GOZI LA NG'OMBE: Haruna Moshi na kijana muuza kahawa

Katika pitapita zangu nimefika sehemu nikakuta watu wana furaha isiyokuwa na kifani, kutazama vyema wamevalia jezi za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Nikasogea kwa sababu kimsingi sikuwa na haraka yoyote ile ili kufahamu nini kinaendelea au kuna taarifa gani inayohusu soka kwa sababu Watanzania na soka la timu ya taifa kwa sasa ni ndugu wanaopendana.

Kufika nikakutana na sura ninazozifahamu, Athumani Idd Chuji, Haruna Moshi ‘Boban’, Nizar Khalfan na mdogo wao Mbwana Samatta.

Majina hayo yalinifanya niketi kwa sababu lazima kinachozungumzwa kilikuwa kizito na chenye tija kwa ajili ya ubongo wangu.

Nilikuta Nizar anasimulia maisha yake ya Marekani, akajinasibu na goli alilowafunga Senegal pale CCM Kirumba lakini pia urafiki wake na Marcio Maximo na namna ambavyo alimwamini.

Nizar alikuwa kifua mbele kwa sababu ya balaa alilolifanya pale Vancouver Whitecaps na kwamba yeye ndiye aliyefungulia watu dunia na kuonyesha umuhimu wa kucheza nje.

Athumani Idd yeye alikuwa anahoji kuna wachezaji wangapi waliocheza kwa kiwango kikubwa kwenye vilabu viwili vya Simba na Yanga kumzidi?

Alikuwa anacheka kuona viungo wa sasa namna wanavyoshindwa kutawanya mipira kwa Msuva na Samatta kwenye timu ya Taifa na namna ambavyo walitakiwa watizame enzi zake, alivyokuwa na Godfrey Bonny mambo yalivyokuwa mepesi kwa washambuliaji.

Haruna Moshi kama kawaida na ukimya wake alikuwa anawasikiliza kama yule kaka ambaye anaona wadogo zake wanavyopiga kelele wakati yeye ndiye anayefahamu kila kitu.

Alikuwa anatabasamu kwa kila neno lakini akamshika begani Samatta na kumwambia waulize hata hawa akina Nizar na Chuji kama walishakutana na Mtanzania mwenye miguu yangu.

Waulize kama waliwahi kukutana na ulimbo ulionasa mpira vyema kuliko wangu. Waambie wakufahamishe kama waliwahi kucheza na kipaji kama changu au wakwambie kama waliwahi kufanya balaa kama ninaloweza kufanya. Samatta akitikisa kichwa, Haruna akaongeza kuwa niliishi Sweden kwa mkataba wa uhakika kwenye klabu ya Gefle IF, nilikuwa Mtanzania niliyebeba ndoto ya wachezaji Ulaya na sio Marekani kwa Nizar.

Ndio, Samatta alikuwa ameketi na wachezaji ambao waliishi kwenye zama ambazo Marcio Maximo alikuwa anahamasisha washabiki kujaa uwanjani kwenda kuona miguu yao ambayo hata yeye kuna wakati alihisi imezaliwa kwenye fukwe za Rio De Janeiro kabla ya kuhamishwa na kuja kupambana na zile za Coco Beach.

Samatta alikuwa ameketi na kuwasikiliza wanaume watatu ambao kwa wakati wao walibeba ndoto ya mtoto wa Kitanzania mwenye kipaji cha soka, ndoto ya mtoto aliyekuwa na tamaa ya kuondoka Morogoro, Tabora, Kigoma au Mwanza ili afike Dar es Salaam na kucheza “derby” ya Kariakoo.

Waliuishi uhalisia wa wengi na hata Samatta alikiri pale kuwa walikuwa ni vipaji ambavyo ni nadra kuviona na kuwa alijifunza mengi kupitia wao.

Kijana mmoja wa kahawa akapita na alipowaona akawapa ofa ya kahawa ya bure lakini huyu ndiye aliyeweka uhalisia wa mazungumzo yalivyopaswa kuwa.

Aliwapa kahawa sio kwa sababu ya ubora wao, bali kwa sababu walikuwa wameketi na Mbwana Samatta. Aliamini wale ni marafiki wa Mbwana Samatta na walikuwa na bahati iliyoje kuzungumza na kijana ambaye anabeba sio tu ndoto ya Watanzania bali na furaha yao kwa ujumla kila anapofunga kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Alipomaliza kutuwekea kila mmoja kahawa ya moto, akauliza kama Samatta anawaza kutua Manchester United kwa sababu yeye kama shabiki wa klabu hiyo haelewi kazi wanayofanya Martial na Rashford.

Huyu ni kijana mwenye miaka takribani ishirini ambaye ukiwaza unakuja kufahamu kuwa hana haki ya kutokuwakumbuka Athumani Idd, Haruna na Nizar. Wakati wao wanafanya makubwa, huyu alikuwa haruhusiwi kwenda uwanjani bila mzazi lakini anaona kwa sasa kila anayoyafanya Samatta.

Lakini vijana wa sasa wanasoma vitu, mitandao ya kijamii inawasaidia pia. Hakuna historia iliyoandikwa ya watu hawa na pia hawakuweza kuishi kwenye uhalisia wao.

Athumani Idd kwa haraka akamuuliza kijana yule, kama anawafahamu Haruna Moshi, Athumani Idd na Nizar Khalfan. Bila kusita kijana akasema alikuwa anasikiliza redioni wakati wanafanya mambo yao pale Uwanja wa Taifa, aliwahi kusikia walikwenda nje na wakarudi bila kuelewa walishindwa nini.

Akaenda mbali na kuuliza wana umri gani kwa sasa. Kwa kuropoka nikasema hawazidi miaka 32 kila mmoja. Akasonya na kukusanya vikombe vyake vilivyokuwa tupu tayari, akaondoka zake akimsihi Samatta aendelee kupambana na akasema kumbe Haruna Moshi na wenzie walitakiwa wawe wanamalizia makali yao pale England. Nami nikastuka, kumbe nilikuwa ndotoni.