Hasara ya Sh2 trilioni yanukia EPL

Ikiwa msimu huu utafutwa kutokana na janga la corona, klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL) huenda zikapata hasara ya takribani Sh2 trilioni.

Hata hivyo, kuna taarifa kwamba huenda EPL ikarejea mwezi ujao, lakini kutokana na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kusimamisha kwa muda usiojulikana Ligi ya Mabingwa na ile ya Europa, huenda pia England ikalazimika kufuta ligi zake.

Fedha hizo ni zile zitokanazo na makusanyo ya fungu la udhamini wa ligi, udhamini wa runinga, mahudhurio ya viwanjani na faida ya huduma zitolewazo viwanjani kwa mashabiki.

Mchambuzi wa masuala ya udhamini wa michezo, Dk Peter Rohlmann anaamini kuwa hakuna namna ambayo klabu 20 zinazoshiriki EPL zitakwepa kupata hasara hiyo ambayo inazinyemelea.

“Hiyo hasara itakuwa ni janga. Inajumuisha fedha zinazopotea kutokana na tiketi za viingilio viwanjani, fedha ya udhamini zinazopotea, bonasi, huduma za vyakula na uuzaji wa bidhaa za klabu,” alisema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Rohlmann, hasara hiyo itapungua hadi kufikia kiasi cha zaidi ya Sh300 bilioni ikiwa tu ligi hiyo itaendelea kuchezwa bila uwepo wa mashabiki viwanjani.

Taharuki kama hiyo haionekani kuikumba Ligi Kuu England pekee, bali tayari baadhi ya ligi nyingine kongwe zimeshaanza kuhofia kuwa itakuwa ni vigumu kuchezwa bila kuruhusu mashabiki viwanjani.

Hofu kama hiyo imeonyeshwa pia na mtendaji mkuu wa Ligi Kuu Ujerumani, Christian Seifert ambaye amedai halitakuwa jambo lenye tija kwa ligi kuchezwa bila mashabiki.

“Hakuna mtu ambaye ni shabiki wa mechi kuchezwa pasipo uwepo wa watazamaji, lakini inaweza kuwa njia pekee kwa klabu kufanya biashara. Bila mapato ya runinga, udhamini na viingilio, tutahimili kwa muda mfupi tu,” alisema Seifert.

“Mechi kuchezwa bila uwepo wa watazamaji itakuwa ni njia ya kustahimili kwa muda mfupi na si vinginevyo.”

Athari hiyo haionekani itagusa tu klabu, bali hata Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa) nalo linanyemelewa kuingia hasara ya kiasi kikubwa cha fedha ikiwa mashindano yake mbalimbali hayatachezwa.

Kwa mujibu wa tathmini ya Rohlmann, Uefa itapata hasara ya zaidi ya Sh1 trilioni ikiwa mashindano ya Euro 2020 hayatachezwa.