Kelvin: Kinda la Stars lililobeba matumaini ya Watanzania Afcon

Monday May 13 2019

 

By Thomas Ng’itu, Mwananchi

Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inajiandaa kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Taifa Stars itashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39 ambapo mara ya mwisho ilishiriki mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.

Wakati Taifa Stars ikijiandaa kwa fainali hizo, Kocha Emmanuel Amunike ameita wachezaji 39 wanaotarajiwa kuingia kambini kwa mechi za kirafiki kabla ya kwenda Misri.

Miongoni mwa wachezaji walioitwa na Amunike ni mshambuliaji kinda wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’, Kelvin John ambaye kiwango chake uwanjani kimewakuna wengi.

Idadi kubwa ya mashabiki wa soka, wanampa nafasi kubwa Kelvin kung’ara katika mashindano hayo makubwa Afrika kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao.

Kelvin anayecheza nafasi ya mshambuliaji halisi, alionyesha kiwango bora katika fainali hizo ingawa Serengeti Boys ilifungwa mechi zote tatu dhidi ya Nigeria, Uganda na Angola.

Advertisement

Kiwango chake kimewavutia mawakala mbalimbali waliokuja nchini kushuhudia fainali hizo na wamemtaja kinda huyo ni mchezaji mwenye sifa ya kucheza katika klabu za Ulaya.

Haikushangaza nyota wa zamani wa Liverpool na Senegal, El Hadji Diouf kusifu kazi nzuri ya Kelvin katika fainali hizo. Nguli huyo alikuwepo nchini katika mashindano hayo.

Spoti Mikiki ilizungumza na Kelvin kuhusu mikakati yake baada ya kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars akiwa ndiye mchezaji mwenye umri mdogo.

Taifa Stars

Kelvin anasema siri ya kuitwa Taifa Stars ni mafanikio aliyopata katika fainali za Afcon ambazo zilimtambulisha kwa Amunike ambaye alikuwa miongoni mwa maofisa walioshiriki katika uratibu wa mashindano hayo akitokea Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kinda huyo anasema katika maisha yake ya soka hakuwahi kuwa na ndoto ya kuitwa moja kwa moja Taifa Stars itakayoshiriki fainali za Afcon.

“Ilikuwa ni mshangao wa aina yake, kuitwa timu ya Taifa tena ukiwa na umri mdogo si jambo dogo. Nashukuru kupata fursa hii nitaitumia vizuri,”a lisema Kelvin ambaye ameitwa katika kikosi hicho na kinda mwenzake Claryo Boniphace.

Mbwana Samatta

Endapo Kelvin atapenya katika mchujo wa kwenda Misri, atakutana na Samatta anayecheza soka la kulipwa Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.

“Ni fahari kucheza na Samatta kwasababu ni mchezaji mzuri, lakini ni changamoto kubwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza,” anasema kinda huyo.

Hata hivyo, anasema atapambana katika mazoezi kumshawishi Amunike kumpa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ili atimize ndoto ya kucheza soka nje kama ilivyokuwa kwa Samatta.

“Samatta ni mchezaji anayejituma muda wote, napenda kujifunza kupitia kwake kwa kuongeza nidhamu ndani ya uwanja. Naamini nidhamu imechangia kupata mafanikio,” anasema Kelvin.

Kiwango bora cha Kelvin kimewavutia mashabiki wa soka ambao wamempa jina la Mbappe wakimfanisha na nyota wa Paris Saint Germain (PSG), Kylian Mbappe.

Ajax, Man City

Kiwango cha mchezaji huyo kimezivutia klabu za Ulaya ikiwemo Ajax Amsterdam ya Uholanzi iliyocheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutolewa na Tottenham Hotspur.

Kelvin anasema mbali na Ajax, pia anawindwa na Manchester City ya England ambayo imeonyesha ni ya kumsajili.

Kinda huyo anasema mazungumzo baina pande hizo yanaendelea na jukuku hilo lipo mikononi mwa wasimamizi wake.

“Wasimamizi wangu wanaendelea na mazungumzo, mimi nipo tayari kucheza sehemu yoyote kama mambo yatakuwa sawa mtaona naondoka lakini kwasasa mazungumzo yanaendelea,”alisema Kelvin. Kelvin ana rekodi ya kufunga mabao 25 katika mashindano ya shule za msingi na 14 sekondari.

Advertisement