Busungu ajiweka mtegoni Yanga

Thursday December 1 2016

 

By Olipa Assa, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Yanga, Malimi Busungu ameeleza kufurahia ujio wa kocha mpya, George Lwandamina na kuahidi kurudisha makali yake.

Busungu aliyekuwa majeruhi na kukaa benchi kwa muda mrefu chini ya kocha Hans Pluijm alisema umefika wakati kwake kupata namba kwenye kikosi hicho cha Mzambia.

Lwandamina amepokea mikoba ya Pluijm aliyepandishwa cheo kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Hata hivyo, kilichomkuta Busungu kabla ya kuanza mazoezi juzi kimemshangaza kama si kumkatisha tamaa.

Aliliambia gazeti hili: “Sijui nimekumbwa na nini, maana nilikuwa nimepania siku ya kwanza kuanza mazoezi na kocha (Lwandamina) baada ya kukosa namba chini ya Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi.”

Alieleza kwamba alipata ajali akienda Dodoma, alipofika Dumila, Morogoro alionekana ndiye aliyekuwa na makosa, hivyo akapelekwa polisi.

“Niliripoti polisi, nimeambiwa nitaarifiwa siku ya kusomewa mashtaka, hii inanichanganya kiasi kwamba ninaweza kuanza kazi nikiwa na mawazo mengi kichwani,” alisema.

Busungu anayetarajiwa kujiunga na timu yake leo, alisema anaona kama atakuwa kwenye changamoto ya ushindani kutokana ujio wa kocha huyo mgeni.

Advertisement