GOZI LA NG'OMBE: Griezmann, vazi la Barcelona lina taabu yake

Tuesday July 30 2019

 

By Nicasius Agwanda

Barcelona wameishi katika ndoto miaka mingi kwenye usiku wa giza, usiku wenye giza lisilowatisha wengi na usiku wenye mang’amung’amu yasiyowastua wapinzani. Barcelona waliishi kwenye ndoto hii wakiamini ndio uhalisia wa vazi walilovaa kwa kipindi kirefu, vazi la ‘tik taka’.

Vazi lililozaliwa pale La Masia, vazi lililonakishiwa na ubongo wa Johan Cruyff na baadaye kupigwa msasa na Pep Guardiola kabla halijaipendeza timu ya taifa ya Hispania. Ni vazi hili ambalo liliitikisa pete ya Sir Alex Ferguson pale Wembley na kufahamu kuwa muda wa vazi alilolizoea ulipita. Vazi ambalo angelivaa Valencia Old Trafford na kupendeza halikutakiwa tena na sasa wengi walivaa vazi lililoanzishwa La Masia na kuanza kusambaa sehemu nyingi kwa makocha vijana. Kila vazi huwa na kifungo chake, kwa Barcelona liliimarika wakati Xavi, Busquet, Iniesta na ndugu yao Lionel Messi walipoamua kuishi kwa upendo.

Hapa waliweza kumkaribisha kila mgeni na akapendeza ndani yake. Alipendeza David Villa, Sanchez, Neymar na Suarez. Wote hawa walipendeza kwa sababu kiini cha vazi kiliendelea kuishi na hata MSN iliendelea kupata huduma ya nyuzi za vazi hili kutoka kwenye kiini ambacho Guardiola alikipiga msasa vyema.

Dunia huwa haisimami, mshale wa sekunde haujawahi kuomba nafasi ya kupumua na majira ya mwaka yanabadilika kila uchwao. Hata mawio hayana tabia zinazofanana siku hizi, mambo yapo tofauti kila siku.

Mvi zilipoingia kwenye kichwa cha Xavi akatupa mkono wa kwaheri, kiini kikabaki na wachezaji wawili katikati na MSN ikaongeza nguvu.

Wakati wengi tukiwa tuna imani na yanayoendelea Camp Nou, mtoto mmoja mtukutu ambaye vazi lilianza kumpendeza maradufu akataka ufalme wake mahala kwingine akaondoka, anaitwa Neymar. Huyu wakaleta kijana ambaye alikuwa anaacha ziwa azibe viatu vyake anaitwa Ousmane Dembele.

Advertisement

Nyakati zikaendelea kuleta mvi kwenye vichwa vya watu, kipindi kikawa Iniesta. Akatuaga vichaa wa soka akaondoka zake. Barcelona hawakutumia akili nyingi, kwa sababu siku zote kuna mtu aliyefananishwa naye ambaye wangempata, anaitwa Coutinho.

Katika kipindi hiki chote kiwanda cha vazi lililowatisha wengi cha La Masia hakikuwa na wataalamu tena. Hakuna jina lililopatikana ambalo lingekuja kuboresha maisha Camp Nou. Coutinho akatua kwa fedha ambazo kimsingi ziliwapatia Liverpool Van Djik na kipa Allison Becker.

Sio Dembele wala Coutinho walioweza walau kuvutia kwenye vazi walilovishwa na wanaonekana wanalichukia. Wameshindwa na hawaonekani kuelekea kuweza na kiwanda hakizalishi tena nyuzi zinazoendana na vazi lao, kiwanda kimeexpire.

Barcelona wanaendelea na bahati nasibu, kupata nyuzi kwenye viwanda vya nje, nyuzi za gharama na nyuzi ambazo hazijatokana na asili na utamaduni wa vazi la Catalunya. Hawana namna, lazima waagize nje lazima wawapate akina Griezmann.

Mfaransa anayekuja kujaribu kuleta jaribio jingine kwenye vazi linaloonekana kuanza kupoteza mvuto wake.

Vazi ambalo kiraka kinachoitwa Malcolm kipo kama kimepoteza njia na hakipo mahala pake. Dunia haiwasubiri Barcelona na fedha zinanuka hivyo lazima wazimwage nje wenye nyuzi wazichukue. Griezmann ni mchezaji bora, lakini kama ilivyokuwa kwa Dembele, Coutinho hawajawahi kuishi uhalisia huu.

Uhalisia wa La Masia ambapo ncha ya mkuki ni Lionel Messi. Ni Ngumu na ndio maana inaacha swali zaidi. Haieleweki hata kama Neymar atarejea maana inaweza kuwa hatari zaidi iwapo kama itamchukua muda kuzoea. Yale ya Coutinho na Dembele kisha Malcolm yanatisha. Karibu Griezmann, karibu Camp Nou, karibu Catalunya, karibu katika vazi ambalo limechanika mahala pa Neymar, Iniesta na Xavi. Halivutii kwa kipindi kirefu Sasa na wengi tunategemea wewe ndio nuru mpya. Unaweza Kutizama akina Coutinho walishindwa nini.

Moja ya mambo yatakayovutia ni suala zima la kuhakikisha kuwa tunaketi mbele ya televisheni na kutazama Barcelona mpya. Barcelona inayoweza kuwa na Neymar aliyeongezeka ndani yake pia. Barelona mpya yenye Griezmann aliyependwa pale Atletico Madrid, Griezmann atakayetizamwa dhidi ya Real Madrid kwenye El Classico.

Tutakuwa na glasi yenye mvinyo kutafuta jina jipya kama ilivyokuwa kwa MSN wakati Barcelona inatikisa Ulaya au kutafuta dhihaka mpya kama tulivyofanya kwa akina Coutinho. Maisha ndivyo yalivyo, sherehe ni muda wote iwe wakati wa furaha au wakati wa majonzi, yaani watafurahi adui zako au watafurahi washirika wako. Ni jambo jema kuona changamoto yako mpya na inautia kwelikweli. Lakini miguu ipo kwenye breki, hatutaki kuwa na uhakika kwa sababu hili vazi lina taabu zake lakini karibu sana.

Advertisement