Malipo ya watumishi yazua jambo Chuo Kikuu Dar es Salaam

Muktasari:

Baada ya kutangazwa kwa orodha hiyo wiki iliyopita, wahadhiri hao kupitia Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), wamekuwa katika majadiliano kwa njia mbalimbali ikiwamo kukutana na kutumia makundi ya ‘WhatsApp’ kujua hatima ya madai yao na leo viongozi wao wanakwenda Dodoma kuonana na maofisa wa Ofisi ya Rais-Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Orodha ya malipo ya malimbikizo ya madai ya watumishi wa umma imeibua sintofahamu kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuonyesha kuwa wanaostahili kulipwa mwezi huu ni 33 tu kati ya zaidi ya 1,000 wanaodai.

Baada ya kutangazwa kwa orodha hiyo wiki iliyopita, wahadhiri hao kupitia Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), wamekuwa katika majadiliano kwa njia mbalimbali ikiwamo kukutana na kutumia makundi ya ‘WhatsApp’ kujua hatima ya madai yao na leo viongozi wao wanakwenda Dodoma kuonana na maofisa wa Ofisi ya Rais-Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Orodha iliyotolewa Ijumaa iliyopita na katibu mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro inaonyesha kwamba watumishi watakaolipwa malimbikizo ya madai yao mwezi huu ni 27,389. Ilitolewa muda mfupi baada ya waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuzungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kueleza kwamba Serikali imetenga Sh43.39 bilioni za madai mbalimbali yaliyohakikiwa yatakayolipwa pamoja na mshahara wa mwezi huu kwa watumishi hao.

Dk Mpango alisema fedha hizo zinajumuisha madai ya watumishi ya zaidi ya miaka 10 iliyopita na kwamba kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, hadi kufikia Julai Mosi mwaka jana kulikuwa na madai ya mishahara yenye jumla ya Sh127.6 bilioni kwa watumishi 82,111.

Kuhusu kilio hicho cha Udasa, Dk Ndumbaro alisema, “Orodha iliyotolewa ni ile iliyokamilika kuhakikiwa, uhakiki bado unaendelea na hiyo iliyotoka ni ile iliyokuwa tayari katika mfumo wa mishahara. Uhakiki unaendelea kwa watumishi wote wa umma ambao wana madai yanayohusiana na mishahara.”

Jana, wahadhiri wapatao 50 walikutana nje ya lango la kuingilia Ukumbi wa Nkrumah wa chuo hicho kwa kile walichodai wamekuwa wakinyimwa ukumbi kuanzia saa 7:20 mchana na kumalizika saa 8.04 mchana wakijadiliana kuhusu suala hilo wakiwa wamesimama.

Mwandishi wetu aliyekuwapo katika mkusanyiko huo alishuhudia washiriki wakizungumza kwa hisia walipokuwa wakichangia hoja huku baadhi wakiutupia lawama uongozi huo wa chuo.

“Tunataka kujua madai yetu tunalipwa au hatulipwi? Kwa nini majina yetu hayapo na wengine yapo? Lakini kwa nini majina yetu hayapo? tunaambiwa fomu zimepelekwa kule mbona sisi hatujui?” alihoji mmoja wa wahadhiri hao huku akidakiwa na mwingine; “Kama hatutakiwi kudai basi tuelezwe, mwenyekiti (wa Udasa – Dk George Kahangwa) tunaomba utuletee yote na je, ni miaka mingapi tunadai? Wengine tangu mwaka 2012 tunatakiwa kulipwa.”

Mwingine alisema “Eti mnampongeza DVC (Naibu Makamu Mkuu wa Chuo), mnampongeza kwa lipi? Au tunatofautiana katika kufikiri, tunapaswa kuhoji madai yetu tutalipwa nini? Tunatakiwa kupongeza na kudai madai yetu kama wana Udasa hakuna wa kuja kutupigania.”

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Dk Kahangwa alisema, “Ni kweli madai hayo yapo na kwa sasa siwezi kuzungumza kwa kina ila yapo na kesho (leo) tunakwenda Dodoma ofisi ya Utumishi.”

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye alisema wameshawasiliana na Utumishi na kuahidiwa kuwa suala hilo litafanyiwa kazi.

“Kama umeongea na mwenyekiti wa Udasa atakuwa amekueleza tulipofikia na kesho (leo) Udasa na maofisa wetu wanakwenda Dodoma. Lakini hili si tatizo la hapa tu hata taasisi nyingine za umma nao majina hayajatoka na Utumishi imesema inayafanyia kazi,” alisema Profesa Anangisye.

Kuhusu kufanyia kikao nje ya ukumbi, makamu mkuu huyo alisema, “Hatuwezi kugombana na wahadhiri wetu, ukumbi ulikuwa tayari na shughuli nyingine, ingekuwa ngumu kuwapa ukumbi uliokwisha kupewa watu wengine.”