Glovu ngeni zilivyomponza Mwakinyo kwa Tinampay

Mashabiki wengi wa ngumi wanajiuliza maswali namna Hassan Mwakinyo alivyocheza na kushinda dhidi ya Arnel Tinampay usiku wa Ijumaa iliyopita kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mwakinyo ambaye baada ya pambano hilo alikiri kushinda kwa tabu kwa matokeo ya pointi, ameanika namna glovu zilivyomponza ulingoni.

Baada ya kupanda ulingoni, mashabiki walilazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 10 huku Mwakinyo akijaribishwa glovu tofauti na kuvuliwa akiwa ulingoni.

“Ilikuwa ni changamoto ambayo wengi hawaijui, lakini glovu nilizopigania zilikuwa zinanibana,” alisema Mwakinyo na kuendelea.

“Sikuweza kukunja ngumi ipasavyo, kwani glovu zile hazikuniruhusu kufanya hivyo kwa kuwa hazikuwa zikinitosha.

Anasema licha ya kumbana, lakini pia zilitoka kutumika kwenye mapambano ya utangulizi hivyo zilikuwa na jasho, lakini alilazimika kucheza hivyo hivyo ili kutoonekana tofauti kwa mashabiki waliofurika uwanjani kumshuhudia.

“Pata picha umevaa viatu vipya halafu vinakubana, ndivyo ilikuwa upande wangu kwenye glovu zile, ilifikia mahali nilishindwa kukunja kabisa ngumi, lakini sikutaka kuacha pambano kwani ningeonekana natoa visingizio.

Katika pambano hilo, mabondia hao walipanda ulingoni saa 5.10 usiku na pambano likachezwa saa 5.25 usiku, baada ya vuta nikuvute ya glovu ambapo awali Mwakinyo alivaa glovu zake zenye nembo ya SportPesa lakini kocha wa Tinampay alizikataa wakiwa ulingoni.

“Sijui sababu ya kuzikataa glovu zangu, lakini changamoto ilikuja baada ya glovu zilizokuwepo taifa zote kutonitosha na tayari tuko ulingoni, nikalazimika kuvaa ambazo zinanibana.”