Mbowe, upande wa mashtaka watoana jasho mahakamani

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa nini asifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti huku upande wa mashtaka ukiweka vielelezo mbalimbali kuonyesha dharau ya washtakiwa wote

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anaiheshimu sana Mahakama na anatambua kama kiongozi na kama raia nafasi ya Mahakama katika kusimamia haki kwenye taifa.

Amesimama mahakamani hapo leo Jumatatu Novemba 12, 2018 Saa 5:51 asubuhi kuieleza Mahakama hiyo kwa nini isimfutie dhamana baada ya kusafiri nje ya nchi bila kibali.

Mbowe ameieleza Mahakama hiyo kuwa ni ukweli usiopingika kuwa yeye na washtakiwa wenzake ni viongozi na wana majukumu mengi ya kiuongozi ya kutenda ndani na nje ya nchi.

"Imani yangu mheshimiwa hakimu, mwenendo wote wa Mahakama hii unatupa ugumu wa kubalansi heshima yetu kwa Mahakama na majukumu yetu nje ya Mahakama," ameeleza Mbowe mahakamani hapo.

“Oktoba 25, mwaka huu nilikuwepo mahakamani wakati huo kamati za bunge zilikuwa zikiendelea na leo Novemba 12 mwaka huu tupo katika Mahakama yako wakati Bunge likiendelea na kwamba siku hiyo Mahakama iliipanga kesi hiyo kuendelea Novemba Mosi mwaka huu,” ameongeza.

Mbowe ameIeleza Mahakama kuwa Oktoba 28, 2018 alisafiri kwenda Washington DC nchini Marekani kwenye mkutano wa Oktoba 30, 2018 na kwamba kwa ratiba yake alistahili kuondoka huko Oktoba 30, usiku na kurejea Dar es Salaam Oktoba 31 kwa ajili ya kuendelea na kesi Novemba Mosi, 2018.

Mshtakiwa huyo wa kwanza katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka huu, Mbowe amedai kabla hajaanza safari hiyo alipata matatizo ya ugonjwa na kwamba kwa mazingira aliyokuwepo haikumruhusu kusafiri safari ndefu ya ndege kwa ushauri wa kitabibu na miiko ya kinachomsumbua.

Amedai jitihada za kujaribu kupata matibabu nchini Marekani zilikwamishwa na bima yake ya matibabu ya kimataifa kwa sababu ilikuwa inaruhusu matibabu katika nchi ambazo si Marekani wala Ulaya bali inaruhusu atibiwe kati nchi za Afrika Mashariki, Afrika Kusini na Dubai.

Mbowe amesema kwa misingi hiyo ilimlazimu kutafuta ‘apointiment’ kwenda kwenye matibabu katika nchi za Emirates na kwamba hiyo ni kutokana na ushauri aliopewa mbali na bima, kutokana na utofauti wa saa kati ya tano iwapo atatoka alipo kwenda Dubai kwa matibabu na ni zaidi ya 24 iwapo angekuwa nchini .

Amedai alikwenda Dubai ambako aliweza kupata matibabu na amepewa mapumziko hadi atakaporejea tena huko kwenye matibabu Novemba 17, 2018.

Amedai licha ya kupewa mapumziko na wakati akisubiri kurejea katika matibabu yake Novemba 17, 2018 aliona taarifa mbalimbali zenye kupotosha kuhusiana na ugonjwa wake na matibabu anapopata kwa ujumla.

Pia, akaona Mahakama ilivyokwazika kutokana na kutokuwepo kwake na kwamba haikuwa rahisi kwa yeye kutuma taarifa za matibabu kwa sababu bado wanaendelea na matibabu na kwamba taarifa ya ugonjwa ni siri ya mgonjwa na daktari.

Pia, ameiarifu Mahakama kuwa alipatwa na msiba wa ndugu yake ambao ulifanyika nyumbani kwake Hai Kilimanjaro. “Hivyo niliondoka Dubai Novemba 9, 2018 kwenda Nairobi na hatimaye kwenda Hai Kilimanjaro kuhudhuria mazishi hayo.” Amesema.

