Mavugo ndani, Majwega atimka

Laudit Mavugo

Muktasari:

Mavugo aliwasili Dar es Salaam juzi na kukutana na viongozi wa Simba baada ya mazungumzo yao amekubali kusaini mkataba huo wa kuitumikia timu hiyo kwa kipindi hicho.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo (pichani) amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba.

Mavugo aliwasili Dar es Salaam juzi na kukutana na viongozi wa Simba baada ya mazungumzo yao amekubali kusaini mkataba huo wa kuitumikia timu hiyo kwa kipindi hicho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema Mavugo anaanza kuutumikia mkataba wake aliosaini msimu uliopita, lakini wakashindwa kufikia mwafaka na mabosi wake wa Vital O.

“Tulisaini naye mkataba lakini baadaye ikatokea mvutano na mabosi wake, ujio wake sasa ni muendelezo wa mkataba baina yake na Simba aliosaini msimu uliopita,” alisema Hanspope.

Msimu uliopita, Simba ilimtaka Mavugo na kumtangulizia Dola 10,000, lakini uongozi wa Vital O ulikataa ukitaka Dola 100,000 ilikumwachilia mshambuliaji huyo.

Wakati Mavugo akisaini Simba, Mganda Brian Majwega aliyetimuliwa yuko mbioni kujiunga na klabu ya Vipers inayoshiriki Ligi Kuu Uganda.

Vipers inapewa nafasi kubwa ya kumsajili Majwega aliyemaliza mkataba wake na Simba hivi karibuni.

“Uhamisho wake utakamilika wiki ijayo mambo yakienda sawa,” rafiki wa karibu wa mchezaji huyo aliuambia mtandao wa Kawowo Sports. “Atasaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola15,000,” aliongeza.

Kama uhamisho huo utakamilika Majwega atakutana na kocha wake wa zamani wa KCCA na Azam, George ‘Best’ Nsimbe.