Warriors, Raptors kazi ipo fainali NBA Marekani

Hatimaye fainali ya jumla ya Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), msimu huu itazikutanisha timu za Golden State Warriors.

Golden State Warriors inacheza fainali hiyo baada ya kuibuka bingwa wa ukanda wa Magharibi ilipoifunga Portland Trail Blazers pointi 4-0.

Toronto Raptors itacheza fainali hiyo ikiwakilisha ukanda wa Mashariki baada ya kuwaondoa wapinzani wao wakubwa Milwaukee Bucks kwenye mchezo wa sita na kupata ushindi wa pointi 4-2 alfajiri ya Jumapili.

Timu hizo zitapambana katika fainali ya jumla ya msimu huu ambapo mechi baina yao itaanza kuchezwa usiku wa kuamkia Ijumaa wiki hii kusaka bingwa wa ligi hiyo maarufu zaidi duniani.

Golden State Warriors itacheza fainali ya tano mfululizo baada ya kucheza fainali nne zilizopita na kushinda ubingwa mara tatu ikipoteza moja.

Warriors inasaka ubingwa wa tatu mfululizo baada ya kutwaa fainali zote mbili zilizopita mbele ya waliokuwa mabingwa mfululizo wa kanda ya Mashariki,Cleveland Cavaliers ambao wamepoteana msimu huu kutokana na kuondokewa na LeBron James.

Kwa upande wao Toronto Raptors, itakuwa fainali yao ya kwanza kucheza katika historia yao kwa kuwa hawakuwahi kufanya hivyo.

Raptors licha ya kutopewa nafasi ya kufika fainali hii, imefanikiwa kuwa na matokeo ya aina yake msimu huu ikiwemo kuziondoa timu mbili ngumu zilizopewa nafasi ya kucheza fainali.

Timu hizo ni Philadelphia 76ers ya wakali Joel Embiid na Jimmy Butler kwenye nusu fainali ya ukanda wa Mashariki na katika fainali ikiing’oa Milwaukee Bucks iliyotabiriwa kucheza fainali.

Shujaa wa Raptors ni Kawhi Leonard ambaye amekuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo msimu huu akiibeba katika mechi zake huku akisaidiwa vyema na wakali wengine akina Serge Ibaka, Pascal Siakam na Kyle Lowry.

Warriors kwa upande wao wanabebwa zaidi na uwepo wa nyota Stephen Curry ambaye amekuwa na mwendelezo bora kila msimu hususani mechi za mtoano huku akisaidiwa vyema na wakali akina Draymond Green,Klay Thompson na Kevin Durant ambao wamekuwa na mchezo mzuri katika mashindano hayo.