VIDEO: Manispaa ya Kinondoni yaanza usajili wa vitambulisho vya taifa kwa wenye ulemavuManispaa ya Kinondoni yaanza usajili wa vitambulisho vya taifa kwa wenye ulemavu

Mlemavu wa viungo Elia Selemani akisajiliwa ili apatiwe kitambulisho cha taifa katika shughuli yabusajili wa vitambulisho hivyo manispaa ya Kinondoni.

Muktasari:

Watu wenye ulemavu watapewa vitambulisho vya taifa ili kuwasaidia kupata huduma muhimu na za msingi wanazokosa kwa kutokuwa na vitambulisho vya taifa.

Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni imeanza usajili wa vitambulusho vya taifa kwa watu wenye ulemavu baada ya kubaini kundi hilo hukosa huduma nyingi za msingi kwa kutokuwa na vitambulisho.

Akizindua usajili huo katika viwanja vya shule ya msingi Ndugumbi, leo Septemba 2, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo amesema utafanywa kwa siku tatu ukihusisha makundi yote ya walemavu.

“Zipo huduma nyingi ambazo wenzetu hawa wamekuwa wanakosa kwa sababu ya ulemavu wao, niwaombe tu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha," amesema Chongolo.

Amesema pia uandikishaji huo utapunguza usumbufu na ucheleweshaji wa baadhi ya huduma kwa wenye ulemavu.

Awali Ofisa Msajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Manispaa ya Kinondoni, Dickson Mbanga amesema kwa walemavu ambao.  hawataweza kufika kwenye usajili huo umeandaliwa utaratibu wa kuwafuata nyumbani.

"Tumeandaa utaratibu maalum kwa ajili yao tunataka kuona kila mlemavu anapata kitambulisho hiki kwa sababu ya umuhimu wake hasa kwenye huduma nyingine za msingi kama matibabu na mikopo," amesema Mbanga.

Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulamavu Manispaa ya Kinondoni, Subira Semsimbazi amesema pamoja na kusaidiwa usajili huo bado zipo changamoto nyingi zinazowakabili.

“Mkuu tunaomba tupate nafasi kukaa nawe tukuelezee changamoto zetu nyingi ambazo naamini zinaweza kutatuliwa kama ilivyofanyika kwenye hili la kitambulisho," amesema.