Vuta nikuvute ya Rais Uhuru Kenyatta, Ruto yafikia pabaya

Saturday January 18 2020

 

By Reginald Miruko, Mwananchi

Kwa vipindi viwili Uhuru Kenyatta na William Ruto wamekuwa marafiki wa karibu na wamegombea pamoja na kushinda uongozi wa juu wa Kenya.

Wakati Kenyatta amekuwa Rais, mwenzake amekuwa naibu Rais. Lakini urafiki wao unakwenda mrama. Na ndoa yao ya kisiasa inaelezwa kusambaratika.

Wawili hao waliunganisha nguvu na kugombea pamoja kupitia Jubilee katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2013. Kabla ya hapo Ruto alikuwa anamuunga mkono Raila Odinga hadi uchaguzi uliosababisha vurugu wa mwaka 2007.

Ingawa kila mmoja anaendelea na majukumu yake ya uongozi kwa mujibu wa katiba, wafuatiliaji wa siasa za Kenya wanasema kuna ufa mkubwa baina yao.

Vyombo vya habari navyo vinaeleza kuwa maneno ya Kenyatta na Ruto hayalingani na vitendo vyao ambavyo vinaonyesha uhusiano mbaya, kila mmoja akihujumu mwenzake.

Ingawa wawili hao hawashambuliani moja kwa moja, washirika wao ndio wamekuwa wakitangaza hisia na misimamo yao kwa umma.

Advertisement

Rais Kenyatta amekuwa akitoa matamshi kwa mafumbo, yanayoaminika kuwa anamshambulia Ruto kuhusu masuala tofauti; huku mwenzake akishikilia kuwa uhusiano wao uko imara na wanafanya kazi pamoja.

Wanasiasa walio upande wa rais wakiongozwa na David Murathe na kundi la ‘Kieleweke’ wamekuwa ndio mijeledi ya kumgonga Naibu Rais; huku yeye akitumia kundi la ‘Tangatanga’ kumshambulia Rais Kenyatta.

Makundi hayo yanawashirikisha baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitoa maneno makali yanayoashirika malumbano kati ya Rais Kenyatta na Ruto.

Kulingana na vyombo vya habari, hata baadhi ya vitendo vya Rais Kenyatta vinaonyesha hamwamini tena mshirika wake katika uwakilishi wake kwenye hafla.

Kulingana na utaratibu, naibu rais ndiye anayefaa kumwakilisha rais kwenye hafla, lakini katika siku za karibuni amekuwa akiwatuma maofisa wa serikali ama wabunge kumwakilisha licha ya Ruto kuwepo kwenye hafla hizo, linasema gazeti la Taifa Leo la Kenya

Kwa mujibu wa gazeti hilo, hivi karibuni kulitokea mtafaruku katika mazishi ya mamake Rigathi Gachagua, mbunge wa Mathira, wakati Mbunge wa Kieni, Kanini Kega aliposema ametumwa na rais kuipatia

familia hiyo Sh500,000 za kuifariji licha ya kuwa Ruto alikuwapo.

Mwaka jana Waziri wa Utumishi wa Umma, Margaret Kobia alimwakilisha Rais kwenye hafla ambapo ilihudhuriwa na naibu rais katika Kaunti ya Nyeri.

Vitendo vya maofisa wakuu serikalini wakiongozwa na Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na katibu wake Karanja Kibicho pia vinaonyesha mfarakano unaokumba ndoa ya wawili hao iliyobatishwa kama “UhuRuto”.

Rais ampunguzia madaraka

Mwa mtazamo wa baadhi ya watu Kenyatta alimdhalilisha Ruto mwaka jana alipomwondoa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri kuhusu Maendeleo na kukabidhi wadhifa huo kwa waziri Matiang’i.

Katika tukio jingine, wiki iliyopita Ruto alikatazwa kulala katika makao rasmi ya Naibu Rais mjini Mombasa kwa agizo la ofisa wa ngazi ya juu serikalini.

Maofisa wa usalama, utawala wa mikoa na mashirika ya serikali pia wamekuwa wakikwepa hafla za naibu rais kwa kuogopa kuadhibiwa kwa kujihusisha naye.

Vita ya kisiasa kati wawili hao vimekuwa vikipamba moto tangu Rais Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga washikane mkono mwaka 2018.

Mgawanyiko Jubilee

Vita vya wawili hao pia vimekigawa chama cha Jubilee katika makundi mawili, huku Rais akionekana kutojali hali hiyo.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) Novemba mwaka jana, Mbunge wa Suna Mashariki (ODM), Junet Mohamed alieleza waziwazi kuwapo migawanyiko ndani ya Jubilee, huku Rais Kenyatta akionekana akiangua kicheko.

Pia wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra, mwezi huohuo wa Novemba Rais hakushiriki kwenye kampeni za Jubilee na chama hicho kikashindwa.

Tangatanga walaani

Kufuatia tukio la Ruto kuzuiwa kutumia makazi ya naibu Rais Mombasa iliyoripotiwa na Gazeti la Sunday Nation, timu yake maarufu kama Tangatanga imedai kuna maafisa fulani katika ofisi ya Rais ambao wanaendeleza kampeni za kumhujumu kiongozi huo.

Seneta wa Kericho, Aaron Cheruiyot na Moses Kuria, mbunge wa Gatundu Kusini walidai maafisa hao ambao hawakuwataja ndio pia wamekuwa wakiwahangaisha viongozi wanaounga mkono azma ya Ruto kuingia Ikulu mwaka 2022.

