SIASA ZA KITAA: Wasiojulikana ni picha za kina Rambo

Wednesday May 15 2019Dk Levy

Dk Levy 

Sasa ni Mdude Nyagali. Baada ya hesabu za Ben na Azory kuhesabiwa mpaka watu wakachoka. Tulianza na saa, siku baadaye ikawa wiki. Ikaja miezi kabla ya kupata uvivu na kuamua kuhesabu kwa miaka. Tunakoelekea tutaanza na karne, maana hata dalili za kupatikana hazipo.

Mdude. Alipata umaarufu kupitia uumbaji wa maneno na kisha kutupia mitandaoni. Na amesikika zaidi baada ya kutekwa kimiujiza flan hivi. Huku nyuma watu walewale wafanyao kilekile wakaanza tena ‘Bringi Baki Fulani Alaivu’. Ghafla akarudishwa.

Ustaa wa ‘watu wasiojulikana’, na wale ‘watekwaji’. unaenda sambamba na neno ‘bringi baki fulani’. Wamekuwa mastaa baada ya kutekwa na Wabongo wengi wamelijua neno ‘Bringi Baki’ baada ya matukio yao. Kabla ya hapo neno ‘bringi’ walijua ni vito vya thamani vinavyovaliwa shingoni na mikononi.

Tunakoelekea watu wataanza ‘kumisi’ tukio la kutekwa mtu. Ili mradi aingie mitandaoni na kuandika ‘Bringi Baki Fulani’. Maana imekuwa kama mchezo. Anatekwa mtu, zinasambaa taarifa kisha mitandaoni kunachafuka. Baada ya muda fulani tunaachana na tukio tunaendelea ni mengine.

Neno ‘Bringi Baki Fulani’ unaweza kudhani ni wimbo mpya wa WCB. Maana waandishi wa neno hili wanajisifu kabisa kuwa huko Kenya limekuwa lina-trend. Watu wanasahau hali anayopitia mtekwaji kwa muda huo, wanaanza kuona fahari kuungwa mkono na Wakenya kwa neno ‘Bringi Baki Fulani’?

Mimi binafsi siamini kama hawa ‘Watekaji’ ni Watanzania wenzetu. Hii mijitu itakuwa ndo ile mijamaa tuliyokuwa tunaitazama kwenye ‘muvi’ za kina Rambo na wenzake. Ambao walikuwa wanateka au kuua kijiji kizima bila kukamatwa. Hao ndo wameibuka upya na kuja kwetu.

‘Muvi’ kama ‘Missing ini Action’ nikiikumbuka naona kabisa ndio walewale wamekuja upya Bongo. Siku wakikamatwa hao ‘Watekaji’ ndipo utawaona kina Rambo. Chuck Norris, Van Damme, Cyborg na makatili yote. Ambayo kwenye ‘muvi’ yalikuwa yanatandika hata watu mia moja kwa mpigo bila kesi.

Kama kawaida sisi Wabongo tunaendelea kununua mikanda yao na kutazama hizi sinema za ‘watu wasiojulikana’. Safari hii hatukai tena sebuleni kwa mtu kutazama. Hapana, tunaishia mitandaoni tu na kuulizia “Injinia soma hiyo, na sasa ni Mdude Nyagali soma hiyooooo... siku ya ngapi?” Aiseeee.

Advertisement