Simba, Yanga mtegoni Ligi Kuu

Saturday September 24 2016

 

By Charles Abel, Oliver Albert [email protected]

Dar es Salaam. Ni Jumamosi yenye mitego kwa timu za Ligi Kuu zitakaposhuka viwanja vitano tofauti nchini ili kusaka pointi tatu muhimu.

Wakati ligi hiyo ikiingia mzunguko wa sita, mechi za leo na kesho zina uwezekano wa kuweka sawa mambo au kuyatibua kwa baadhi ya timu.

Mtego hatari upo kwa Simba na Yanga, ambazo baada ya mechi za leo na kesho, zinatarajia kukutana, Oktoba Mosi.

Ingawa pasipo shaka, mawazo na mkazo kwa timu hizo mbili upo kwenye mechi baina yao wiki ijayo, matokeo ya michezo yao leo na kesho, yataziweka kwenye mtihani.

Yanga ipo Shinyanga kuikabili Stand United kesho, ni lazima iibuke na ushindi ili ijiweke sawa kisaikolojia kabla ya mechi ya Jumamosi, pia ushindi utaisaidia kuing’oa Simba kileleni mwa msimamo wa ligi zinapokutana wiki ijayo.

Mabingwa hao watetezi, wanapaswa kuwa makini na Stand yenye wachezaji walioahidi kuweka pembeni matatizo yao, kuhakikisha wanazoa pointi tatu muhimu.

Yanga ilipiga kambi mkoani Shinyanga, huku ikitajwa kuwa tayari viongozi na wanachama waandamizi wameshatua huko ili kuhakikisha wanavuna pointi tatu kesho.

“Tunaiheshimu Stand kwa sababu ni timu nzuri na ina kocha mzuri. Tupo ugenini ambako kwa hali halisi hatutoweza kucheza soka letu la siku zote, ila tunachokizingatia ni kupata pointi tatu,” alisema kocha Hans Pluijm.

Kocha msaidizi wa Stand, Athuman Bilali ametamba kuwa timu yake haina hofu kwa Yanga, ingawa wanaiheshimu.

Simba itakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuikabili timu dhaifu ya Majimaji ambayo itaingia kwenye mchezo huo na nguvu mpya iliyotokana na udhamini mnono waliopata kutoka Kampuni ya GSM.

Ushindi kwenye mchezo wa leo utaisaidia Simba kuwa sawa kisaikolojia kuelekea kwenye mechi ya watani wa jadi.

Majimaji imekuwa jijini tangu juzi na mkwara mzito baada ya kuwekwa kwenye moja ya hoteli za kifahari, kufanya mazoezi kwenye viwanja vya kisasa vya Gymkhana pamoja na kuahidiwa kitita cha Sh10 milioni kutoka GSM iwapo itaibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.

“Timu imekuja Dar es Salaam kutafuta pointi tatu na siyo vinginevyo. Tumefanya maandalizi mazuri ambayo ni ishara kuwa tunataka kuanza ligi.

Tunafahamu kuwa tunakutana na Simba, inayofanya vizuri kwenye ligi na sisi tumeshapoteza mechi tano, hivyo ni lazima mechi hii tushinde, vinginevyo tutakuwa kwenye hali mbaya,” alisema meneja wa Majimaji, Godfrey Mvula.

Tambo hizo zimejibiwa na meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyesema kuwa timu bora uwanjani itapata matokeo.

“Kama wao wameamua kutoa tambo, basi kuna kitu kinachowapa jeuri, ila sisi tunachoamini ni kuwa kwenye soka, aliyefanya maandalizi mazuri ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

“Kikosi chetu kiko vizuri kwa ajili ya mchezo na tunawaomba mashabiki na wapenzi wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho (leo),” alisema Mgosi.

Mtego mwingine kwa Simba ni kumtumia mshambuliaji Ibrahim Ajib mwenye kadi mbili za njano, sawa na raia wa Ivory Coast, Frederick Blagnon.

Mchezaji huyo akipangwa leo, kisha akapata kadi ya njano, kikanuni atakosa mchezo wa Yanga, ambao ni wazi Simba inautolea macho kuliko hata huo wa leo.

“Naupa uzito sawa mchezo dhidi ya Majimaji kama ule tuliocheza na Azam au timu nyingine za Ligi Kuu. Suala la kumtumia au kutomtumia Ajib, litajulikana kesho (leo),” alisema kocha wa Simba, Joseph Omog.

Mjini Mtwara, Azam FC itakuwa ugenini kukabiliana na Ndanda katika mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Timu hiyo inayonolewa na Zeben Hernandez kutoka Hispania, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi yake dhidi ya Simba wiki iliyopita kwa bao 1-0 huku Ndanda ikishinda ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Majimaji.

“Mchezo uliopita (Simba) ulikuwa mzuri kwa timu yangu, tulikuwa bora mchezoni zaidi yao, lakini kwa kosa moja tulilolifanya wenzetu walilitumia kutufunga.

“Kwa sasa, ninachofanya ni kuwaweka sawa wachezaji wangu na muhimu kwangu kwa sasa ni kuilekeza akili yetu katika mchezo ujao na kuachana na habari za mchezo uliopita,” alisema kocha Hernandez.

Mechi nyingine zitakuwa: JKT Ruvu v Mbeya City, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi wakati Prisons v Mwadui, Sokoine, Mbeya, Mtibwa Sugar dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Manungu, Turiani.

Advertisement