Dilunga: Mtambo wa mabao unaowinda kiatu cha dhahabu

Monday May 13 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere anaongoza kwa kufunga mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa amefunga 20 hadi sasa katika mashindano hayo.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Rwanda, ameingia katika kundi la nyota wengine wanaowania tuzo ya mfungaji bora akiwemo Said Dilunga wa Ruvu Shooting mwenye mabao 10.

Dilunga anasema bado ana nafasi ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora kwa kuwa ligi hiyo bado inaendelea na Ruvu Shooting imebakiwa na mechi nne.

Nyota huyo anaungana na wengine wasiokuwa na majina katika Ligi Kuu, lakini wamekuwa tishio ambao ni Dickson Ambundo wa Alliance na Eliud Ambokile ambao wamefunga mabao 10 kila mmoja.

Wengine wanaoigia katika kapu hilo ni Heritier Makambo wa Yanga mwenye mabao 16 sawa na Salim Aiyee wa Mwadui ya Shinyanga, Emmanuel Okwi na John Bocco wa Simba ambao kila mmoja ana mabao 14.

Washambuliaji hao kila mmoja ana nafasi ya kutwaa kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora msimu huu endapo tu atachanga vyema karata kabla ya kumalizika mashindano hayo.

Advertisement

Tofauti na Kagere, Makambo, Okwi na Bocco wenye majina makubwa katika soka, Dilunga hafahamiki sana licha ya kucheza katika Ligi Kuu muda mrefu.

Idadi kubwa ya mashabiki wa soka wanaposikia jina la Dilunga moja kwa moja fikra zao zinakwenda kwa kiungo wa Simba, Hassani Dilunga ambaye amekuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hiyo msimu huu.

Wachezaji hao ambao si ndugu, wamekuwa katika mashindano hayo muda mrefu ingawa wanacheza namba tofauti ambapo Dilunga (Said) anacheza nafasi ya mshambuliaji.

Katika mahojiano maalumu na Spoti Mikiki, Dilunga anasema ana kiu ya kucheza timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ na alitamani kuwemo katika orodha ya wachezaji 39 walioitwa na kocha Emmanuel Amunike.

Amunike ameita wachezaji 39 kujiandaa na fainali za Kombe la mataifa ya Afrika (Afcon), zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri. Hata hivyo, ni wachezaji 23 pekee ndio watakwenda Misri kushiriki mashindano hayo.

Dilunga anasema hajakata tamaa kuitwa Taifa Stars kwa kuwa ni ndoto yake ya muda mrefu, atapambana kucheza kwa kiwango kikubwa ndani ya klabu yake ili kumshawishi kocha kumuita katika kikosi hicho.

“Nilitamani kwenda Misri katika fainali za Afcon, lakini kutoitwa kwangu hakunifanyi nisononeke maana yake ni kwamba kiwango hakijatosha kumshawishi kocha, hivyo natakiwa kuonyesha ubora zaidi.

“Waliotwa ni wachezaji wazuri watakwenda kulipigania Taifa, nitakuwa nyuma yao kipindi cha fainali hizo kama Watanzania wengine ambao watakuwa wakiombea dua njema timu yetu,”anasema Dilunga.

Siri ya Mabao

Dilunga anasema haikuwa kazi nyepesi kufikisha mabao 10 msimu huu na kuingia katika orodha ya washambuliaji wa Ligi Kuu wanaowania tuzo ya ufungaji bora.

Mshambuliaji huyo anasema juhudi, maarifa na ushirikiano mzuri wa wachezaji wenzake ni siri ya mafanikio yake katika kikosi cha Ruvu Shooting.

“Pamoja na ushirikiano ninaopata, lakini mimi binafsi nina mbinu zangu za kufunga mabao. Nina mbinu ya kukaa katika eneo zuri ambalo nina uhakika mpira utanifikia tu, lazima nitafunga,”anasema Dilunga.

Ataka rekodi

Mshambuliaji huyo anasema pamoja na kuipa mafanikio Ruvu Shooting anataka kuifikia rekodi ya Abduralhman Mussa aliyefunga mabao 14 msimu 2016/2017 katika kikosi hicho.

Dilunga anasema atakuwa na furaha endapo ataifikia rekodi hiyo au atavunja.

“Kuna mechi nne kabla ya kumalizika ligi msimu, nitahikikisha nakuwa na wastani wa kufunga katika kila mchezo ili niweze kufikia rekodi ya Abduralhman Mussa,”anasema Dilunga.

Simba, Yanga

Dilunga anasema mkakati wake ni kucheza soka la kulipwa Ulaya kama nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na wengine wanaocheza nje ya nchi.

Hata hivyo, anasema Simba na Yanga na klabu kongwe nchini na idadi kubwa ya wachezaji wa Tanzania wana kiu ya kuzitumikia, lakini kwa upande wake hatakuwa na haraka ya kufanya uamuzi.

“Niko tayari kucheza Simba au Yanga, lakini itabidi wafanye kazi kubwa ya kunitoa hapa, haitakuwa kazi rahisi kwasababu mimi ni mwajiriwa wa jeshi,”anasema Dilunga.

Mshambuliaji huyo hakusita kutaja mchezo wa kesho dhidi ya Yanga, akidai utakuwa wa aina yake kwa kuwa anataka kufunga ili kuipaisha Ruvu Shooting katika msimamo wa Ligi Kuu. “Tunataka kusogea katika nafasi za juu za msimamo wa ligi, tumefanya maandalizi ambayo yamelenga kwenda kuwashambulia si kujilinda.

“Hatuna tabia ya kucheza kwa kuzuia muda wote, ushindi katika mechi hiyo ni muhimu kwa kuwa utatuweka kwenye nafasi nzuri na kujinasua katika presha ya kushuka daraja,”anasema mshambuliaji huyo.

Advertisement