VIDEO: Mbowe: Chadema haitashiriki uchaguzi Liwale, udiwani kata 37

Muktasari:

Chadema kimedai uchaguzi wa Septemba 16, 2018 uliofanyika kwenye majimbo ya Monduli na Ukonga uligubikwa na ubakaji wa demokrasia ikiwamo wakurugenzi kutumika kukwamisha urudishaji wa fomu, mawakala kuzuiliwa kwenye vituo vya kupigia kura na watendaji wa Serikali kutumika kwenye kampeni pamoja na kutoa ahadi za maendeleo kwa wananchi wa maeneo zilipofanyika chaguzi hizo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kwa sasa chama hicho hakitashiriki chaguzi ndogo za udiwani na ubunge ukiwamo wa Liwale na udiwani kwenye kata 37 kwa kigezo kwamba kumekuwa na uvunjifu wa sheria katika mfumo mzima wa uchaguzi.

Mbowe amesema hayo leo Septemba 19, 2018 alipokuwa akiwasilisha uamuzi wa kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana jana kutafakari yaliyotokea kwenye chaguzi ndogo za ubunge za Ukonga, Monduli na kata 23 uliofanyika Jumapili iliyopita ya Septemba 16, 2018.

Mbowe amesema hujuma za uchaguzi huanza mapema katika hatua za kupata wagombea ambapo wakurugenzi wanatumika kubaka demokrasia ya nchi.

Amesema kwenye uchaguzi uliopita wakurugenzi walitumika kuhakikisha wagombea wa chama tawala wanapita bila kupingwa.

"Walikuwa wanafunga milango wanaondoka, muda ukiisha wanatangaza mgombea wa Chadema hakurudisha fomu hivyo wa CCM amepita bila kupingwa" amesema Mbowe.

“Kwa sasa tunakwenda kufanya mabadiliko ndani ya chama, tunakwenda kujijenga na hatuwezi kushiriki wakati tunaonewa na sheria hazifuatwi. Kwa sasa tunarudi nyuma,” ameongeza:

Amesema kumekuwa na tatizo kubwa la wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kutotambulika mapema huku suala hilo likifanyika kwa makusudi maalumu.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema kwenye Jimbo la Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura 700,000.

Amesema kuna mambo ya kibatili yalifanyika kwenye uchaguzi wakitoa matamko na kutoa ahadi kwa wananchi wakati wa kampeni wakitumia magari ya Serikali.

"Tumewaona mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Waziri wa Ardhi William Lukuvi na wengine wengi wakifanya kampeni ilhali ni watendaji wa Serikali" amesema Mbowe.

Amedai wasimamizi wa uchaguzi katika vituo vya wapiga kura ambapo mawakala walizuiliwa kuingia, walitumika kupiga kura.