Mbuzi wawili watumika kwa kisomo cha mfanyabiashara Mo Dewji aliyetekwa Tanzania

Muktasari:

Viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba wametumia mbuzi wawili kusoma dua ya kumuombea mfanyabiashara Mohammad Dewji 'Mo Dewji’


Dar es Salaam. Viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba wakiwa na mbuzi wawili wameingia katika ukumbi wa makao makuu ya klabu ya Simba tayari kwa kusoma dua ya kumuombea mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo Dewji’ apatikane akiwa salama.

Mfanyabiashara huyo alitekwa jana alfajiri Oktoba 11, 2018 jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay alipokwenda kwa lengo la kufanya mazoezi.

Mapema leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 uongozi wa klabu ya Simba ulitangaza uamuzi wa kufanya kisomo saa 8 mchana baada ya sala ya Ijumaa makao makuu ya Simba, Msimbazi kwa ajili ya kumuombea Dewji aliyetekwa na watu wasiojulikana.

Tayari mchana huu mwitikio umekuwa mkubwa kwa watu kujitokeza kwa wingi huku mjadala ukiwa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na MCL Digital wamesema amefunga kuhakikisha bilionea huyo anarejea na kuungana na familia yake.

"Jamani Dewji ni mtu wa watu, Mungu amkumbuke na kumuepusha na maswahiba, yaani mpaka tunashindwa kufanya vitu muhimu,” amesema mmoja wa wanawake hao.