Breaking News

Ubora wa kikosi Simba uko hapa

Tuesday August 6 2019

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Klabu za Simba na Yanga zipo katika hatua ya mwisho ya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika 2019/2020.

Simba itafungua pazia la michuano ya kimataifa ugenini kwa kuvaana na UD Songo ya Msumbiji Agosti 10 kabla ya kuanza kibarua cha kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Agosti 23.

Hatua ya Simba kufanya mabadiliko makubwa kwa kuwapunguza baadhi ya wachezaji katika kikosi chake na kuongeza wapya katika usajili wa dirisha kubwa inaweza kuwa silaha pekee kwa kikosi hicho kupata mafanikio msimu ujao.

Pamoja na maandalizi ya msimu mpya, Simba yenye maskani Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, leo inazindua rasmi jezi zake ambazo itazitumia kwa michuano ya msimu ujao.

Pia kesho itahitimisha wiki yake ya Simba Day ambapo itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa, jijini.

Kocha Patrick Aussems anasema kambi ya Afrika Kusini imempa picha ya kutambua ubora wa kikosi chake kwa michuano ya msimu ujao.

Advertisement

“Ingawa niliwakosa baadhi ya wachezaji walioitwa timu ya Taifa, lakini kwa ujumla wachezaji wamepata mafunzo bora na wamenipa matumaini ya kufanya vyema msimu ujao.

Awali, klabu hiyo ilifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na wachezaji kutembelea Hospitali ya Ocean Road kutoa misaada kwa wagonjwa.

Wakati Simba iliweka kambi nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu ujao, Yanga ilijichimbia kambini mkoani Morogoro kwa programu za mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu na Kimataifa. Yanga pia itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kila pembe ya dunia, kinapofika kipindi cha maandalizi ya msimu mpya, klabu mbalimbali zinatoka katika miji yao na kwenda kujichimbia nje ili kupata utulivu wa kufanya maandalizi kabambe.

Hapa nchini utamaduni huo upo hasa kwa Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikitoka nje ya Dar es Salaam kwenda kuweka kambi ama mikoani au nje ya nchi kujiandaa na msimu mpya.

Kuelekea msimu mpya wa mashindano wa 2019/2020, Spoti Mikiki inajaribu kuangazia maandalizi ya Simba ambayo itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi.

Ubora wa Kikosi

Katika dirisha kubwa la usajili, Simba ilifanya mabadiliko makubwa kwa kuwapunguza baadhi ya wachezaji kwenye kikosi chake na kuongeza wapya ili kuimarisha timu yao msimu ujao.

Wachezaji ambao imeachana nao ni Zana Coulibaly, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Adam Salamba, Deogratias Munishi, Asante Kwasi, Nicholas Gyan, Murushid Juuko, Mohammed Ibrahim, Paul Bukaba, Abdul Selemani na James Kotei.

Katika kuimarisha kikosi chake imewaongeza Tairone Silva, Wilker Da Silva, Gerson Fraga Vieira, Sharaf Shiboub, Francis Kahata, Beno Kakolanya, Ibrahim Ajibu, Haruna Shamte, Miraji Athumani, Gadiel Michael na Deo Kanda.

Pia iliwaongeza mikataba Jonas Mkude, Said Ndemla, Aishi Manula, John Bocco, Paschal Wawa, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Meddie Kagere na Cletous Chama.

Kimsingi ni usajili ulio na balansi kwani umejaribu kuongezea nguvu katika nafasi za wachezaji wa idara zote kuanzia ile ya kipa, mabeki, viungo na washambuliaji.

Kana kwamba haitoshi, Simba ilimuongeza mtaalamu wa tiba ya viungo, Paulo Gomez Dardenne kwenye benchi lake la ufundi kwa ajili ya kumsaidia Kocha Patrick Aussems.

Kambi

Ikilenga wachezaji wake wapate maandalizi mazuri na hali ya utulivu katika kujiandaa na msimu mpya, Simba ilijichimbia Afrika Kusini ambako iliweka kambi katika mji wa Rustenbeg.

