Wanasheria: Jaji Mkuu anaomba mamlaka yaliyo mikononi mwake

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma hivi karibuni alipendekeza makosa yote yawe na dhamana kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano wa mahabusu kwenye magereza nchini.

Katika matamshi yake ambayo ameyatoa mara kadhaa, amekuwa anaivua lawama mahakama kuhusu ucheleweshaji wa kesi akisema upelelezi wa kesi ndio tatizo la msingi katika eneo hilo.

Lakini maoni hayo ya Jaji Mkuu Profesa Juma yamepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanasheria wakisema mahakama yenyewe inaweza kuwa suluhisho la tatizo hilo.

Alichosema Jaji Mkuu

Miongoni mwa kauli zake ni ile aliyoitoa Julai 19, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwaapisha wanasheria waliomaliza mafunzo ya sheria kwa vitendo kuwa mawakili jijini Dar es Salaam kuwa mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi mahakamani lakini kinachosababisha hali hiyo ni upelelezi kutokukamilika kwa wakati.

“Kuchelewa kumalizika kwa shauri mahakamani wa kulaumiwa ni wapelelezi na si mahakama,” alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu anasema sheria zimeegemea zaidi kwenye adhabu kubwa zenye upelelezi unaochukua muda mrefu zinaongeza msongamano, huku akitolea mfano wa mashauri ya mauaji, matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya, uhujumu uchumi na ubakaji.

Ili kutatua changamoto hiyo, Profesa Juma anapendekeza masharti ya dhamana kulegezwa na kushauri kutumia vitambulisho vya Taifa kwenye dhamana na sheria kutamka wazi muda wa kufanya upelelezi, ambao upelelezi haujakamilika basi shauri hilo linafutwa mahakamani.

Maoni ya wanasheria

Miongoni mwa wanasheria waliojadili suala hilo ni Onesmo Olengurumwa, mratibu wa Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), ambaye licha ya kumpongeza Jaji Mkuu kwa kusema hadharani changamoto hiyo, yeye hakubaliani naye.

“Tulitarajia kuona Jaji Mkuu akija moja kwa moja na mkakati mahsusi wa kimahakama kutatua changamoto hizo badala ya kulalamika, sisi tunadhani wanaopaswa kulalamika ni sisi wananchi wa kawaida,” anasema.

Olengurumwa anasema ili kutatua changamoto za mfumo wa uendeshaji wa kesi za jinai hapa nchini, ni lazima taasisi mbalimbali zihusike – Mahakama, Bunge, Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Mashirika ya haki za Binadamu, Jumuia za wanasheria na wananchi.

“Historia ya dunia inaonyesha katika ujengaji wa mifumo ya haki, mahakama zimekuwa mstari wa mbele kwa asilimia kubwa, bila kusubiri Bunge litunge sheria wala Serikali iweke au itengeneze taratibu za kiutawala za kutatua changamoto za utoaji haki.

“Marekani, Uingereza, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Ghana na India ni baadhi ya nchi zenye historia nzuri ya jinsi ambavyo mahakama imekuwa mstari wa mbele kutatua changamoto za utoaji haki,” anasema.

Mwanasheria huyo ambaye pia ni mwanaharakati, ametaja fursa kadhaa za kisheria zinazoweza kutatua changamoto ya kuchelewa kesi kuwa ni pamoja na kupitia mapitio ya kimahakama, mashauri ya kikatiba na mamlaka ya mahakama.

“Mahakama imepewa nguvu kubwa kupokea malalamiko dhidi ya maamuzi ya kiutawala yaliyovunja misingi ya kikatiba na haki za asili katika kufanya maamuzi. Hapa imepewa nguvu kuchunguza kama wenye mamlaka wanatumia mamlaka yao sambamba na kuheshimu misingi ya haki,” anasema na kuongeza:

“Baadhi ya Watanzania wamekuwa wakienda Mahakamani kufungua mashauri dhidi ya viongozi mbalimbali na mahakama imekuwa ikitengua maamuzi yaliyofanyika,” anaongeza.

Kuhusu mahakama kama chombo pekee chenye mamlaka ya kupokea mashauri na malalamiko ya uvunjaji wa haki za kikatiba nchini, Olengurumwa anasema imepewa mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ukiukwaji wa haki za kikatiba kama zilivyoanishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi ya 30 ya Katiba ya Tanzania.

“Hapa Tanzania Mahakama imetumia mamlaka haya kwa kiwango cha chini sana ukilinganisha na nchi nyingine kama India, Afrika Kusini na Kenya,” anasema.

Anasema kuna Watanzania wengi wamekuwa wakiomba mahakama itengue sheria kandamizi ambazo hata Jaji Mkuu anazilalamikia lakini mashauri haya yameonekana kutokupewa kipaumbele na mahakama yenyewe.

“Mfano wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai imekuwa na walalamikaji wengi mahakamani lakini mahakama mara nyingi haioni umuhimu wa kutangaza vifungu vinavyolalamikiwa vifutwe kwa kuwa vinakinzana na Katiba,” anasema.

