Mdee atajwa kuugua kortini, bungeni yupo

Muktasari:

  • Jana asubuhi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, lakini mshtakiwa hayupo.

Dar/Dodoma. Wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikishindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Halima Mdee kwa sababu anaumwa, mbunge huyo wa Kawe (Chadema) jana alionekana bungeni.

Jana asubuhi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, lakini mshtakiwa hayupo.

Baada ya Kishenyi kueleza hayo, mdhamini wa Halima Mdee, Fares Robinson aliieleza mahakama kuwa anaumwa.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, aliipanga kesi hiyo Oktoba 8, siku ambayo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi wao.

Katika kesi hiyo, mashahidi wawili wa upande wa mashtaka tayari wamekwishatoa ushahidi wao ambao ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Batseba Kasanga.

Mdee anakabiliwa na kesi ya uchochezi akidaiwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni alitoa maneno kuwa Rais John Magufuli “Anaongea hovyohovyo, anatakiwa afungwe breki,” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, wakati Mahakama ikielezwa Mdee ni mgonjwa, jana asubuhi alikuwa bungeni na kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge, aliwasilisha taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa mwaka 2018.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu kukamilika kwa Serikali na kamati ya Bunge ya Bajeti kusoma taarifa zao za Muswada huo, Mdee naye aliwasilisha taarifa ya upinzani.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada huo, alisema baada ya sera ya ujamaa kushindwa, uchumi duniani unaendeshwa na nguvu ya soko na sasa sekta binafsi ni mdau muhimu.

“Kulazimisha kutumia mbinu za kijamaa katika zama hizi kwa Serikali kutaka kukumbatia kila kitu ni kujitoa ufahamu na ni jambo lisilowezekana,” alisema Mdee ambaye ni waziri kuvuli wa Fedha na Mipango