GOZI LA NG'OMBE: Asante mama Samatta

Monday May 27 2019

 

By Nicasius Agwanda

Wakati wa kujiandaa na sikukuu za Krismasi, mama mmoja aliyebarikiwa alikuwa anajiandaa kuingia chumba cha kujifungulia, ilikuwa Desemba 23 miaka 26 iliyopita. Akiwa na uchungu pengine alikuwa anatamani kupata mtoto wa kike au hakufahamu namna gani angeweza kumlea vyema.

Naam. Na hata wakati ulipofika mtoto akatoa sauti ya kilio kwa maana ya kutangaza uwepo wake duniani wazazi wakaamua kumpa jina la Mbwana.

Mihangaiko ya malezi kama wazazi mpaka leo ni miaka 26 na sasa kalamu zetu zinamwaga wino tukiwa na furaha kama Taifa kwa zawadi waliyotuletea, furaha ya kipaji cha mchezo pendwa kilivyokuwa baraka kwetu na chanzo cha amani ya moyo wetu linapokuja suala la ndani ya uwanja.

Kenya hawawezi kuturingia na Victor Wanyama, Uganda hawawezi kuleta kelele za Farouk Miya na hata Burundi hawawezi kutusema kwa kuwa na Berahino ambaye aliwahi kuwakataa kabla ya hali ya hewa ya timu ya Taifa ya England haijamkataa.

Tunaye mchezaji ambaye wikiendi kadhaa zilizopita alikuwa anasherekea ubingwa wa Jupiler ambalo ni jina la Ligi Kuu Ubelgiji.

Samatta si tu alikuwa mchezaji wa timu hiyo hapana, yeye ndo aliyeweka kijiko ndani ya kinywa cha Genk na kuwalisha mabao yake 23 ambayo yaliwapa ubingwa wa ligi.

Advertisement

Samatta ndiye aliyekuwa mshambuliaji aliyewapa umaana kwenye Ligi ya Europa kwa kuwapa mabao tisa katika mechi 12 tu alizocheza.

Samatta wa Tanzania alikuwa anageuka kuwa tunu ya ‘wazungu’ na kuimbwa jina lake kama ambavyo Mohammed Salah na Sadio Mane wanavyotamba pale Liverpool.

Kama haitoshi Samatta ameshinda tuzo ya ‘Ebony Shoe’ ambayo wanapewa wachezaji wenye asili ya Afrika ambao wamefanya vyema kwenye Ligi Kuu Ubeligiji, tuzo kubwa kwelikweli.

Jina la Mbwana Samatta limeandikwa kwa wino sawa na wachezaji walioshinda tuzo hiyo ambao ni Vincent Kompany, Daniel Amokachi, Marouane Fellaini, Romelu Lukaku, Michy Batshuayi, Mido na Youri Tielemens. Majina yote haya yamefanya mambo kwenye ligi kubwa hususani Ligi Kuu England.

Ndio, tunaye Samatta tunayejivunia na ambaye tukiwa tunaelekea katika michuano ya Afrika kule Misri tutakuwa na uchambuzi murua wa vituo vikubwa kuwa tuna mchezaji tishio, tuna moja ya washambuliaji mahiri, tuna sababu za kuwa hatari. Tunalo jina ambalo linawakilisha rangi zetu nne za bendera yetu vyema. Wakati Algeria atatajwa Mahrez, Kenya akitajwa Wanyama, Senegal akitajwa Mane huku kwetu itakuwepo picha kubwa ya Mbwana Samatta.

Huu ndio utofauti wetu na miaka mingi iliyopita ambayo iliwahi kuwa na usemi maarufu wa ‘Kichwa cha Mwendawazimu’.

Libarikiwe tumbo lililokuzaa ungeweza kuwa usemi maalumu ambao bibi yangu Imelda Agwanda angeweza kumwambia Samatta kwenye uso wake ili kuonyesha ni kwa namna gani Watanzania tunafurahi kila hatua anayopiga. Mapema mwaka huu niliandika makala mbili tofauti juu yake. Moja nilimwambia kuwa Mbwana Samatta, Funga, Funga, Funga na nyingine ilisomeka Samatta, Nimeiona Dhababu Mbele.

Makala ya kwanza ilimwambie afunge ili atimize ndoto yake ya kununua ‘private jet’ kwa sababu niliamini mwaka huu ungekuwa wake na pili ilikuwa baada ya mabao mawili dhidi ya Beskitas ambayo ililenga kukazia kwenye makala iliyopita kuwa sasa tunaweza kulifikia chimbo lenye madini ambalo Watanzania wanalitamani nayo ni ligi kubwa.

Dunia yenye uhaba wa wafungaji ndio dunia ambayo anaishi Samatta, dunia yenye utamaduni wa kuona ni kuamini ndiyo anayoikalia Samatta na uhitaji wa washambuliaji wa kisasa wanaoweza kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani kwenye eneo la mbele ndio anayoipatia Mbwana.

Yupo katika kipindi sahihi, eneo sahihi na wakati sahihi. Yupo katika wakati wa mavuno na wakati ambao tunaandaa bajeti zetu kununua jezi za klabu pendwa ya ligi kubwa atakayosajiliwa. Wakati wake ni huu.

Wino wangu una mengi ya kuandika lakini leo pamoja na wasifu nimeamua nimpongeze mama Samatta, ambaye duniani hatupo naye lakini alichotuachia ni baraka ya kipekee, alichotuachia kimekuwa nuru kwenye giza la soka tulilokuwemo.

Sijamsahau baba lakini huyu tunakutana maeneo na anapongezwa na wengi.

Huyu mama alituhifadhia zawadi kwa miezi tisa, akailea ikakua na leo inatupa raha, leo inatufanya tununue tiketi za Misri kwa ajili ya AFCON, leo inawafanya vijana wadogo waamini hakuna kinachoshindikana.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka hii, lakini pamoja na kwamba hautousoma ujumbe lakini kwa niaba ya Watanzania tunasema, AHSANTE MAMA SAMATTA.

Advertisement