Ameomba kuweka kumbukumbu mahakamani hapo kuwa yeye ni mgonjwa wa moyo kwa miaka mingi na kwamba magonjwa wa moyo si homa na wala si ugonjwa wa majeraha ndiyo sababu Wazungu wanauita "Silent Killer' ni ugonjwa ambao unastahili uangalizi.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amesema anawasilisha nyaraka zake za safari, za matibabu, bima ya matibabu kama uthibitisho mahakamani hapo.

Baada ya Mbowe kueleza hayo, Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori amedai amemsikiliza Mbowe kwa umakini akiishawishi Mahakama isimfutie dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Nyantori amedai washtakiwa hao Mbowe na wenzake ni kama washtakiwa wengine wowote na kwamba kwa mujibu wa hati ya mashtaka inayowakabili walipaswa kufuata taratibu za Mahakama na masharti ya dhamana na amri walizopewa.

Walipewa dhamana Aprili, 2018 walitakiwa kufika mahakamani bila ya kukosa na kuripoti Polisi Ijumaa ya kila wiki.

Nyantori amedai kutokufika mahakamani kutokana na kazi za kibunge, ubunge ni mhimili kama ulivyo mhimili wa Mahakama hivyo kwa kuwa washtakiwa wameshtakiwa kwa kesi ya jinai ratiba zao zinatakiwa kuendana na ratiba za Mahakama.

Wakili huyo wa Serikali aliendelea kudai kuwa mdhamini wa Mbowe wakati akitekeleza jukumu lake la udhamini alieleza kuwa Mbowe alikuwa mgonjwa mahututi na alikimbizwa Afrika Kusini kwa matibabu. Na kwamba kwa maneno ya mdhamini hali aliyokuwa nayo hakuweza hata kuzungumza.

Nyantori amedai Mahakama ilichukua maneno hayo katika kumbukumbu za Mahakama na kuahirisha Kesi hadi Novemba 8, 2018 huku ikieleza uthibitisho wa kuumwa kwa Mbowe upelekwe mahakamani hapo.

“Leo Mbowe anatueleza alikwenda Washington DC badala ya Afrika Kusini na kwamba anatibiwa Dubai. Hii inaonyesha udanganyifu kutokana na kutofautiana kwa mshtakiwa na mdhamini wake,” ameeleza Nyantori.

Hata hivyo Nyantori  ametoa hati ya kusafiria ya Mbowe akionyesha kuwa Novemba 7, 2018 alikuwa Dubai na alitibiwa Novemba 8, 2018. Pia, amedai Novemba 2, 2018 Mbowe alikuwa Brussles Ubelgiji ambapo alitoka Novemba 6, 2018 kwenda Dubai.

Nyantori amedai wanaonyesha hayo kwa sababu ya kuionyesha Mahakama mshtakiwa alikuwa anaumwa anatibiwa Dubai.

Pia wakili hiyo kuiwasilisha hati ya kiapo kutoka kwa kamanda wa polisi mkoa wa Ilala Kamishna Msaidizi Salum Hamduni ambaye washtakiwa walipewa jukumu na Mahakama kuripoti kwake kila Ijumaa ya kila wiki.

Katika viapo hivyo, wakili huyo amedai mshtakiwa wa kwanza na wenzake hawakwenda kuripoti Polisi kama walivyotakiwa na Mahakama wakati walipewa masharti ya dhamana.

Pia, kuwasilisha kiapo cha Kamanda wa Uhamiaji, Steven Mhina ambaye alimhudumia Mbowe wakati akianza safari na kwamba amedai siku hiyo Mbowe alikuwa mzima na hakusindikizwa na wala hakuwa na msaada wa mtu yeyote.

Amedai kamanda Mhina alimhoji Mbowe kuwa anasafiri kwa ajili ya kufanya nini na kwamba akamueleza kwa mapumziko.

Viapo hivyo vimewasilishwa mahakamani hapo pamoja na kiapo cha wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango.

Baada ya kueleza hayo, Wakili Nyantori ameiomba Mahakama iwafutie dhamana washtakiwa wote kwa sababu za uvunjifu wa masharti ya dhamana. Sheria ichukue mkondo wake na shauri liendelee kusikilizwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kilichojiri