LIGI KUU: Tambwe aipaisha Yanga, Simba yashikwa

Sunday December 20 2015

Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma (kushoto) 

Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma (kushoto)  akimtoka beki wa Stand United, Nassoro Said Chollo wakati wa mchezo wa  Ligi Kuu uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Picha na Said Khamis. 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar/Mikoani. Baada ya ukame wa mabao katika michezo miwili mfululizo, mshambuliaji Amissi Tambwe jana alifunga mabao matatu ‘hat trick’ ya kwanza msimu huu na kuisaidia Yanga kupata ushindi  mnono wa mabao 4-0 na kuendelea kuongoza ligi kwa kufikisha pointi 30.

Kwa mabao hayo, Tambwe  amefikisha mabao manane msimu huu na hivyo kuchochea kasi ya kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu baina yake na kina Elius Maguli wa Stand mwenye mabao tisa, Donald Ngoma (Yanga) na Hamis Kiiza (Simba) wenye mabao manane na Kipre Tchetche wa Azam aliye nacho sita.

Wakati Yanga wakipata ushindi huo mnono, mahasimu wao wa jadi, Simba walishindwa kulinda bao lao la mapema na kuwaruhusu wapinzani wao, Toto Africans ya Mwanza kusawazisha bao dakika za nyongeza za mchezo  huo. 

Katika mchezo  uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Tambwe alianza kuifungia Yanga bao dakika ya 18 akimalizia kazi nzuri  ya Thaban Kamusoko aliyemhadaa kipa wa Stand, Frank Muwonge na kumpasia mfungaji.

Tambwe aliipatia tena Yanga bao la pili dakika ya 36, akiunganisha vizuri krosi safi iliyopigwa na Juma Abdul kabla ya kufunga bao la tatu, dakika ya 45 akipokea pasi ya Ngoma.

Kiungo Kamusoko aliyeipa timu yake ushindi mjini Tanga Jumatano dhidi ya African Sports alihitimisha karamu ya mabao kwa  timu yake baada ya kufunga bao la nne kwa kichwa dakika ya 62, akipokea krosi ya Juma  Abdul.

Katika mchezo huo ambao Yanga walitawala kwa kiasi kikubwa kwa muda wote wa mchezo huku wapinzani wao Stand United wakicheza kwa kujihami zaidi, jambo lililowakosesha ushindi.

Stand  ilifanya mashambulizi mawili langoni  mwa Yanga kupitia kwa Haruna Chanongo, dakika ya 41 baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga na kupiga shuti kali lililogonga mwamba na kumkuta kiungo Amri Kiemba aliyeunganisha kwa kupiga mpira na kuokolewa na mabeki.

 Dakika ya 20, Jacob Massawe wa Stand alionyeshwa kadi ya njano kwa kubishana na mwamuzi huku kiungo wa Yanga, Said Juma ‘Makapu’ naye  akionyeshwa pia kadi ya njano kwa  kumchezea rafu Massawe.

Hata hivyo,  baadaye mchezaji wa Stand Jeremiah Katula aliyeingia kipindi cha pili badala ya Maguli alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko Tambwe.

Kirumba, Mwanza

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Toto Africans kwenye mchezo uliokosa ufundi kutokana na uwanja kujaa maji na kusababisha utelezi mwingi ulioathiri mchezo huo.

Simba  ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa Daniel Lyanga,  lakini Toto walisawazisha dakika za nyongeza kupitia kwa Evarist Bernard na hivyo kuifanya Simba kufikisha pointi 23 na kubaki nafasi ya nne.                                                                                                            

Kabla ya mchezo huo mashabiki wa Simba na Toto nusura wachapane makonde baada ya  mwanachama mmoja wa Simba aliyefahamika kwa jina moja la Idrissa kuingia kwenye benchi la ufundi la Toto na kuchukua vifaa vyao jambo lililowafanya mashabiki  wa Toto kumcharukia na kutaka kumpiga kabla ya kuokolewa na Polisi.

Ilielezwa uwanjani hapo kuwa mwanachama huyo alijichanganya alipoona vifaa vya Toto vilivyokuwa na rangi nyekundu ndipo alipotaka kuvichukua akidhani ni vya Simba.

Shinyanga

 Kwenye Uwanja wa Mwadui,  Shinyanga,wenyeji mwadui waliichapa Ndanda ya Mtwara mabao 2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na wakongwe Jerry Tegete na Jabir Aziz.

Tabora

Nako kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, wenyeji Kagera Sugar walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Sports ya Tanga, bao la washindi lilifungwa na beki Salum Kanoni kwa penalti, dakika ya 17.

Mbeya

Kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Prisons ambayo wiki iliyopita iliaibishwa na JKT Ruvu kwa kufungwa mabao 4-1, ilitoshana nguvu na Mtibwa Sugar baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana.

Ligi hiyo inaendelea leo kwa mechi baina ya Majimaji ya Songea dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Majimaji,  JKT Ruvu dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, pia kwenye Uwanja wa Sokoine, Mgambo JKT watakuwa wageni wa Mbeya City.

Imeandikwa na Charles Abel (Dar),Saddam Sadick (Mwanza), Robert Kakwesi (Tabora),Godfrey Kahango (Mbeya) na Masoud Masasi (Shinyanga)

Advertisement