MAKALA YA MALOTO: Wakuu wa mikoa, wilaya wampunguzie Rais mzigo

Wednesday July 24 2019

 

By Luqman Maloto

Tangu namba yangu ya simu iwekwe gazetini ili kupata maoni ya wasomaji wa safu, nimepigiwa simu na watu wengi. Wapo wanaopongeza, wanaokosoa, lakini wengine hutumia kama jukwaa la kueleza kero zao.

Ukisikiliza kero za wananchi, malalamiko yao ni dhuluma na kutotendewa haki na mamlaka za nchi. Sauti za moyoni za wananchi wengi ni kukosa imani na viongozi wa ngazi za chini.

Sasa sishangai kuona Rais John Magufuli akifanya ziara mikoani na kugawa pesa kwa wananchi mbalimbali wenye kumlilia shida. Sababu ni mbili; ya kwanza ni kuwa kuna wakuu wa mikoa na wilaya hawana muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi ndani ya mamlaka zao. Wengine wanasikiliza lakini hawatatui au hawatendi haki. Matokeo yake wananchi wanakosa imani na viongozi.

Unakuta mwananchi anapiga simu kuomba msaada wa namna ya kumfikia Rais Magufuli au Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Ni kwa sababu anakuwa ameona huko ndiko anaweza kupata utatuzi wa kero yake.

Wapo wananchi huhangaika hadi kupata namba za mawaziri. Tatizo mawaziri hawapokei simu. Viongozi wanakuwa mbali sana na wananchi. Umepewa dhamana ya kuhudumia watu, lakini upo mbali nao.

Ulimwengu wa sasa wa teknolojia ya habari na mawasiliano, haumlazimishi kiongozi aishi uswahilini ndipo ajue kero za watu. Ni suala la kupokea simu tu, lakini viongozi hawazipokei. Wana wasaidizi, wamepewa rasilimali za kuhudumia watu lakini hawawafikii watu, mpaka Rais?

Advertisement

Hivi karibuni, Rais Magufuli alipokuwa Mbeya alipokea kero nyingi mpaka akaagiza viongozi kutenga siku za kusikiliza kero za wananchi.

Wakati wananchi walipambana kupata nafasi ya kumfikia Rais Magufuli na vilio juu, viongozi wa mkoa huo walipiga. Mmoja alisema vyama vifutwe ili kibakie kimoja, utadhani ikibaki hivyo ndio kero za watu zitakwisha.

Mama kama mkimbizi

Wiki hii nilipokea simu ya mwanamke (jina nalihifadhi), akiomba anitumie barua ya malalamiko aliyomwandikia Waziri mkuu, Kassim Majaliwa lakini wasaidizi wake hawamsaidii. Anasema kuna msaidizi mmoja wa waziri mkuu kila siku huomba akumbushwe upya, yaani ambacho huambiwa huwa hatilii maanani.

Kuwafikia viongozi ni kazi kubwa mno, lakini changamoto nyingine ni wasaidizi wao. Badala ya kuwa daraja la kuwaunganisha viongozi na wananchi, wanageuka ukuta. Mwishowe wananchi wanamsubiri Rais ziarani mikoani wamlilie, awape na pesa.

Sababu ya kuishi kwa kutangatanga ni mtego aliouweka wa kuwakamata majangili waliokuwa na meno ya tembo. Anasema aliweka mtego vizuri na kukamata wahusika pamoja na meno yenyewe. Anadai watuhumiwa walipokamatwa, aliitwa na ofisi ya mkuu wa wilaya.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mkuu wa wilaya alimwambia alifanya kosa kujifanya ofisa wa Tanapa, hivyo alichukuliwa na polisi kufunguliwa jalada na kutakiwa kuandika maelezo yake.

Baadaye kwa vyanzo vyake alisikia kwamba amefunguliwa kesi ya kukutwa na meno ya tembo. Alipoona anageuziwa kibao na kupewa kesi isiyo na dhamana, alikimbia makazi yake huku akitafuta mamlaka za juu zimsaidie.

Ukimsikiliza mama huyo anatia huruma, ipo SMS alinitumia anasema anatamani kujiua. Haimaanishi kila anachosema ni sawa, lakini nani asiyejua kuhusu tabia za kubambikiana kesi? Vema huyo mama angesikilizwa na kusaidiwa.

Kwa kuwa sakata zima linahusu Wizara ya Maliasili na Utalii, nilimtumia Waziri Hamis Kigwangalla barua na maelezo ya mama huyo na namba zake za simu. Kigwangalla aliniahidi kufuatilia. Kwa kuwa anamlalamikia mkuu wa wilaya, pia nilimtumia Waziri wa Tamisemi ambaye hakujibu chochote.

Ukweli kero ni nyingi. Wasaidizi wa Rais Magufuli, hasa wakuu wa mikoa na wilaya, wangesimama vizuri kutatua kero za wananchi na kutenda haki, wangeondoa kwa kiasi kikubwa vilio vya wananchi na kumpunguzia mzigo Rais.

Advertisement