Malawi,Tanzania kufanya kongamano la biashara Mbeya

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Edwin Rutageruka

Muktasari:

Lengo la kongamano hilo ni  kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.


Dar es Salaam.Tanzania na Malawi zitaandaa kongamano la pamoja la biashara  na uwekezaji litakalofanyika Julai 26 na 27 mkoani Mbeya.

Lengo la kongamano hilo ni  kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Hayo yamesemwa leo Machi 22 katika taarifa iliyotumwa kwenye vyomba vya habari na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Edwin Rutageruka, kwamba kwa mda mrefu wafanya biashara kutoka Malawi wamekuwa wakifanya  biashara  chini katika mfumo usio rasmi.

Uamuzi wa kuandaa kongamano la siku mbili ulitokana na mkutano mwingine wa kibiashara ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makala Machi 20, na kuvutia wafanyabiashara wa mpakani.

“Katika kikao kati ya mabalozi wa Tanzania na Malawi tulikubaliana kuandaa kongamano kubwa la kibiashara likiwa na lengo la kuvutia wawekezaji kutoka Malawi na Tanzania,” amesema  Rutageruka.

Katika kikao hicho balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndiolowe ameelezwa kufurahishwa kwake na kupongeza uamuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo na hivyo kuchangia kuboresha maisha ya wqananchi wa pande zote mbili.

Naye balozi wa Tanzania nchini Malawi Martin Mashiba amesema kuwa nchi za Tanzania na Malawi ni majirani kihistoria na kijiografia hivyo kongamano hilo litadumisha uhusiano uliopo na kuendelea kukuza uhusiano wa kibiashara.