Manara akamatwa Dar, ahojiwa tukio la kutekwa Mo Dewji

Muktasari:

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amekamatwa na polisi kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’


Dar es Salaam.  Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amekamatwa na polisi kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Manara alikamatwa jana jioni na kuachiwa kabla ya leo asubuhi Oktoba 12, 2018 kukamatwa tena na polisi.

Akithibitisha kukamatwa kwa Manara, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Manara anashikiliwa kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia, jambo ambalo si kweli.

Mpaka saa 9:55 alasiri ya leo Ijumaa Oktoba 12, 2018, Mo Dewji ametimiza saa 34 tangu alipotekwa Alhamisi asubuhi katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40 alitekwa na Wazungu wawili waliomvizia alipokuwa akishuka kwenye gari lake ili aingie kwenye mazoezi kwenye gym ya Hoteli ya Colosseum.

Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.

“Manara tunamshikilia kwa uchunguzi zaidi yeye amekuwa akisambaza taarifa mbalimbali za tukio hili kwenye mitandao ya kijamii kwa madai kuwa ametumwa na familia, lakini sio kweli, hajatumwa na familia hivyo tunamshikilia,” amesema Kamanda Mambosasa.

Mapema jana Manara alinukuliwa  akisema taarifa ya Mo kupata matatizo imemshtua kila mmoja na kwamba bado wanaliachia jeshi la polisi kufanya kazi ya kumpata mwekezaji wao.

“Wanasimba wawe watulivu wakiliachia jeshi la polisi kufanya kazi yake na kwamba wanaamini MO atapatikana akiwa hai,” alisema Manara.