Ziara ya Kenyatta na diplomasia na uchumi wa Afrika Mashariki

Sunday July 7 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Huwezi kuchagua jirani ila unaweza kuchagua rafiki. Lakini ni faraja zaidi pale unapopata jirani ambaye ni rafiki yako. Ndivyo ilivyo kwa Tanzania na Kenya, hizi ni nchi jirani na rafiki. Pia, marais wake wawili wamekuwa wakijitambulisha kama marafiki wanaotamani kudumisha mahusiano ya kijamii, uhuru wa bila mipaka katika biashara na hata kuoana.

Katika kudumisha hayo, Ijumaa Juni 5, mwaka huu, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitua katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita kwa mwaliko binafsi wa rafiki yake Rais John Magufuli.

Katika ziara hiyo ya binafsi, Rais Kenyatta anazungumzia udugu, urafiki na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Kenya.

Ziara hiyo imekuja katika kipindi ambacho uhusiano wa Tanzania na Kenya ulikuwa sehemu ya mjadala kutokana na masuala mbalimbali – chanya na wakati mwingine hasi.

Ingawa taarifa ya Ikulu ya Tanzania haikueleza bayana sababu za ziara hiyo, hapana shaka kwamba mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia baina ya Tanzania na Kenya yalijadiliwa.

Hii ni kwa sababu ziara hiyo imekuja kipindi ambacho Kenya inahitaji kuungwa mkono katika kuwania kuwa mwenyeji wa makao makuu ya eneo huru la biashara barani Afrika, ikishindana na nchi za Ghana, Eswatini, Madagascar na Misri.

Advertisement

Tayari nchi hizo zimewasilisha maombi kwenye Umoja wa Afrika. Ethiopia na Senegal pia zilikuwa zimeomba lakini zikajitoa baadaye.

Uamuzi wa nchi ipi itachaguliwa utajulikana leo katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) ambao Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan anashiriki kwa niaba ya Rais Magufuli nchini Niger.

Viongozi hao watapanga tarehe ya kuanza biashara kwenye eneo hilo huru ambalo litajulikana kama African Continental Free Trade, mataifa 52 kati ya 55 wametia saini makubaliano hayo.

Makao makuu hayo ya eneo huru la biashara litalenga kuwaunganisha watu bilioni 1.27 barani humo na pato lao la jumla ni dola trilioni 3.4; na kuondoa vikwazo vya biashara na ushuru kati ya mataifa wanachama.

Pamoja na hayo, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo anaitazama ziara hiyo kwa mapana zaidi, akisema inalenga kusawazisha dosari zote zinazotishia mahusiano ya diplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Pia, anasema ziara hiyo ya siku mbili inaweka misingi itakayoimarisha wepesi katika mwingiliano wa shughuli za kibiashara.

“Inawezekana wakajadiliana kuhusu masuala ya kibiashara ili kujenga hamasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohimiza suala la uhuru wa mipaka katika bidhaa, kazi na watu. Hamasa hii haijazingatiwa vizuri, kwa hiyo watajadili kuondoa hata vita ya kibiashara na kurejesha utulivu kwa Watanzania,” anasema.

Pamoja na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi za Kenya na Tanzania, pia yapo masuala kadhaa yanayotia doa, ikiwamo kauli iliyotolewa mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Charles Njagua, maarufu Jaguar ambayo imeibua hisia kali.

Hata hivyo, hatua ambayo Kenya imechukua dhidi ya mbunge huyo ya kumpandisha kizimbani bila kujali wadhifa wala itikadi yake, imeonyesha kuwa nchi hiyo haiko pamoja naye.

Mbunge huyo alitaka wageni wanaofanya biashara nchini humo wakiwamo Watanzania waondoke la sivyo wangefurushwa.

Hata hivyo, kulikuwapo na watu wanaomuunga mkono mbunge huyo, akiwamo mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale akisema serikali zinafaa kuwalinda wananchi wa kawaida kutopoteza kazi kwa idadi kubwa ya raia wa kigeni waliomo nchini.

Mbunge huyo alimtaja Sylvia Mulinge, mtaalamu wa mawasiliano katika kampuni ya Safaricom ya Kenya, kuwa alinyimwa fursa ya kufanya kazi katika kampuni ya Vodacom nchini Tanzania.

