Mambo matano yaliyowatikisa CCM, upinzani

Muktasari:

Wakati wabunge wa upinzani wakiinyooshea kidole Serikali kwa kushindwa kukabiliana na Matukio ya utekaji, mauaji, ajira, Katiba na umaskini, mambo hayo yamelitikisa Bunge kwa wabunge wa upinzani na CCM kushambuliana kwa hoja. Mvutano huo ulishika kasi zaidi Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alipochangia na mawaziri wawili kuomba kiti cha Spika kimtake afute maoni yake.

Dodoma. Matukio matano ya utekaji, mauaji, ajira, Katiba na umaskini yamelitikisa Bunge kwa wabunge wa upinzani na CCM kushambuliana kwa hoja.

Wabunge hao walizua mjadala mkali jana wakati wakichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2019/2020.

Wakati wabunge wa upinzani wakiinyooshea kidole Serikali kwa kushindwa kukabiliana nayo mambo hayo, wenzao wa chama tawala waliisifu.

Mvutano huo ulishika kasi zaidi Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alipochangia na mawaziri wawili kuomba kiti cha Spika kimtake afute maoni yake.

Awali, Sugu alisema kuna kipindi Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwahi kusema viongozi wapimwe akili, lakini hakumwelewa ila sasa anamwelewa kuwa ni vyema viongozi wakapimwa akili.

“Sasa hivi unaweza kushangaa tu mkuu wa wilaya ama wa mkoa anainuka huko anazungumza mambo ambayo hayaeleweki,” alisema Sugu.

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama kusimama na kuomba kuhusu utaratibu.

Alisema Bunge la 10 lilikufa na kwa mujibu wa kanuni si sahihi mbunge kutoa kauli za kuudhi.

Hata hivyo, Sugu alikataa kufuta maneno hayo na kutaka Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kufuta mchango wote kwa sababu haoni ni wapi pa kufuta.

Akiendelea kuchangia, mbunge huyo alikemea tabia ya polisi kufanya mauaji kwa raia.

Alisema jimboni kwake zaidi ya watu watatu wameuawa na polisi na mmoja ndugu zake wameacha mwili wake mpaka jana hawajauzika wakitaka uchunguzi huru.

Kauli hiyo ilifanya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kusimama na kusema Sugu anatoa tuhuma nzito kwa polisi ambazo hawezi kuzithibitisha, hivyo afute tuhuma hizo.

“Watu wanaanza kushangaa wanaotukana polisi, wakati polisi wangu wako huku ndani, naomba mchangiaji badala ya kujikita kusema polisi wanaua, nikimwambia alete taarifa sijui atafanyaje...” alisema Lugola.

Akijibu hilo, Sugu alisema, “Wewe mwenyewe (Lugola) ni mmoja wa waliopata sintofahamu ya awamu ya tano, ulipigwa kesi ya rushwa sijui iliishia wapi.” Kauli hiyo iliibua shangwe kutoka kwa wabunge wa upinzani. Naye Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema katika mipango iliyoletwa na Serikali haijazungumza kuhusu nyongeza ya mishahara ambayo ndiyo husaidia mipango ya kuongeza ufanisi katika maendeleo.

“Waziri (Philip) Mpango na Serikali yenu leo mnaleta propaganda, watu wanaishi maisha magumu sana tukizungumza ukweli ninyi mnaligeuza jambo linaonekana baya kwa jamii.

“Waziri wewe unaishi maisha mazuri, kama ni mzalendo ni pamoja na wewe kuishi maisha ya kimaskini kama wengine, lakini unaendesha gari zuri VX na unaishi kwenye nyumba nzuri, anza basi wewe kutuonyesha mfano, tuonyeshe huo mfano wa uzalendo wewe huutaki huo uzalendo?” alihoji Heche.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Munde Tambwe alisema viongozi wa Serikali ya awamu ya tano akili zao zimezidi, ndio maana wamefanya mambo ya maendeleo.

Aliwataka wabunge wanaodai Serikali haikutoa ajira wamuogope Mungu kwa sababu katika tovuti ya utumishi kuna ajira nyingi zinatangazwa.

Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga alimuomba Spika Job Ndugai kufanya sherehe ndogo ya kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanazozifanya.