Wababe wa London Marathon hawa hapa

Jana Jumapili ilikuwa siku ya kushuhudiwa mbio kubwa ulimwenguni kama sio kuwepo kwa ugonjwa wa corona ambao umesababisha mambo mengi kusimama.

Mashindano ya riadha ya Rotterdam Marathon yalikuwa yafanyike huko Uholanzi, lakini sasa yatafanyika Oktoba 24. Ila London na Boston Marathon yaliyokuwa yafanyike mwezi huu nayo yamepigwa kalenda. Leo tunaitazama London Marathon kwa ufupi. Kwa mara ya kwanza ilifanyika Machi 29, 1981 ambapo mwanariadha Dick Beardsley, raia wa Marekani alimaliza wa kwanza akitumia muda wa saa 2:11:48.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Mashindano hayo yalikuwa ni wazo la mwandishi wa habari Christ Brasher na mwanariadha John Disley na kwa mara ya kwanza yalipata maombi ya washiriki zaidi ya 20,000 na waandaaji wakawachuja hadi kufikia washiriki 6,747 lakini waliomaliza walikuwa 6,255. Mwanariadha Dirk Beardsley ndiye aliyekuwa kinara kwa wanaume akitumia saa 2:11:48 huku Joyce Smith akimaliza wa kwanza kwa wanawake akitumia saa 2:29:57 wote wakiwa ni raia wa Marekani.

London Marathon ni mashindano ya mialiko binafsi na yana tofauti kubwa na yale ya Jumuiya ya Madola, Mashindano ya Dunia na hata ya Olimpiki kwa kuwa yanahusisha ushiriki wa nchi, lakini London ni mialiko binafsi ya wanariadha wenye sifa za kipekee.

Wanaoalikwa London Marathon ni wale tu waliopata medali kwenye mashindano makubwa au wenye muda mzuri (bora), ndio maana tangu kuanza kwa mashindano hayo Tanzania haijafikisha wanariadha 30 walioshiriki.

REKODI ZILIVYO

Katrin Dorre-Heining raia wa Ujerumani ndiye mwanariadha wa kwanza kuwa bingwa mara tatu mfululizo kwa upande wa wanawake akifanya hivyo 1992, 1993, na 1994 huku kwa wanaume Dionicio Ceron, raia wa Mexico akifanya hivyo 1994, 1995, na 1995.

Mwanariadha Igrid Kristiansen wa Norway ndiye amekuwa bingwa mara nyingi kwa wanawake akifanya hivyo mara nne mwaka 1985, 1985, 1987 na 1988 wakati kwa wanaume Eliud Kipchoge akiwa bingwa mara nne mwaka 2015, 2016 na 2018 na 2019.

Nchi ya Kenya ndio imetamba zaidi kwa kuwa mabingwa mara nyingi kwenye mashindano hayo kwa kuchukua ubingwa mara 14 kwa upande wa wanaume huku kwa wanawake wakiwa mabingwa mara 12.

WABABE WA MUDA

Rekodi ya muda ilianza kuwekwa na Khalidi Khannouchi mwaka 2002 ya saa 2:05:38 iliyodumu miaka mitano kabla ya kuvunjwa na Mkenya Martin Lel mwaka 2008 akitumia saa 2:05:19, lakini Samuel Wanjiru akaivunja mwaka 2009 akitumia saa 2:05:10, mwaka 2011 Emmanuel Mutai akaivunja akitumia saa 2:04:40.

Wakenya waliendelea kutesa kwani Wilson Kipsang mwaka 2014 akaivunja akitumia saa 2:04:29 kabla ya Eliud Kipchoge kuivunja kwa saa 2:03:05 mwaka 2016 na 2019 akaivunja tena kwa kuweka muda wa saa 2:02:37.

Kwa wanawake mwanariadha Grete Waitz wa Norway ndiye alikuwa wa kwanza ikiwa mwaka 1983 akiweka muda wa saa 2:25:29, lakini mwanariadha Paula Radcliffe wa Uingereza ndiye anayeshikilia rekodi ya muda aliyoiweka mwaka 2003 ya saa 2:15:25 na haijavunjwa hadi leo.

Kwa Tanzania, mwanariadha Samson Ramadhani ndiye mwenye rekodi nzuri kwenye mbio za London na haijavunjwa hadi leo akiiweka mwaka 2005 alipomaliza nafasi ya tano akitumia muda wa saa 2:08:01.

TANZANIA YAJITOSA

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki mwaka 1983 ikiwakilishwa na mwanariadha Juma Ikangaa aliyemaliza nafasi ya saba kwa kutumia muda wa saa 2:12:12 huku akishuhudiwa Mwingereza Miki Gratton akinyakua ubingwa kwa kutumia muda wa saa 2:09:57 na pia kocha Zakaria Barie alishiriki mwaka 1983 na 1984.

WENGINE WALIOSHIRIKI

Wanariadha wengine waliowahi kushiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Gidamis Shahanga, Suleiman Nyambui na Alfredo Shahanga aliyemaliza nafasi ya sita mwaka 1991 kwa kutumia muda wa saa 2:11:20 huku Samwel Samawe akiishia njiani.

Robert Naali mwaka 1992 alimaliza nafasi ya tatu katika mashindano hayo akitumia muda wa saa 2:10:11 huku Antonio Pinto raia wa Ureno akiwa bingwa akitumia saa 2:10:02 yaani wakipishana kwa sekunde tatu.

Mwaka 1995 mwanariadha Samson Ramadhan aliweza kuwanyanyasa wafukuza upepo wengi wakiamini atakwenda kuvunja rekodi ya dunia kabla ya misuli kuanza kukaza akibakiza kilomita chache na hatimaye alifanikiwa kumaliza nafasi ya tano akitumia saa 2:08:01.

SIMBU YUMO

Mwaka 2017, Mtanzania Alphonce Simbu alikuwa miongoni mwa washiriki katika mashindano hayo na kumaliza katika nafasi ya tano kwa kutumia muda wa saa 2:09:10.

Baada ya kutoka hapo mwaka huohuo, Simbu alifanya yake kwenye mbio za dunia zilizofanyika London kwa kunyakua medali ya shaba akimaliza katika nafasi ya tatu akitumia muda wa saa 2:09:51.

Simbu alipata nafasi hiyo ikiwa mwaka mmoja baada ya kufanya vyema kwenye michezo ya Olimpiki kule Rio de Janeiro, Brazil, alikotumia muda wa saa 2:11:15 na sasa amefuzu katika mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Tokyo, Japan mwaka ujao.