Namna ya kumpa huduma aliyevunjika mkono

Monday May 27 2019

 

Wakati wa kushiriki michezo au mazoezi ajali mbalimbali zinaweza kumpata mwanamichezo ikiwemo kuvunjika mifupa ya mkono.

Katika maisha yetu ya kila siku ya kimichezo ni kawaida kuona mwanamichezo amevunjika mkono akiwa uwanjani na watu wasijue cha kufanya au pengine eneo hilo lisiwe na mtoa huduma ya kwanza.

Leo tutaona namna ya kumpa huduma ya kwanza mwanamichezo aliyevunjika mkono eneo la chini ya kiwiko.

Eneo la chini ya mkono huwa na mifupa miwili inayounda ungio la kiwiko na eneo la juu huwa na mfupa mmoja unaounda ungio la bega kwa juu.

Mkono ambao umevunjika kwa wastani mpaka uvunjikaji mkubwa huweza kuonekana kwa kutazama mabadiliko katika mkono huo ikiwemo uwepo wa uvimbe , kubadilika kwa rangi eneo hilo na umbile lisilokuwa la kiasilia.

Vilevile mgonjwa huonekana mwenye hisia za maumivu makali huku akishindwa kuutumia mkono huo. Jambo la kwanza katika kumsaidia mgonjwa wa aina hii nikutomwondoa eneo hilo, mtathimini hapo hapo ili kubaini kama ni kuvunjika au kuteguka au ni majeraha ya tishu laini.

Advertisement

Kumbuka kuwa wewe sio mtaalamu wa afya huna ujuzi wa kurudishia mfupa uliovunjika, unachofanya ni huduma ya kwanza wakati ukitafuta namna ya kumfikisha katika huduma za afya au ukisubiri msaada.

Mtulize mjeruhiwa wa mkono hapo hapo alipojijeruhi wakati ukitafuta namna ya kumpa huduma. Kumuondoa kunaweza kusababisha mtikisiko wa vipande vya mifupa vilivyovunjika na kusababisha majeraha zaidi na maumivu makali.

Vipande vya mfupa uliovunjika vinapotikisika huweza kujeruhi tishu laini ikiwemo mishipa ya fahamu.

Tafuta vifaa tiba mbadala katika eneo uliopo, tafuta kati ya vitu vifuatavyo ikiwemo banzi bapa, kipande cha mbao, mti ulionyooka au boksi gumu na kitambaa au bandeji.

Hatua ya pili ya kufanya, jaribu kuuweka mkono huo katika ulalo wake wa kiasili kwa uangalifu huku ukiupa usaidizi mkono huo, zungushia kitambaa au bandeji katika mkono huo bila kufunika vidole.

Kisha chukua mkono huo uulaze kwa juu katika banzi/mbao, chukua kitambaa kingine ufunge ili kuunganisha banzi na mkono huo uliovunjika.

Hakikisha vidole vya mikono vinakuwa wazi, vile vile usikaze sana bandeji au kitambaa ulichotumia kuvingirisha mkono huo.

Gusa vidole vya mkono huo kama havina baridi au kufa ganzi, unapokuta viashiria hivi ina maana umeukaza mkono kupita kiasi hivyo kubana mishipa ya damu inayotawanya damu eneo hilo.

Ning’iniza mkono huo kwa kuufunga na kitambaa kingine kwa kuzungushia shingoni mkono ukiwa katika mkao wa nyuzi tisini ukigusa kifua.

Inakubalika pia kumwekea barafu ili kupunguza maumivu wakati unampeleka katika huduma za afya.

Unapofikia hatua hii, mgonjwa anakuwa amepata utulivu hivyo anaweza kupelekwa katika huduma za afya kupata matibabu zaidi kwa mtaalamu.

Advertisement