Safari ya Simba kutwaa ubingwa ilianzia hapa

Monday May 27 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Si jambo la kushangaza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya kufikisha pointi 91 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote ile kwenye mashindano hayo ambayo yamebakiza raundi moja kabla ya kumalizika kesho.

Tangu nusu ya msimu wa ligi, Simba ilishaonesha dalili zote za kutetea taji lao msimu huu kama ilivyofanya msimu uliopita na hilo lilichangiwa na sababu mbalimbali za ndani na nje ya uwanja.

Hakuna njia ya mkato kuyafikia mafanikio na hilo linajidhihirisha kwenye safari ya Simba katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ambao mwisho wa siku ilifanikiwa kupata na kukata ngebe za watani wao wa jadi Yanga ambayo ilikuwa inafukuzia kwa kasi.

Kwa kulitambua hilo, Spoti Mikiki inajaribu kukuangazia sababu au maeneo gani ambayo yameifanya Simba kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ambalo linaifanya kuwa imechukua kombe hilo mara 20.

Nguvu ya kiuchumi

Simba ilitenga bajeti ya takribani Sh6 bilioni kwa ajili ya kujiendesha msimu huu wa ligi, fedha ambazo zimetumika katika usajili, maandalizi ya timu, malipo ya mishahara, posho, gharama za kambi, usafiri, matibabu na shughuli za utawala.

Advertisement

Matokeo ya hili yalionekana baada ya Simba kuwapa huduma nzuri za daraja la juu wachezaji wake na kuwaweka katika hali nzuri kisaikolojia. Bila shaka huduma hizo zote zilikuwa kama deni lililoongeza morali na hamasa yao katika kuipigania timu hiyo hadi ikafanikiwa kutwaa ubingwa.

Wakati Simba ikitumia fungu la fedha, hali ilikuwa tofauti kwa klabu nyingine ambazo zimekuwa na changamoto ya kiuchumi na zinashiriki kwenye ligi zikiwa na bajeti ndogo ambazo ziliachwa mbali na ile ya Simba jambo ambalo limezipa wakati mgumu kupambana nayo kwenye ligi.

Usajili

Kiasi cha fedha kinachokadiriwa kufikia Sh1.3 bilioni kilitumiwa na Simba kuimarisha kikosi chake msimu huu kwa kusajili nyota wapya na kuongeza mikataba ya baadhi ya wachezaji wengine ambao mikataba yao ilikuwa inaelekea ukingoni.

Baadhi ya nyota wapya waliosajiliwa ni Meddie Kagere, Clatous Chama, Deogratias Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Paschal Wawa na Adam Salamba.

Kwa bahati nzuri kundi kubwa la wachezaji wapya waliosajiliwa lilifanya vizuri na baadhi yao wamekuwa nyota tegemeo kwenye kikosi cha kwanza na wametoa mchango mkubwa ndani ya timu hiyo wakichagizwa na wale ambao waliwakuta katika kikosi.

Mfano, katika pointi 91 ambazo zimeipatia Simba ubingwa wa Ligi Kuu, Kagere pekee amechangia kuipa timu hiyo takribani pointi 22 ambazo kama wasingezipata, leo hii ubingwa wasingepata na wangejikuta wako nafasi ya tatu.

Maandalizi bora ya msimu

Wakati kundi kubwa la timu likiweka kambi ya maandalizi hapa nchini na nyingine zikifanya hivyo kwa kuchelewa, Simba yenyewe ilikwenda Uturuki ambako iliweka kambi ya wiki mbili.

Katika kambi hiyo, walikutana na miundombinu na vifaa bora ambavyo viliwapa nafasi ya kujiandaa vizuri hasa kujenga stamina kwa wachezaji. Pia walipata nafasi ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya timu imara ambazo ziliwapa mazoezi ya kutosha.

Benchi la ufundi

Hakuna namna unayoweza kueleza mafanikio ya Simba pasipo kumtaja Kocha Patrick Aussems na wasaidizi wake ambao wamefanya kazi kubwa kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri.

Kwa kutambua ubora wa kikosi chake, Aussems amekuwa akipanga wachezaji sahihi katika mechi husika kulingana na aina ya mpinzani na katika mechi nyingi aliingia na mbinu ya kushambulia na kufunguka dakika zote za mchezo.

Mbinu hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani katika idadi kubwa ya mechi ilipata ushindi ingawa baadhi walipoteza pointi.

Na katika benchi hilo la ufundi la Simba, kuna mtu anaitwa Adel Zrane ambaye ni mtaalamu wa viungo na kuwaweka fiti wachezaji ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuwafanya wachezaji wa Simba wamudu ratiba ngumu ambayo walikuwa nayo kwenye Ligi Kuu ambapo kuna wakati walilazimika kucheza mechi nne mfululizo za mikoani ndani ya siku 10.

Ubora wa wachezaji

Maandalizi na huduma nzuri ambazo Simba imepata zimekuwa chachu ya kuimarisha ufanisi na mchango wa wachezaji wao ndani ya uwanja ambapo wamekuwa wakicheza kwa ari na morali ya hali ya juu tofauti na wachezaji wa timu nyingine ambazo wachezaji wao wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi.

Pamoja na uelewano wa kitimu ambao Simba wameonyesha, pia kiwango na ubora wa mchezaji mmojamoja vimekuwa ni silaha muhimu ya timu hiyo kutwaa ubingwa kwani mara kadhaa ambapo timu ilionekana kuelemewa, kundi kubwa la mechi za namna hiyo ziliamriwa kwa uwezo binafsi wa mchezaji mmoja.

Na katika kudhihirisha hilo, Aishi Manula ndiye kipa ambaye ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara chache zaidi kuliko mwingine yeyote akiwa amefungwa mabao 14 tu, lakini sehemu nyingine inayothihirisha ubora wa mchezaji mmoja mmoja wa Simba ulikuwa lulu kwao kutwaa ubingwa ni safu yao ya ushambuliaji ambapo kabla ya mechi ya jana dhidi ya Biashara United ilikuwa imepachika mabao 54.

Kagere ndiye kinara ambaye kabla ya jana alikuwa na mabao 23, akifuatiwa na John Bocco aliyefunga mabao 16 wakati Emmanuel Okwi yeye amepachika mabao 15 na hata Adam Salamba ambaye huwa hapangwi mara kwa mara yeye amepachika mabao manne.

Kimataifa

Baada ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kutolewa kwenye robo fainali, kiu ya mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba ilikuwa ni kuona timu yao inakwenda kushiriki kwa mara nyingine mashindano ya Klabu Afrika msimu ujao na ivuke au ifike pale ilipoishia sasa hivi.

Lakini kwa bahati mbaya Simba ilitolewa mapema na Mashujaa FC ya Kigoma katika raundi ya kwanza ya Kombe la Azam Sports Federation ambalo bingwa wake ndio anawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Nafasi pekee ambayo Simba iliyobaki nayo mkononi ilikuwa ni kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kulikuwa na ulazima wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ili warudi tena kimataifa na si vinginevyo.

Ni wazi kwamba hilo liliongeza msukumo na umakini wa hali ya juu kwenye Ligi Kuu na ambako ilikuwa inafanya maandalizi mazuri kwenye kila mchezo ili ipate pointi tatu muhimu ambazo zingeiwezesha kutwaa ubingwa kama ilivyofanya.

Maoni ya wadau

“Mafanikio ya soka yanachagizwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji ambao timu au klabu husika zimefanya, hivyo ukitazama hilo na kulinganisha na kinachotokea kwenye Ligi Kuu, utakubaliana na mimi kwamba Simba imestahili kutwaa ubingwa lakini ni fundisho kwa klabu nyingine kwamba hakuna njia ya mkato katika soka,” alisema beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa.

Kiungo wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Said alisema Simba ilifanya maandalizi mazuri na ilistahili kutwaa ubingwa msimu huu.

“Ukitazama ubora wa mchezaji mmoja mmoja kwenye Ligi Kuu wa Simba wamewaacha wengi mbali wengine wa timu za Ligi Kuu lakini bado hao wachezaji wake wana kazi ya kuthibitisha ubora wao kwenye mashindano ya kimataifa (Klabu Bingwa Afrika),” alisema Jemedari.

Advertisement