“Kuna watu fulani serikalini wanajidanganya kwa kumkosea heshima Naibu Rais William Ruto na sisi kama wafuasi wake. Lakini nataka kuwaambia kwamba hawatafaulu,” amesema Kuria.

Huku akilaani kitendo hicho, Seneta Cheruiyot alilinganisha yaliyompata Ruto na Wakenya wa kawaida ambao nyakati zingine hujikuta wamefungiwa milango ya nyumba zao kwa kutolipa kodi.

“Kama mtu wa kawaida, Naibu Rais alirejea kutoka Krismasi na kukuta kufuli langoni... Tunawajua waliotekeleza kitendo hicho lakini najua watafeli,” Cheruiyot akasema katika akaunti yake ya Twitter.

Makazi rasmi ya Naibu Rais yalifanyiwa ukarabati kwa gharama ya Sh152.4 milioni mwaka 2018 kwa kuwa zamani yalikuwa makazi ya mkuu wa Mkoa wa Pwani chini ya utawala wa zamani wa mikoa.

Ilitarajiwa kuwa akizuru Pwani kwa shughuli za kikazi, Ruto angeishi hapo badala ya hotelini.

Kwa mujibu wa habari hizo, Ruto alilazimika kulala katika hoteli ya English Point Marina baada ya kufika katika makazi yake na kukuta wafanyakazi wakipakia mizigo yake kufuatia agizo “kutoka juu”.

Mbio za Ruto 2022

Hayo yote yanatokea yakifungamanishwa na juhudi za Ruto kutaka uraia mwaka 2022. Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale anasema kuna mipango ya kichinichini katika Serikali ya Jubilee kumzuia Ruto kushinda urais katika uchaguzi ujao.

Kwa mujibu wa Duale, mtindo uliotumiwa na baadhi ya washawishi serikalini kumzuia Rais Uhuu Kenyatta na Ruto kuwania urais wa 2013, ndio umeanza kutumiwa sasa katika serikali kuzima nyota ya Naibu Rais.

Katika mahojiano yake na The Sunday Nation, Duale alisema kilinge hicho kiko katika Serikali ya Jubilee na kinafanya juu chini ili Ruto asiwe Rais, nia yake ikiwa kumuunga mkono “kiongozi wa taifa atakayelinda masilahi yao binafsi.”

Ruto azuiwa kwenda Sudan

Mlolongo wa matukio kuhusu Ruto haukuishia hapo, wiki iliyopita alilazimika kuahirisha safari yake ya kwenda Sudan baada ya ndege aliyokodi kunyimwa kibali.

Ruto alikuwa amepanga safari hiyo kwenda kujionea ufugaji kuku unavyofanyika katika shamba moja jijini Khartoum, lakini alikatiza safari yake baada ya Mamlaka ya Viwaja vya Ndege (KCAA) kutokutoa kibali cha ndege hiyo kusafiri.

Tukio hili lilitokea wiki tatu baada ya Ruto kulazimika kutumia ndege ya abiria wa kawaida kwenda likizo ya Krismasi nje ya nchi, wakati ndege ya kijeshi (KDF) aliyokuwa amepangiwa kukatazwa kuondoka, yeye na familia yake wakiwa tayari wameingia ndani.

Desemba 23, 2019 majira ya saa mbili za jioni, Ruto na familia yake walikuwa katika uwanja wa ndege wa JKIA jijini Nairobi tayari kuondoka kwa ndege ya jeshi aina ya Bombadier Dash 8 kwa safari ya Botswana na Namibia kwa mapumziko ya Krismasi.

Ripoti zinasema Naibu Rais alikuwa amezungumza na Rais Kenyatta wiki moja kabla ya safari hiyo na akapata kibali cha kutumia ndege hiyo ya kijeshi.

Lakini yeye na familia yake wakiwa wamepanda ndege hiyo, walipata habari kutoka kwa marubani kuwa wamepokea maagizo kutoka kwa wakubwa wao kuwa wakatize safari.

Ilibidi washuke na mizigo yao kuondolewa ndipo wakalazimika kutumia ndege ya Kenya Airways iliyokuwa ikielekea Afrika Kusini, ambako walikaa kwa saa kadhaa jijini Johannesburg walikounganisha ndege nyingine ya kuwapeleka Namibia.

Habari zinasema alipofika Namibia na Botswana, Ruto alipokewa kwa heshima zinazomstahili. Akiwa Namibia alipewa magari ya serikali na ndege iliyompeleka Botswana.

Uhuru asema nimechoshwa

Wakati vitendo vingine baina ya wawili hao vikiwa kimyakimya, kauli ya Rais Kenyatta Desemba 5 huenda ndiyo ilitoa mwanga kuhusu mawazi yake aliposema amechoka kwa siasa za kundi la Ruto.

Akizungumza alipofungua zahanati katika eneo la Mang’u, Kaunti ya Kiambu, Rais Kenyatta alisema amechoka na siasa za kila mara za kundi la Tangatanga ambalo linaunga mkono Ruto kuwa rais 2022.

“Kabla ya ripoti ya BBI walikuwa wakipiga siasa kote. Sasa tumetoa ripoti wameanza siasa zingine. Tumefika pahali na tunasema tumechoka. Hawa ni watu ambao hawajui wanachofanya. Itakuwa hivi ama vile. Wakome kutupigia kelele kila mara,” akasema.

“Huwa wanaona nimenyamaza wanadhani mimi ni mjinga. Hakuna kitu ambacho sijui,” akaongeza.

Rais Kenyatta alihitimisha matamshi yake akisema, “Ni Mungu na wananchi wanaojua atakayeongoza.”

Advertisement