Mawakili wa Maua Sama, Shafii wakimbilia Mahakama Kuu

Muktasari:

TLS kutoa mawakili kuwasaidia kupata haki yao

Dar es Salaam. Wakati mwanamuziki Maua Sama, watangazaji Soudy Brown, Shaffi Dauda, msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na watuhumiwa wengine watano wa makosa ya mtandao wakiendelea kusota rumande kwa zaidi ya saa 100, mawakili wao wameamua kupeleka maombi Mahakama Kuu ili kuwanasua.

Uamuzi huo umekuja baada ya kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kudai kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Mambosasa alisema upelelezi haujakamilika kwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wapo Dodoma inabidi wasafirishwe kuunganishwa na wenzao katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, wakili Jebra Kambole alisema watafungua kesi Mahakama Kuu ili wateja wake waweze kupewa dhamana au kufikishwa mahakamani.

“Sheria ipo wazi huwezi kumshikilia mtuhumiwa zaidi ya saa 24 bila kumpeleka mahakamani, wateja wetu wameshikiliwa zaidi ya saa 100,” alisema Kambole.

Alisema kama upelelezi wa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani haujakamilika, sheria inaruhusu kupewa dhamana wakati upelelezi ukiendelea.

Naye wakili Fredrick Kihwelo anayemtetea Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene aliyeshikiliwa kwa zaidi ya saa 72, alisema mteja wake amenyimwa dhamana kwa madai ya kukamilisha upelelezi.

“Jana (juzi) nimefuatilia na leo (jana) tena nimekuja polisi wanasema wanakamilisha upelelezi kwaajili ya kuwafikisha mahakamani,” alisema Kihwelo na kuongeza:

“Hata kama wanakamilisha upelelezi mtuhumiwa ana haki ya kupata dhamana akiwa polisi hivyo nimeshaandaa maombi ambayo nitayawasilisha Mahakama Kuu.”

Wengine wanaoshikiliwa ni Antony Luvanda maarufu Mc Luvanda, Michael Mlingwa maarufu Mx Carter, meneja wa Maua Sama, Fadhili Kondo.

Akizungumzia kukamatwa kwao, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema: “Sio kosa la jinai kutoheshimu fedha. Noti ya fedha siyo binadamu hadi uiheshimu.”

Alisema kosa la jinai ni pale mtu ameitumia hiyo fedha vibaya kama kuichana, kuifanya ipoteze uhalisia wake lakini kuidharau au kutoiheshimu siyo kosa.

“(Kifungu walichokitumia) Hakisemi kwamba kudharau, kutoheshimu ni kosa la jinai,” alisema Fatma huku akidokeza kwamba TLS itatoa mawakili wa kuwasaidia waliokamatwa kupata haki ya kisheria.

Fatuma anaungwa mkono na wakili wa kujitegemea, Ambrose Nkwera aliyesema, “Kama mtu atatumia kwa nia mbaya noti ya fedha kwa kuichana au kuiharibu atakuwa ametenda kosa la jinai.”

Nkware alisema suala la kudharau au kutoheshimu noti ya fedha si kosa la jinai.