Kambi hiyo ilikuwa ni ya siku 15 ilianza Julai 15 ambayo ndio Simba ilitua nchini humo. Kambi ilihusisha programu za uwanjani na zile za ‘gym’ ambazo zilifanyika kwa nyakati tofauti asubuhi na jioni.

Baada ya kumaliza programu za ufundi uwanjani na zile za kuwaweka wachezaji fiti, Simba iligeukia mechi za kirafiki ikiwa ni sehemu ya kujipima ni kwa kiasi gani wachezaji wamezifanyia kazi programu ambazo wamezifanya nchini Afrika Kusini.

Walianza kucheza mechi dhidi ya Orbret Tvet iliyoshinda mabao 4-0, iliifunga Platinum Stars 4-1, ilitoka sare ya bao 1-1 na Township Rollers na mchezo wao wa mwisho ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Orlando Pirates.

Ubora

Moja ya maeneo ambayo yanaipa jeuri Simba katika msimu ujao ni safu yake ya ushambuliaji.

Katika msimu uliopita, ilipachika jumla ya mabao 77 na mabao zaidi ya 50 yalifungwa na washambuliaji wake watatu John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Licha ya kumkosa Okwi, Simba imezidi kuimarika katika eneo hilo baada ya kumuongeza mshambuliaji Wilker Da Silva ambaye ni raia wa Brazil.

Mbali na Silva ambaye ataongeza nguvu kwa ushambuliaji wa kati, pia Simba imeongeza pia viungo washambuliaji na mawinga ambao ni chachu ya kuzalisha na kufunga mabao pindi nafasi inapopatikana.

Mastaa hao ni Kanda, Miraji, Kahata na Ajibu ambao wanaongeza wigo wa uteuzi wa kikosi cha kwanza na mbinu au mfumo kulingana na aina ya mpinzani wanayekabiliana naye.

Pia kuna taswira ya wazi kwamba jambo jingine ambalo litaiimarisha Simba msimu ujao ni ufiti na utimamu wa mwili wa wachezaji wake ambao umetokana na kambi ya maandalizi Afrika Kusini.

Simba inakabiliwa na mashindano manne tofauti hivyo ufiti na utimamu huo utawafanya wachezaji waweze kuhimili ratiba ngumu ya mechi ambazo ziko mbele yao.

Udhaifu

Changamoto inayoweka kuikabili Simba msimu ujao ni kuchelewa kupata muunganiko mzuri wa kitimu.

Kundi kubwa la wachezaji limesajiliwa kutoka nchi na mabara tofauti ambao baadhi yao hata mazingira na hali ya hewa ya Tanzania na Afrika hawajazoea.

Hawa wanahitaji muda kidogo kumudu mazingira ya Simba na soka la Tanzania hususani falsafa na mbinu za benchi la ufundi jambo ambalo linaweza kuwagharimu kwa kuchelewa kupata muunganiko mzuri ndani ya uwanja.

Bahati mbaya kundi kubwa la wachezaji walioachwa walikuwa wameanza kumudu aina ya soka la Simba na walishatengeneza muunganiko mzuri na wenzao hivyo kuondoka kwao pasipo shaka kutaifanya timu hiyo kuanza upya.

Matarajio

Kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, hapana shaka, Simba itakuwa ni moja wa washindani wa ubingwa na inaingia ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo kutokana na maandalizi waliyofanya.

Kama ilivyo kwenye ligi ndivyo inavyoonekana itakavyokuwa katika michuano ya Kombe la FA.

Lakini kwenye mashindano ya kimataifa, kwa namna ambavyo wamekibadilisha kikosi chao, mafanikio makubwa ambayo Simba inaonekana watapata ni kufika hatua ya makundi ingawa haionyeshi kama itaweza kufika pale walikofikia msimu uliopita ambako ni hatua ya robo fainali au kwenda juu zaidi.

Advertisement