BARAZA LA SALIM: Wapeni wanyonge viwanja watoke mabondeni

Wednesday May 29 2019

 

Kila ikinyesha mvua kubwa na kutokea mafuriko utasikia matangazo ya kila aina kutoka Idara ya Hali ya Hewa, Idara ya maafa na kadhalika.

Katika hayo watu wanaoishi katika maeneo hatarishi, kama kwenye mabonde hutakiwa kuhama na kwenda kutafuta maeneo salama.

Hili suala la mafuriko si la mzaha hata kidogo, lakini ukilifuatilia kwa karibu utaona kama vile ni linafanyiwa mchezo wa maigizo kwa lengo la kuchekesha umati.

Ninapoyasikia matangazo haya hujiuliza: Hawa wanaoyatoa walifanya utafiti kujua kwa nini hawa watu walijenga katika maeneo hayo na kwa nini sehemu hizo hazifanyiwi marekebisho ili ziwe salama kwa wakazi wake?

Kama tunataka kuwa wakweli, lazima tukubali tatizo hili linatokana na kuwepo ubinafsi mkubwa wa ugawaji wa viwanja Zanzibar.

Ukichunguza utakuta watu waliopewa viwanja vikubwa kwa ajili ya nyumba, bustani na kiwanja cha kuchezea kandanda kila pembe ya visiwani wakati wengine wamekosa hata kipande cha kujenga kibanda cha kuku.

Advertisement

Hawa wanaojiona ni watu wakubwa na wenzao wadogo wamechukua viwanja kwa majina yao, wake au waume zao, wajomba, mashangazi, watoto na wajukuu.

Watu hawa hawana aibu wala haya na hawajui vibaya. Upo wakati huundwa tume za kuchunguza viwanja vilivyogawiwa na Idara ya Majenzi.

Lakini, ndani ya tume hiyo wamo wafanyakazi wa idara walionyooshewa vidole kuhusika na kashfa hio. Hiki ni kichekesho.

Nimelizungumzia suala hili hata kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alipokuwa na utamaduni uliopotea wa kukutana na waandishi wa habari baada ya kila muda ili kumhoji juu ya masuala mbalimbali na kubadilishana mawazo.

Nilipendekeza kila pakigaiwa viwanja, kwa vile hizi ni zama za ukweli na uwazi, basi orodha ya watu waliopewa iwekwe hadharani na isiwe siri.

Ushauri huu wapo ambao hawakuupenda na walinuna, lakini bado ninaamini kufanya hivyo kutapunguza ufisadi wa baadhi ya watu wanaoshika na nafasi za uongozi au kukabidhiwa madaraka yanayohusu ugawaji wa viwanja Zanzibar.

Vilevile itaisaidia serikali kujisafisha na uoza unaofanywa na baadhi ya watumishi wake, wakiwemo viongozi, na kuonekana ni safi na haibagui.

Lakini, kwa namna viwanja vinavyogaiwa sasa kwa umuhimu kutolewa kwa akina fulani, wananchi wengi wamejenga dhana kwamba Zanzibar ina madaraja ya raia.

Tusikatae ubaguzi upo na unafumbiwamacho na ndio maana wapo wanaothubutu kubagua hadharani.

Kwa mfano hawa wabaguzi huwaambia watu waliochanganya damu na ambao wao na wazee wao wamezaliwa Zanzibar kuwa ni machotara wasiostahiki kuishi Visiwani.

Miongoni mwa wanaofanya hayo chambilicho wenyewe wamechanganya damu na wengine walikuja Zanzibar kwa mbeleko na bado hata mila na desturi za watu wa Vsiwani hazimo ndani ya damu zao.

Kinachosikitisha ni kuona viongozi wa nchi wanawafumbia macho huu na hawaguswi kwa vile ni haki yao kwa kuwa wao wapo juu ya sheria.

Wapo watu wanaojiita raia wa daraja la kwanza na ndio hupewa viwanja na watoto wao kupata nafasi za masomo nje ya nchi, ajira serikalini.

Wale pangu pakavu hawapati chochote. Katika kundi hili wapo waliokaa zaidi ya miaka 40 bila kupatiwa viwanja na serikali.

Wanapoulizia huonekana vichaa wanaodai haki wasiyostahiki. Unapokuwa na ubaguzi wa aina hii ndio wale wanaoitwa hohehahe wanaoishi kama mayatima au wakimbizi ambao hukimbilia hizo sehemu hatarishi na mabondeni. Wanafanya hivyo si kwa kupenda bali kwa shida ya kutaka kujijengea kibanda cha kujistiri.

Kosa lao ni umasikini na unyonge wao na hawana mtu wa kuwabeba kupata haki zao kama raia wengine.Haya maafa ya mvua ni ya kila mwaka na hatuoni wanaoathirika kupatiwa viwanja vilivyopimwa ili wajenge makazi mapya au maeneo hayo kufanyiwa matengenezo ili kupunguza maafa.

Mpaka haki itakapopatikana katika ugawaji wa viwanja na watu wote kuonekana sawa, maafa ya mvua yatatuandama kila mwaka.

Advertisement