Mbunge huyo aligusia hata ng’ombe waliokamatwa kwa kuingizwa nchini kinyemela walivyopigwa mnada na jinsi vifaranga walioingizwa kinyume na taratibu walivyoteketezwa kwa moto katika mapambano dhidi ya maradhi ya mifugo.

Pamoja na masuala hayo yanayotatiza uhusiano ya Kenya na Tanzania, Shoo anasema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla wake zimekuwa katika mivutano ya kibiashara na maslahi ya kimipaka, akitolea mfano wa vita ya kibiashara kama inavyoonekana China na Marekani.

“Kwa mfano mazingira ya kuchoma vifaranga kutoka Kenya, kuna kipindi walikataa bidhaa zetu, pia mzozo wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Uganda, hadi Rwanda wakafunga mpaka, pia kuna mzozo wa Burundi na Rwanda, na vitu vingi vya Burundi vinapitia Dar es Salaam na vingine vinapitia Mombasa,” anasema Shoo akifafanua kuwa hayo ni mambo ambayo marais hayo wanayazungumzia.

“Biashara kubwa zaidi katika EAC ni kati ya Kenya na Tanzania kwa sababu Kenya inaongoza kwa uchumi mkubwa ikifuatiwa na Tanzania. Kwa hiyo Kenya wakikataa bidhaa zetu na sisi tukakataa bidhaa zao itaumiza uchumi wa nchi zote na pia bandari za Dar es Salaam na Mombasa zitaathiriwa.

Anaongeza “amani na mahusiano ya ujirani yatapungua sana, kwa hiyo ziara hiyo ni muhimu sana,” anasema.

Mbali na mzozo hiyo, Shoo anasema Tanzania kuonekana imara kuliko nchi zote EAC kisiasa na kiusalama, jambo linaloweza kuwa sehemu ya majadiliano kati ya wakuu hao wa wawili katika kutengeneza hamasa ya kuondoa dosari zilizopo.

Shoo hayuko mbali na mshauri wa masuala ya kidiplomasia hapa nchini, Profesa Kitojo Wetengere ambaye pia anasema jambo kubwa katika ziara hiyo litakuwa kuondoa dosari zinazoathiria mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia.

“Hivi karibuni kuna mbunge alichafua hali ya hewa. Baadaye Serikali ya Kenya ikakanusha kwamba yale ni maneno ya mtu binafsi. Hali hiyo ilionyesha kwamba mtu mmoja anaweza kuwa chanzo cha kuharibu mahusiano mazuri yaliyofanyika katika nchi hizo.

“Kwa hiyo ujio wa Rais Kenyatta, unataka kuonyesha kwa vitendo kwamba sisi ni majirani, ndugu na washirika katika biashara na uwekezaji na hii ndiyo diplomasia yenyewe,” anasema naibu mkurugenzi huyo wa zamani wa mafunzo, utafiti na ushauri wa kitaalamu katika Chuo cha Diplomasia.

Kauli za Kenyatta na Magufuli

Nje ya mazungumzo yao ya faragha, katika mkutano huo wa hadhara mjini Chato, Rais Kenyatta alisema anatamani siku moja kuona watu wa Afrika Mashariki wanakuwa sehemu ya ardhi moja isiyokuwa na vikazo vya aina yoyote.

“Wanasiasa wengine wanazungumza bila kufikiri, wengine wanaropoka tu, wawezaje kumwambia Mtanzania hawezi kufanya biashara Kenya, kumwambia Mtanzania hawezi tembea Kenya, hawezi kutafuta bibi (mchumba) Kenya, anaonya Rais Kenyatta akishangiliwa na wananchi wa Geita.

“Vile vile huwezi zuia Mkenya aje kufanya biashara yake Tanzania, hii siyo East Africa ya zamani, ya watu wenye fikra ndoto, za ujinga, ukabila, sisi tunataka Afrika Mashariki ya watu wenye maono ya mbele.”

Mwenyeji wa shughuli hiyo, Rais Magufuli aliungana na mgeni wake akisema jambo la msingi ni kuwaondolea shida Watanzania na Wakenya kwa kuweka miundombinu mizuri itakayosaidia kasi ya shughuli za kibiashara miongoni mwao.

Akitumia takwimu Rais Magufuli anasema biashara kati ya nchi hizo kwa mwaka jana zilikuwa na thamani ya Sh1.045 trilioni, wakati Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Sh482.43 bilioni na kuagiza bidhaa kutoka Kenya zenye thamani ya Sh563.07 bilioni.

Advertisement