Mjumbe wa bodi MCL aagwa, aimwagia sifa Mwananchi -VIDEO

MJUMBE WA BODI MCL AAGWA, AIMWAGIA SIFA MWANANCHI

Muktasari:

  • Rweyemamu ametumikia nafasi ya ujumbe wa bodi ya MCL kwa miaka kumi kuanzia 2008 hadi 2017 akiwa mkurugenzi wa fedha na ukaguzi aliyeacha mafanikio.

Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), jana Jumatano Machi 21, 2018 wamemuaga mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo, Mohamed Rweyemamu aliyemaliza muda wake.

Rweyemamu ametumikia nafasi ya ujumbe wa bodi ya MCL kwa miaka kumi kuanzia 2008 hadi 2017 akiwa mkurugenzi wa fedha na ukaguzi aliyeacha mafanikio.

Akizungumza na wageni walioshiriki hafla hiyo jijini Dar es Salaam, Rweyemamu amesema huduma ya habari katika jamii inahitaji waandishi wenye weledi, ubora unaohitajika na ajenda zinazojikita katika kusaidia jamii.

Akisisitiza ujumbe wake amesema wananchi wana imani na mchango unaotolewa na vyombo vya habari, hivyo ni wajibu wa MCL kujiona kuwa ina nafasi kubwa ya kulinda heshima iliyojijengea kwa jamii.

“Kwanza naomba kushukuru kwa ushirikiano niliyoupata kwa wajumbe wa bodi, nashukuru pia MCL na NMG (Nation Media Group) kwa ushirikiano nilioupata,”amesema.

Akitoa ujumbe wake kwa bodi hiyo pamoja na MCL amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwa nyuma ya hisia zao wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Amesema  kampuni ya Mwananchi ambayo haifungamani na ajenda zozote za kisiasa ina nafasi kubwa ya kuanzisha zake kwa ajili ya kuendelea kuisaidia jamii.

Rweyemamu amesema ajenda zinazoweza kuibuliwa katika jamii ni pamoja na masuala ya kuendesha vita ya rushwa pamoja na changamoto ya elimu.

“Ubora wa kazi ni jambo muhimu sana, linalinda heshima ya chombo cha habari, ubora wa waandishi unaweza kusaidia katika ubora wa habari zinazoandaliwa, tunahitaji watu wanaofikiri sana,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amesema mchango wa Rweyemamu umekuwa na manufaa makubwa.

 “Kwa kampuni yoyote eneo la ukaguzi wa mahesabu lina umuhimu sana kwa sababu mwisho wa siku utashindwa kulipa kodi, utakosa kulipa mishahara ya wafanyakazi na utashindwa kuangalia maendeleo endelevu, kwa hiyo kwa mchango huo tunakushuruku sana mkurugenzi Rweyemamu,”amesema Nanai.

Nanai amesema kwa kutambua uwezo na uzoefu wake, alimuomba aendelee kutoa ushirikiano kwa kampuni pale itakapohitaji kumtumia.

Mkurugenzi wa Fedha wa NMG, Stephen Gitagama ambaye ni kaimu ofisa mtendaji mkuu wa NMG amesema Rweyemamu ametoa mchango mkubwa katika bodi hiyo tangu ilipokuwa ikipata hasara kabla ya kuanza kutengeneza faida.

NMG inachapisha magazeti ya Daily Nation na Taifa Leo nchini Kenya, The East African ambalo ni la kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Daily Monitor (Uganda),  Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ya Tanzania pamoja na matoleo ya kielektroniki.

Pia inamiliki vituo vya televisheni vya NTV Kenya, NTV na Spark pamoja, vituo vya redio vya KFM na Dembe nchini Uganda na Nation FM nchini Kenya.