Anatoa mfano suala la dhamana kutoka shauri la Daudi Pete dhidi ya Jamhuri, Shauri Na. 80 la mwaka 1998 na mashauri mengine yaliyofuata hadi 2019 akisema Mahakama imeendelea kulifumbia macho suala la haki ya dhamana kwa mtuhumiwa.

“Majaji wa wakati ule kama Marehemu Jaji Mwalusanya na wengine kama Jaji Chipeta, Kisanga, Lugakingira waliendelea kusisitiza katika maamuzi yao kuwa suala la utoaji dhamana linapaswa kuwa la kimahakama zaidi na kuwapo sheria inayozuia dhamana ni sawa na kupokonya mamlaka ya mahakama,” anasema.

Anataja baadhi ya nchi kama Kenya, Canada, Africa Kusini na India Mahakama zao zimefanya maboresho makubwa ya mfumo jinai na haki za binadamu kupitia mashauri yanayopelekwa mahakamani kudai haki.

Kuhusu mamlaka ya kimahakama, Olengurumwa anasema wanaendelea kuipa Mahakama ya Tanzania lawama kwa asilimia 80, kwa sababu kuna ibara ya 107 A (1) ya Katiba ya Jamhuri wa Tanzania, ambayo inasema

Mahakama itakuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho au uamuzi wa mwisho kwenye masuala yote yanayohusu utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mahakama ya Tanzania ikiwa ni mamlaka ya mwisho katika utoaji wa haki katika nchi kwa mujibu wa Ibara ya 107 A (1) ya Katiba kama zilivyo nchi nyingine zinazotumia mfumo wa sheria za kawaida katika falsafa ya sheria, inayo mamlaka ya kutengeneza au kuibua kinga za kisheria ambazo zitasaidia kulinda haki za raia wa nchi hii dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka,” anasema.

Anasema Mahakama ya Tanzania ambayo inatumia mfumo wa sheria wa Common Law kama zilivyo mahakama zote zinazotumia mfumo huu, ina mamlaka ya asili ya mamlaka ya kudhibiti matumizi mabaya ya taratibu za kimahakama na kutoa haki ipasavyo chini ya sheria za Tanzania.

Akitoa mfano, anataja kesi ya James Gwagilo Vs Attorney General, Civil Case No. 23 of 1993 kuwa Mahakama ya Rufaa ilitengeneza kinga mpya ya kisheria ya “Haki ya Kupewa Sababu za Uamuzi” (Nullum Arbittrium Sine Rationibus) ambayo haikuwepo awali katika sheria za Tanzania na haikutambuliwa hata na mfumo wa sheria za kawaida za Uingerezam yaani English common law wa Uingereza.

Suala hilo pia linatazamwa na Dk Onesmo Kyauke, mwanasheria maarufu nchini akiungana na Olengurumwa kuhusu suala la dhamana.

Huku akitoa mfano wa nchi ya Kenya, Dk Kyauke anasema sheria zao zimeipa mahakama mamlaka ya kuamua utoaji wa dhamana.

“Kenya hata kosa la mauaji lina dhamana, ila inabidi upande wa mashtaka utoe sababu kwamba labda atahatarisha usalama wake au ataingilia ushahidi.

Kwa mfano kuna gavana mmoja kule Kenya ameshtakiwa kwa mauaji na amepewa dhamana. Kwa hiyo nafikiri Tanzania tupige hatua tufikie huko.

Hata hivyo, Dk Kyauke anasema kuhusu kauli ya Jaji Profesa Juma ya kutaka kesi zisifunguliwe kabla ya kufanyika kwa upelelezi, hiyo ina ujumbe kwa polisi na DPP.

“Hapo Jaji Mkuu anachosema, hao polisi hawapaswi kupeleka jalada kwa Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP) ili kutayarisha mashtaka kabla upelelezi wao haujakamilika.

“Kuna makosa kama mauaji huwezi ukasubiri mpaka upelelezi ukamilike, lakini makosa kama uhujumu uchumi, mtu achunguzwe kwanza kuliko kumkamata kwa miaka minne au mitano halafu unaambiwa upelelezi bado haujakamilika,” anasema Dk Kyauke.

Daktari mwingine wa Sheria ambaye ni mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam naye anasema mahakama haiwezi kukwepa lawama ya ucheleweshaji wa kesi.

Dk Jesse James, anasema: “Mahakama nao wana sehemu yao ya kusimamia kwa sababu wanaona mtu amekaa muda mrefu na kesi haijaanza. Wanaweza kutumia nyundo yao kwamba wanaiondoa hiyo kesi na kuitupa,” anasema Dk Jesse.

Hata hivyo, anasema Serikali imekuwa ikitumia mwanya huo kufuta kesi kisha kuwakamata tena watuhumiwa.

“Tatizo sheria haziipi mahakama mamlaka makubwa.”

Lakini Dk James anasema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba iko kwenye mkakati wa kurekebisha sheria ili kuzuia ukamataji wa watu kabla ya upelelezi haujakamilika.