziku kutoka Shirika la Pamoja Foundation anasema vita ya ya jumla dhidi ya maadui wa Taifa bado ni mbichi kwa sababu wapo wanaoshindwa kupata matibabu stahiki kwa kukosa fedha kutokana na adui mwingine – umaskini.

“Mtu hana bima ya afya na hana fedha unadhani atapewa huduma za afya stahiki na ya haraka? Kuna tabaka kati ya wenye uwezo na maskini, hivyo licha ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, tutaendelea kupigana vita dhidi ya adui maradhi,” anasema.

Utafutaje maradhi na umasikini bila kufuta kwanza ujinga? Haiwezekani. Ili kuwashinda maadui hawa lazima ufanye yote kwa pamoja ndiyo utapata usitawi wa wananchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi anasema Mwalimu aliamua kupambana na maadui wote watatu kwa sababu alijali ustawi wa wananchi.

Msisitizo kuhusu elimu unawekwa na Profesa Rwekaza Mukandara, mwenyekiti wa sasa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, kuwa ili kufuta ujinga ambao ni chanzo cha umasiki na maradhi, katika miaka ya 1960 hadi 1970, Mwalimu Nyerere aliamua kupanua elimu ya msingi kwa kasi kubwa.

“Na Serikali iliendesha elimu endelevu ya watu wazima na watu walisoma,” anasema.

Na elimu ya wakati huo, ilijengwa katika falsafa ambayo hata leo bado inafaa, anasisitiza Profesa William Anangisye, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Falsafa nzuri ya elimu ni ile inayojikita kutatua changamoto zinazomzunguka mtu. Kama elimu haimfanyi mtu atengeneze ajira katika mazingira yake haifai,” anasema.

Anasema elimu inayotolewa inapaswa kumpatia mtu uwezo wa kutatua changamoto zake, hivyo elimu ya kujitegemea bado ina thamani.

Hata hivyo, mambo si yaleyale, yamekuwa yakibadilika na kuleta athari hasi, kama anavyoeleza Nziku kuwa mabadiliko ya sera mara kwa mara yamekuwa yakiyumbisha elimu hasa pale kila waziri anapoingia kuanzisha jambo lake kwa kufuta yaliyofanywa na waliomtangulia.

“Mfano anakuja waziri anafuta elimu ya kilimo na ufundi, mwingine akija analeta elimu hiyo. Ufundi unaonekana kama elimu ya waliofeli wakati ndio unayotengeneza ajira!”

Lakini, hata elimu inayojadiliwa aliyoianzisha Mwalimu haikuishia tu kwenye ngumbaru, ilisisitiza pia teknolojia na uvumbuzi, kama anavyoeleza Profesa Cathbert Kimambo kutoka UDSM ambayo itakiwa kuzingatiwa ili kuishi ndoto za Mwalimu.

“Hii itasaidia kuwa na elimu ya ujasiriamali yenye ufanisi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mtu mmoja na nchi kwa ujumla,” anasisitiza.

Unawezaje kumjadili Nyerere kwa usahihi bila kuzungumzia kilimo? Si kazi rahisi na Profesa Raphael Chibuda, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine anasema ukifuata mawazo ya Nyerere katika kuendeleza kilimo, kipato cha wananchi wa vijijini kitaongezeka.

Kupitia vita dhidi ya umaskini, michango ya wachangiaji mbalimbali ilionyesha kuwa Mwalimu aliwaongoza Watanzania kuanzisha ujenzi wa uchumi wa kijamaa wa kidemokrasia na katika kipindi hicho mafanikio makubwa ya viwanda yalipatikana.

Mfano, walisema kuwa vifaa vya ujenzi, radio, umeme, nguo, vyakula, vinywaji, dawa na pembejeo vilipatikana ndani na mchango wa sekta ya viwanda kwenye ajira uliongezeka kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na yote, iliwekwa bayana kwamna Mwalimu Nyerere alikataa masharti yote ya Shirika la Fedha Duniani na kuwafukuza wataalamu hao.

“Aliwashangaa na kutokubaliana na sababu walizotoa za kuyumba kwa uchumi na kuwa mfumo wa uliberali ulikuwa ndio mwarobaini wa matatizo yote hayo,” anasema Profesa Godius Kahyarara.

Hata hivyo, baada ya Tanzania kukubali kutekeleza mageuzi ya uchumi, matokeo yake ilikuwa ni kuongezeka kwa umaskini, baadhi ya watu walishindwa kupeleka watoto shuleni, madeni yaliongezeka na sekta kadhaa, hasa kilimo, zilikumbana na changamoto za kukosa ugani.

“Bei ya pembejeo ilipanda, thamani ya shilingi iliporomoka, riba zikaongezeka na kukawa na ukosefu wa ajira kwa kuwa viwanda vingi vilifungwa,” anasema Profesa huyo.

Anasema ubinafsishaji ulisababisha kuuzwa kwa viwanda ambavyo mpaka leo vingine havijaweza kufanya kazi huku sehemu nyingine mashine zikiondolewa.

Hayo yote yanajadiliwa mwaka hata mwaka, lakini yanatusaidiaje? Zakia Meghji, waziri wa zamani wa fedha ndiye anakuja na suluhisho alisema “kila mmoja anapaswa kutafakari misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere na kuangalia namna gani itaendelezwa.”

Advertisement