VIDEO: Mavunde azungumzia ajira ya Mkenya Vodacom

Mavunde alisema waombaji wakishakamilisha taratibu hupata ndani ya siku 14.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde 

BY Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

Mavunde alisema waombaji wakishakamilisha taratibu hupata ndani ya siku 14.

Advertisement

Dare es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde amezungumzia kuchelewa kwa kibali cha kazi cha mkurugenzi mtendaji mpya wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom raia wa Kenya, Sylvia Mulinge aliyeteuliwa kushika wadhifa huo Aprili na kusema Serikali inashughulikia suala hilo.

Mulinge aliteuliwa kurithi mikoba ya Ian Ferrao aliyetangaza kustaafu baada ya mkataba wake wa miaka mitatu kufika tamati na ilikuwa akabidhiwe ofisi kati ya Juni Mosi na Agosti 31.

Akizungumza jana katika mahojiano maaalumu na Mwananchi, Mavunde alisema suala hilo limeshafikishwa kwa kampuni ya Vodacom.

“Katika taratibu hizo niweke wazi kwamba, hata wahusika wenyewe walihusishwa yaani Vodacom, kwamba suala hili linafanyiwa kazi, likikamilika taarifa itatolewa,” alisema Mavunde.

Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu wa kutoa vibali vya wageni kufanya kazi nchini, Mavunde alisema waombaji wakishakamilisha taratibu hupata ndani ya siku 14.

“Katika mfumo wa utoaji wa vibali vya kazi, kwa hivi sasa tumeweka utaratibu mzuri ambao mtu yeyote akikidhi mahitaji ya kinachopaswa kuwasilishwa, kibali hakiwezi kuchelewa kwa siku 14. Ndani ya siku hizo hupata majibu kama amekubaliwa au amekataliwa,” alisema Mavunde.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto ya waombaji kutopeleka mahitaji yote na hata orodha zinapotoka hawafuatilii.

Alisema kwa sasa wizara yake inafanya mazungumzo na Idara ya Uhamiaji ili kuanzisha utaratibu wa maombi kwa njia ya kielektroniki ili kurahisisha biashara na uwekezaji.

“Kikubwa ni uombaji wa vibali kielektroniki, wanasema ‘E-permit’, ili isichukue muda mrefu na kupunguza mawasiliano kati ya mwombaji na watu wetu. Iwe ni ‘online’ tu (katika mtandao). Mtu aombe hukohuko, majibu ayapate hukohuko,” alisema na kuongeza:

“Lengo ni kukuza urahisi wa kufanya biashara kwa sababu tunatambua katika nchi yetu moja ya changamoto ni urahisi wa kufanya biashara.”

Akizungumzia suala la ajira kwa vijana, Mavunde alisema kuna changamoto kubwa ya uchache wa nafasi za ajira huku idadi ya waombaji ikiwa kubwa.

Hata hivyo, alisema katika utawala wa Awamu ya Tano, Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukosefu wa ajira ikiwa ni pamoja na sera ya Tanzania ya viwanda.

“Hapa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais John Magufuli kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kufanikisha upatikanaji wa ajira,” alisema.

Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni ujenzi wa viwanda ili kutengeneza mazingira wezeshi ya ajira na biashara.

Mingine ni kupitia miradi mikubwa kimaendeleo kama ujenzi wa miundombinu ya kama barabara, reli na miradi ya ujenzi inayotoa fursa kwa vijana wengi kupata ajira na kilimo.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept