Miss Tanzania afunguka kuhusu zawadi ya gari

Muktasari:

  • Shindano la Miss Tanzania lilifanyika, Septemba 8, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar es Salaam, ambapo mbali na mshindi kuondoka na gari la thamani ya Sh15 milioni pia alivishwa taji lililogharimu Sh40 milioni.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wadau wa masuala ya urembo wakiponda kuhusu zawadi aliyopewa mshindi wa Miss Tanzania, mwenyewe ajitokeza kufafanua kuwa sicho alichofuata katika mashindano hayo.

Akizungumza na MCL Digital leo Septemba 14,   mrembo huyo, Queen Elizabeth, amesema watu wanapaswa kufahamu kuwa hakwenda kushindana ili apate gari.

Pia amesema gari ambalo watu wanalilalamikia kuwa halina thamani ukilinganisha na ukubwa wa shindano hilo, hawana hoja kwani waandaaji wamejitahidi kwa uwezo wao na yeye ameridhika nalo.

“Gari nimelipenda na nimeridhika nalo. Isitoshe hata katika mashindano hayo kilichonipeleka sio gari,”amesema Queen Elizabeth ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo cha uhasibu(TIA).

 “Binafsi naona dada Basila kafanya jambo kubwa, kwani ni mashindano ambayo naweza kusema watu walikata tamaa, namuomba asife moyo na yasemwayo kwa kuwa huwezi kumridhisha kila mtu.

“Kikubwa tunachopaswa kufanya Watanzania tumuombee na kumpa ushirikiano aweze kufanya vizuri miaka inayokuja kwa kuwa Miss Tanzania ni mashindano ambayo yanayoibua vipaji vya wasichana na kuwapatia fursa mbalimbali za ajira,” amesema.

 Mshindi wa shindano hilo alivishwa taji lenye thamani ya Sh6 milioni.

Wakati kwa upande wa washindi walioingia tano bora, kila mmoja alilamba ajira ya kuwa balozi katika hifadhi za Taifa.