Uongozi mpya Yanga na dhamana ya mabadiliko

Monday May 13 2019

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Mei 5, 2019 Yanga ilifanya ilifanya Uchaguzi Mkuu ambao uliwaingiza madarakani Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanane (8) wapya wa kamati ya utendaji ambao watahudumu kwa miaka minne kwenye klabu hiyo.

Kocha wa soka na mtaalamu wa masuala ya kilimo na mbolea, Dk Mshindo Msolla alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa klabu hiyo, baada ya kupata jumla ya kura 1276 kati ya 1341, akimbwaga Dk Jonas Tiboroha ambaye alipata kura 60.

Dk Msolla atasaidiwa na Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela ambaye aliibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo akiwashinda Chota Magege, Tito Osoro, Yono Kevella na Janeth Mbene.

Vigogo hao wawili wapya wa Yanga wataiongoza kamati ya utendaji inayoundwa na wajumbe Hamad Islam, Injinia Mwaseba, Dominick Albinus, Kamugisha Kalokola, Arafat Haji, Salum Ruvila, Saad Khimji na Rodgres Gumbo.

Uongozi mpya wa Yanga unaingia madarakani ukiwa na changamoto kadhaa ambazo unapaswa kuzifanyia kazi katika kipindi ambacho utakuwepo madarakani kwa maana ya muda wa miaka minne kama Katiba ya klabu hiyo inavyoainisha.

Yanga ina madeni ambayo inadaiwa na wachezaji wake yanayotokana na malimbikizo ya stahiki za mishahara, posho na fedha za usajili kwa baadhi yao.

Advertisement

Pia ina kibarua cha kufanya usajili imara kuwa na kikosi bora cha ushindani kwa ajili ya misimu inayofuata, lakini uongozi una jukumu la kuhakikisha timu hiyo inakuwa na misuli imara ya kiuchumi kuweza kushindana ndani na nje ya nchi.

Hizo ni changamoto ambazo zinapaswa kutatuliwa kwa muda mfupi lakini kuna suala la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo jambo ambalo nalo ni moja kati ya vitu vinavyosubiriwa kwa hamu na wanachama pamoja na mashabiki wa klabu hiyo kuona likifanywa na uongozi huo mpya wa Yanga.

Kwanini kuna ulazima na haja kwa Yanga kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake ambayo inaulazimisha uongozi mpya kuhakikisha klabu hiyo inapitia mara baada ya kuingia madarakani?

Spoti Mikiki linakuletea sababu zinazoilazimisha Yanga kubadili mfumo wa uendeshaji wake kutoka ule wa kawaida uliodumu kwa muda mrefu na kuingia kwenye uwekezaji.

Katiba ya Yanga

Kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Yanga na kuingia kwenye uwekezaji ni suala lililomo kwenye katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2010 lakini tangu mwaka 2007, Wanayanga walisharuhusu kuingia kwenye uwekezaji kama inavyoainisha ibara ya 56 ya katiba ya Yanga.

1. “Kutakuwa na Kampuni itakayojulikana kama ‘Young Africans Sports Corpration Limited’ ambayo itasajiliwa chini ya Sheria ya makampuni kama Kampuni ya Umma yenye hisa (“kampuni”),

2. Wanachama wote wa klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007 wako hai watakuwa kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakazopata kwa mujibu wa mwafaka wa Yanga uliofikiwa na Wanayanga Juni 22, 2006.

3. Klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika kampuni.

4. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.

5. Kampuni itakuwa chombo maalumu cha klabu kitakachokuwa na dhamana ya kufanya biashara ambazo klabu ya ‘Young Africans Sports Club’ itaona kuwa inafaa kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi,” inafafanua Katiba ya Yanga.

Mabadiliko Simba

Mwaka 2016, Simba ilianzisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na ilipofika mwaka 2018, wanachama wa klabu hiyo kwa kauli moja walikubaliana na suala hilo na kumpitisha mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’ kama mwekezaji ndani ya klabu hiyo kwa asilimia 49 ya hisa za Simba.

Tangu Simba ilipoingia kwenye mfumo huo, mambo yameonekana kuinyookea ikifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita na inaelekea kutetea msimu huu, pia imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Hapana shaka kwamba kiu ya kutaka kuona timu yao inafanya makubwa sawa au kuzidi yale ambayo watani wao wamepata ni jambo linaloipa hamu Yanga kubadili mfumo wa uendeshaji katika klabu yao.

Anguko la kiuchumi

Tangu mwenyekiti na aliyekuwa mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji alipojiuzulu mwaka 2017, hali ya mambo ndani ya Yanga imebadilika na klabu hiyo imekuwa ikiyumba kiuchumi kwasababu sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji zilikuwa zikifanywa na fedha zake za mfukoni.

Maisha ya kutegemea fedha za mifukoni mwa watu wachache yamekuwa kama utamaduni wa klabu za Tanzania kwa muda mrefu hasa Yanga.

Aina ya maisha ambayo Yanga imepitia baada ya mwenyekiti wake kujiuzulu, yanaipa hamu ya kuingia kwenye uwekezaji ikiamini kwamba utaiondoa katika maisha ya kutegemea fedha za mifukoni mwa watu na kuwa uchumi imara na endelevu.

Ulinzi wa rasilimali

Uendeshaji wa klabu kwa mtindo wa uwekezaji unaleta uhakika wa ulinzi wa nembo au chapa ya klabu kwani unakuwa na usimamizi thabiti tofauti na mfumo wa sasa ambao suala la usimamizi wa rasilimali za klabu ni changamoto kubwa.

Kwa kutambua kiu ya mabadiliko ambayo wanachama wa Yanga wanayo, wadau mbalimbali wa klabu hiyo wameonekana kutilia mkazo suala hilo wakiamini litaleta tija kwa timu.

“Nimekuwa nikisikia mabadiliko tangu mwaka 2006, nini kinakwamisha? Nadhani viongozi waliopita pamoja na kazi kubwa waliyokuwa wakifanya, walikuwa wakijisahau kwenye hilo.

“Nitaanza na hilo na imani yangu ni kwamba tutalimaliza kwa ushirikiano na viongozi wenzangu pamoja na wanachama wenyewe,” anasema Dk Msolla.

Katika hotuba yake kwa wanachama kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika aliutaka uongozi mpya utakaochaguliwa, kuhakikisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo unafanyika haraka kutokana na mahitaji ya klabu.

“Tumepitia kipindi kigumu, tuliachiwa timu, Baraza la Wadhamini, tumesakamwa lakini yote yanaelekea ukingoni.

“Tunahitaji mabadiliko yafanyike ndani ya miezi sita baada ya uchaguzi, huo ndio mkakati,” alisema Waziri George Mkuchika ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini.

Mgombea wa nafasi ya ujumbe ambaye alianguka kwenye uchaguzi huo, Christopher Kashililika anasema ana imani kubwa na uongozi ulioingia madarakani utabadili mfumo wa uendeshaji.

“Nawapongeza viongozi ambao wamechaguliwa. Wote tuligombea tukiwa na lengo moja la kutaka kuitoa klabu hapa ilipo na kuifanya iwe moja ya klabu kubwa katika medani ya mchezo wa soka Afrika.

“Mfumo wa maisha hivi sasa umebadilika na soka ni sayansi na biashara, hivyo naamini uongozi wetu mpya utatuongoza vyema katika kuingia katika mfumo wa kisasa ambao ni wa uwekezaji ili tuweze kuwa na msingi imara wa kiuchumi ndani ya klabu yetu,” anasema Kashililika.

Advertisement